27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI TISA WAUNGANA KUPINGA UKATILI

mawziri

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MAWAZIRI tisa wa wizara mbalimbali wameungana na kujifunga mkanda kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.

Mawaziri hao na wizara zao kwenye mabano ni Dk. Philip Mpango (Wizara ya Fedha na Mipango), Jenista Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Dk. Harrison Mwakyembe (Katiba na Sheria), Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Dk. Charles Tizeba (Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani ya Nchi).

Pia wamo manaibu waziri Annastazia Wambura (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Dk. Medard Kalemani (Nishati na Madini) na Stella Manyanya (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.

Mawaziri hao waliainisha mikakati yao jana wakati wa uzinduzi wa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ulioandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, utakaoanza kutekelezwa mwaka 2017 hadi 2022.

Tanzania ni kati ya nchi nne duniani na pekee Afrika iliyopata fursa ya kuwa katika kundi la kwanza la kuandaa mpango huo, ambao utagharimu Sh bilioni 267.4 hadi kukamilika.

Akizindua mpango huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema unalenga kuzuia aina zote za ukatili kwa wanawake na watoto kwa kuhakikisha wanafurahia haki ya kuishi bila kufanyiwa ukatili wa aina yoyote.

“Hatutaki uwe mpango ambao unaishia katika makaratasi kama mipango mingine tunayoiandaa, tunataka ikifika 2022 tumuonyeshe anayetoa fedha matokeo ya mpango huu,” alisema Ummy.

Alisema wataanzisha sehemu rafiki katika shule za msingi na sekondari ili mtoto atakapofanyiwa jambo baya la ukatili aweze kupata msaada wa haraka.

“Kutakuwa na kamati za ulinzi na usalama wa mtoto wa kike katika kila mtaa na kijiji, na pia utaanzishwa mtandao wa wanaume katika kila kata ili kulinda vitendo vya ukatili,” alisema.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango, alizitaka wizara, idara, taasisi za Serikali, mikoa na wilaya kutenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 ili kukidhi utekelezaji wa shughuli zilizopangwa.

Naye Waziri Mhagama alisema watatoa miongozo ya kisera katika uratibu na utekelezaji wa mpango huo, na kwamba anaamini utatoa matokeo chanya ndani ya muda uliopangwa.

Aliwaagiza waajiri kuhakikisha wanatoa ajira na ujira sawa kati ya wanawake na wanaume sehemu za kazi, ili kuondoa unyanyasaji na ubaguzi wa kijinsia.

Kwa upande wake, Waziri Mwakyembe, alisema wanaangalia uwezekano wa kubuni mchakato usio na gharama kubwa kwa lengo la kupata mwafaka wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo alikiri imepitwa na wakati.

Pia alisema Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na sheria za mirathi na urithi zitafanyiwa marekebisho ili kuondokana na upungufu wa kisheria uliopo sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles