33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mawakili wakata rufaa kesi ya bilionea Msuya

NA SAFINA SARWATT, MOSHI.

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi imeahirisha kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya, baada ya upande wa utetezi kukata rufaa kutokana na kutoridhishwa na uamuzi uliotolewa wa kutupilia mbali ombi lao la kutopokewa kwa maelezo ya mshtakiwa wa tatu.

Upande wa utetezi unaongozwa na jopo la mawakili wanne ambao ni Hudson Ndusyepo anayemwakilisha mshtakiwa wa kwanza, Majura Magafi anayewawakilisha mshtakiwa wa pili na tano, Emmanuel Safari anayemwakilisha mshtakiwa wa tatu na John Lundu anayewawakilisha washtakiwa wa nne, sita na saba.

Mawakili hao walikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo kutupilia mbali kesi iliyokuwa ndani ya kesi kwa madai mtuhumiwa wa tatu, Musa Juma, alikamatwa na kuteswa na polisi.

Upande huo uliendelea kudai kuwa, mtuhumiwa huyo hakuweza kutoa maelezo polisi, bali alishinikizwa kwa lazima kusaini maelezo ambayo si yake, huku akipigwa na kuingiziwa spoku katika tundu la mkojo.

Akitoa uamuzi wa kesi hiyo ndogo, Jaji Salma Maghimbi, alisema mahakama hiyo ilipata fursa ya kusikiliza ushahidi kwa pande zote mbili, na hakukuwa na kipingamizi kuwa mshtakiwa huyo wa tatu alikamatwa saa tano hadi saa saba za usiku mnamo Agosti 11, mwaka juzi.

Jaji Maghimbi aliendelea kudai kuwa kinachobishaniwa ni muda wa kukamatwa kwa mtuhumiwa na kufikishwa kituo cha polisi saa 10 au 11 alfajiri, na upande wa utetezi unadai kuwa toka kukamatwa kwa mtuhumiwa hadi kufikiswa polisi alikuwa akiteswa na kupigwa.

Alidai kuwa kama mtuhumiwa alipigwa na kuchanwa sehemu ya juu ya mdomo, kabla ya kutia saini katika maelezo aliyoletewa ili ayasaini kama alivyodai mahakamani hapo, basi katika karatasi za maelezo hayo kungekuwa na damu, lakini katika hali ya kushangaza hazikuwa hata na chembe ya damu na kudhihirisha kuwa aliyosema hayakuwa sahihi.

“Kutokana na karatasi hizo kutokuwa na damu, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka uliyachukua maelezo kupitia kwa mtuhumiwa bila kumtesa, na aliyatoa maelezo hayo kwa hiari yake mwenyewe bila kulazimishwa,” alisema Jaji Maghimbi.

Aliendelea kudai kuwa kupitia kifungu cha sheria cha 27, kifungu kidogo cha 1, cha sheria ya ushahidi, pingamizi la upande wa utetezi kutaka mahakama kutoyapokea maelezo ya mshtakiwa wa tatu yaliyotolewa polisi, limetupiliwa mbali na kudai kuwa yatachukuliwa kama kielelezo cha ushahidi kwa upande wa Jamhuri.

Baada ya uamuzi huo, wakili Safari, aliiomba mahakama kumpatia nusu saa ili kujadiliana na mteja wake huyo na washtakiwa wengine pamoja na jopo la mawakili wa utetezi, na Jaji Maghimbi aliridhia kwa kuahirisha kesi hiyo kwa nusu saa kabla ya kuendelea na ushahidi.

Baada ya muda huo kupita na kutimu saa tano na nusu, kesi hiyo iliendelea na wakili Safari aliwasilisha ombi lake kwa kudai baada ya kushauriana na watuhumiwa wote saba pamoja na jopo la mawakili wao, hawakuridhika na hukumu katika kesi hiyo ndogo na waliwaomba kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania na wameshaandaa notisi na zimeshaenda kwa Msajili wa Mahakama.

Safari aliiomba mahakama hiyo kusitisha shauri hilo hadi hapo rufaa hiyo waliyoikata itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi katika Mahakama ya Rufaa.

Baada ya ombi hilo la upande wa utetezi, ndipo upande wa Jamhuri unaoongozwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, ulipodai kuwa uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo unahusu kupokewa kwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu na hayajamtia hatiani mshtakiwa huyo na wala hayajampa adhabu ya kifo.

Chavula aliendelea kudai kuwa sheria inayotoa mamlaka ya rufaa kwa Mahakama ya Rufaa, haiwapi nafasi upande wa utetezi kukata rufaa kwa uamuzi ambao hauitimishi shauri lao.

“Sheria hii katika mazingira haya inatoa fursa kwa mkurugenzi wa mashtaka kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa namna hii, lakini sheria hiyo haiwapi ruhusa upande wa utetezi kukata rufaa wao,” alisema Chavula.

Alisema baada ya kuangalia notisi ya rufaa ya utetezi wanayodai kupokewa na Msajili wa Mahakama, inaweza kusimamisha shauri hilo lisiendelee endapo ingekuwa imesainiwa na msajili, lakini kutokana na kutosaini, aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali ombi hilo na shauri kuendelea kusikilizwa.

Baada ya vuta nikuvute hiyo kwa upande wa Jamhuri na utetesi kuhusu kesi hiyo kuahirishwa hadi rufaa itakapotolewa uamuzi au itupiliwe mbali, Jaji Maghimbi, aliomba kuahirisha kwa saa moja kesi hiyo ili aweze kutoa uamuzi.

Baadaye, Jaji Maghimbi, alisema hawezi kutoa uamuzi kuhusu rufaa hiyo na kuahirisha kesi hiyo hadi pale Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles