28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAKILI 18 CHADEMA KUMTETEA LEMA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wapili kulia), Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tundu Lissu (kulia),Mbunge wa Bunda Esther Bulaya (kushoto)na Mke wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Neema Lema(aliyevaa miwani) wakitoka nje ya mahabusu ya Gereza Kuu Kisongo la Arusha jana walipokwenda kumtembelea Lema anayeshikiliwa kwa zaidi ya miezi miwili tangu akamatwe Novemba mwaka jana.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wapili kulia), Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tundu Lissu (kulia),Mbunge wa Bunda Esther Bulaya (kushoto)na Mke wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Neema Lema(aliyevaa miwani) wakitoka nje ya mahabusu ya Gereza Kuu Kisongo la Arusha jana walipokwenda kumtembelea Lema anayeshikiliwa kwa zaidi ya miezi miwili tangu akamatwe Novemba mwaka jana.

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinakusudia kuungana na mawakili wengine 18 kumtetea Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, anayekabiliwa na kesi mbalimbali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Miongoni mwa kesi zinazomkabili Lema ni pamoja na kesi za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza mjini hapa jana katika ofisi za chama hicho baada ya kutoka kumtembelea Lema anayeshikiliwa kwa zaidi ya miezi miwili katika Mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kutokana na kukosa dhamana katika kesi ya uchochezi dhidi ya Magufuli, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema hatua za kisheria wanazozichukua kuanzia sasa ni kuongeza nguvu kubwa ya uwakili mahakamani kwa kuhakikisha katika kesi zote zinazomkabili mawakili wao wote wanakwenda Arusha ili kumtetea.

“Kuanzia sasa tutaongeza nguvu kubwa ya uwakilishi wa Lema mahakamani, tutahakikisha kesi zote mawakili wote 18 wa chama wanakuja Arusha kwenye kesi zake Lema,” alisema.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki aliambatana na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya pamoja na viongozi wengine wa Chadema mkoani hapa, alitaja hatua ya pili ni kuandika barua kwa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) ambao alidai wamenyamaza na kuwataka watoe tamko kuhusiana na suala hili na waseme kama wanaliunga mkono au hawaliungi kwa sababu wamekiuka wajibu wao wa kusimamia mfumo wa haki katika nchi hii.

“Wamejificha kwa muda mrefu, chama hicho na mawakili wenyewe wana wajibu wa kusimamia mfumo wa haki nchini lakini kwa muda mrefu wamekuwa kimya lakini ukimya huo unawapa nguvu wale ambao wanataka kuvunja milango ya haki kuvamia jengo la haki na kuvuruga haki za Watanzania,” alisema

“Watuambie wanaunga mkono au wanaupinga, tutawaandikia watoe msimamo wao, wasinyamaze wana wajibu wa kusema, hawahusiki tutajua nchi hii haina TLS tena na wakisema wanapinga na hawapendezwi tutawaomba wajiunge, tunataka kesi za Lema mawakili wa TLS Arusha, mawakili wajae mahakamani.”

Pia alisema wataandika barua kwa uongozi Chama cha Mawakili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili nao waungane nao kumtetea Lema aliyedai shitaka la uchochezi lina dhamana lakini hajapewa hadi sasa.

Alisema kila mahakama katika nchi hii kuanzia ile ya mwanzo au ya rufani ina mamlaka ya ziada ya kuzuia taratibu zake  za kimahakama kutumiwa vibaya kukandamiza haki ila katika kesi ya Lema kumeonekana matumizi mabaya ya mfumo wa mahakama.

“Hayo ni mamlaka ya mahakama yoyote, mfano mzuri wa matumizi mabaya ya taratibu za mahakama ni kesi ya Lema, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) waendesha mashitaka wa Serikali na wanasheria wake walikata rufaa Mahakama Kuu iliyopanga kusikiliza rufaa ila siku ya uamuzi walikuja na taarifa ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani na wanafanya hivyo makusudi kuifunga mikono na miguu Mahakama Kuu isifanye uamuzi na Lema aendelee kukaa gerezani,” alisema.

Lissu aliendelea kusema kuwa Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo wa kukataa na kuhoji wanasheria wa Serikali wanakata rufaa juu ya nini na kuwa jaji anafahamu mamlaka hayo na kuwa mahakama inatumika kama chombo cha kukandamiza haki za watu na Katiba ya nchi inataja miongoni mwa majukumu ya DPP ni kuzuia mfumo wa haki kutokutumiwa vibaya pamoja na ulinzi wa kutokuingiliwa na wanasiasa na wakubwa zake katika kufanya uamuzi wa kitaalamu lakini amekuwa akikiuka.

Alisema kutokana na kile kinachoonekana kukandamiza haki za Lema na wanyonge wengine kinyume cha Katiba na sharia za nchi  wameamua pia kulifikisha suala hilo katika jumuiya za kimataifa.

“Tunaanza mkakati wa kupaza sauti nje ya nchi, ndani ya nchi, bungeni, nje ya Bunge, mahakamani, katika vyombo vya habari rais asijidanganye kuwa tutanyamaza, hatutanyamaza,” alisema.

AMPONGEZA ASKOFU

Wakati huo huo Lissu alitumia nafasi hiyo kumpongeza Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa  kwa kuandika barua kuhusiana na suala la kuwepo kwa uhaba wa chakula na ukame.

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

Kuhusu kauli ya Rais Magufuli aliyoitoa juzi ya kukusudia kuyafungia magazeti mawili aliyosema yanaandika habari za uchochezi, Lissu alipinga akisema inangilia uhuru wa vyombo wa habari.

 MBOWE

Awali Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni,alisema  wao kama Chama waliamua kumtembelea Lema na kuwa wakati wanazungumza naye wamefarijika kumkuta na moyo mkuu huku akiamini kuwa fursa ya yeye kuwepo mahabusu itabadilisha mfumo wa mashitaka kwa watuhumiwa.

Alisema kuwa kwa mujibu wa Lema mahabusu wengi waliopo katika gereza hilo wanakabiliwa na kesi ambazo zina dhamana ila mpaka sasa bado wanashikiliwa na kukosa haki ya dhamana.

Akizungumzia suala la mbunge huyo kuendelea kusota rumande alisema alishawahi kuzungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai, Jaji Mkuu Othuman Chande na Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju ili Lema apate haki yake ya dhamana lakini mpaka sasa hajapata.

“Kuanzia Rais hadi uongozi wa chini ambao wana maamuzi wanajua juu ya suala la Lema kukosa dhamana kwa kesi inayompa mtu dhamana, tunapata hofu na namna Majajaji,Mahakimu na wengine wanavyotumia mamlaka yao “alisema Mbowe

“Sisi kama chama tulisubiri  na kujizuia kutoa tamko juu ya suala hili lakini tumeamua kuzungumza sasa,”

KUHUSU VYOMBO VYA HABARI Kama ilivyo kwa Lissu, Mbowe naye alipinga kauli ya Rais Magufuli.

“Ni dhahiri anatisha vyombo vya habari, hivyo uhuru wa vyombo vya habari uko mashakani, …ila hata akitufungia magazeti na mitandao ya kijamii hatutasita kumpinga na kumkosoa,”alisema.

Mbali na hilo, Mbowe pia alilaani vikali tabia ya ukandamizaji na kufunguliwa kesi kwa baadhi ya viongozi kuanzia ngazi za chini na kudai huko ni kudhoofisha upinzani.

“Huu ni wakati wa kufanya siasa za upinzani za kweli kwa wapinzani wote wapenda haki lazima tusimame kwani uonevu na ukandamizaji wa haki unaonekana kushika kasi,hata mimi biashara zangu nyingi zimevunjwa.”alisema

Lema alikamatwa Novemba 2 mwaka jana mjini Dodoma na kufikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha Novemba 8.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles