Na PASCHAL MALULU
MAWAKALA 23 wa bidhaa za vyakula wakiwamo wafanyakazi wa Mji wa Kahama wanashikiliwa na polisi wakidaiwa kusamnbaza na kuuaza bidhaa zinazodaiwa kuchakachuliwa ujazo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema mawakala hao pia walikutwa wametunza vibaya katika maghala yao bidhaa hizo.
DCaliwaambia waandishi wa habari kuwa katika ukaguzi juzi ilibainika mawakala hao wamekuwa wakivujisha ujazo wa bidhaa mbalimbali zikiwamo sukari, chumvi, mafuta ya kupikia na ngano.
Alisema mawakala hao wamekuwa wakipunguza kilogramu 25 hadi 22 na 23 kuwapunja wananchi wakati wa kununua.
Telack alisema katika baadhi ya maghala ya wafanyabiashara ilikutwa mifuko mifuko ya sukari 1000 iliyokuwa haina nembo ya kiwanda chochote.
Alisema mifuko hiyo ikuwa na nembo za makampuni mengine kama Azania, Kilombero na Kagera Sugar ambayo wamekuwa wakitumia kuhamishia sukari na ngano kutoka nje na kuwauzia wananchi kwa bei tofauti.
“Tumekuta mifuko ya sukari ambayo ina ujazo ambao siyo halali, mfuko wa kilogramu 25 unapunguzwa hadi kilogramu 22.
“Huu ni uhujumu uchumi kwa sababu si ujazo wa kiwandani, tutaendelea na msako huu kila mara na bila taarifa ikiwa ni pamoja na kuwakamata wahusika,” alisema Telack.
Alisema wafanyabiashara hao wote mashtaka yao yanaandaliwa na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili ikiwamo kukwepa kodi kwa kuwa kila wanapopunguza uzito hukwepa kodi ya serikali.