30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

MAUZO BIDHAA NJE YAONGEZEKA ASILIMIA 5.2

Na Joseph Lino


RIPOTI ya Hali ya Uchumi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Januari mwaka huu, inaonesha kuboreka kwa uchumi kwa kuongezeka mauzo nje.

 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mauzo ya nje yaliongezeka kwa asilimia 5.2 kwa Desemba mwaka jana, kutokana na biashara ya utalii na ongezeko la dhahabu.

Kwa ujumla, mauzo ya nje yalifikia Dola za Marekani milioni 9,381.6 ikilinganishwa na dola milioni 8,921.9 kwa mwaka uliyotangulia Desemba mwaka 2015.

Ripoti inaonyesha ongezeko hilo linatokana na sekta ya utalii, madini ya dhahabu na bidhaa za ndani.

Sekta ya utalii iliongoza katika kuingiza fedha za kigeni ikifuatiwa na mauzo ya bidhaa za viwandani kutokana kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa kwa thamani ya dola milioni 2,231.4 kufikia mwishoni mwa Desemba jana ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 11.

Hili linatokana vilevile na kuongezeka kwa watalii waliotembelea Tanzania na kiwango cha bidhaa zilizouzwa nje.

Uuzaji wa madini ya dhahabu nje uliongezeka kwa asilimia 22.5 na kufikiwa kwa thamani ya dola milioni 1,449.4 kutokana na kupanda kwa bei katika soko la dunia. Kwa upande wa mazao, mauzo ya tumbaku yalifikia dola milioni 312.7, korosho dola milioni 270.6, pamba dola milioni 468 na chai dola milioni 39.3; kufanya jumla ya dola milioni 1,090.6.

Pia kulikuwa na ongezeko la madini mengine, mazao ya mafuta, nafaka, kakao, mbao na ngozi.

Kwa wastani wa soko la dunia, bei ya pamba ilipanda, huku chai, kahawa na dhahabu zilishuka.

Bei ya dhahabu ilishuka kufikia dola 1,157.4 kwa wakia wa troi moja Desemba mwaka jana ukilinganisha na dola 1,238.4 ya mwaka uliotangulia.

Kupanda kwa bei ya pamba katika soko la dunia kulitokana na uhitaji mkubwa, lakini kwa  upande wa bei ya kahawa  aina ya robusta, ilishuka kufikia dola 2.3 kwa kilo na arabica dola 3.6.

Kushuka kwa bei ya kahawa kulichangiwa na uwingi wa kahawa nchini Brazil, Colombia na Honduras.

Kwa upande wa ripoti ya mfumuko wa bei, umeongezeka kwa asilimia 5 Desemba mwaka jana kutoka asilimia 4.8 Novemba, pia ikilinganishwa na asilimia 6.8 ya Desemba mwaka 2015.

Ongezeko hilo limetokana na mfumuko wa bei ya chakula, vinywaji visivyo na kilevi na mafuta.

Hali ya chakula

Ripoti inaonesha kuwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA) kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka jana, kulikuwa na jumla ya tani 89,692, kiasi ambacho kimekuwa kwa miezi miwili mfululizo bila kubadilika ya tani zipatazo 90,900.

Tofauti ya kushuka kidogo imetokana na kutolewa kwa chakula katika maeneo yanayokabiliwa na uhaba wa chakula na ukame unaoendelea.

Bei ya vyakula

Bei ya jumla ya vyakula kama mchele, maharage na viazi ilikuwa chini kufikia Desemba mwaka jana, ikilinganishwa Desemba mwaka 2015, lakini mahindi na mtama bei yake ilikuwa juu.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kati ya Novemba na Desemba mwaka jana, ambapo bei ya mazao yote ya chakula ilipanda, isipokuwa viazi ambavyo bei ilishuka.

Bidhaa toka nje

Uagizaji bidhaa kutoka nje umeanguka kwa asilimia 13.7 na kufikia dola milioni 10,397.4 hadi kufikia Desemba mwaka jana na uagizaji bidhaa ndio uliongoza na kuwa asilimia 80.2. Kwa ujumla kulikuwa na mapungufu ya uagizaji bidhaa nje kwa viwango mbalimbali isipokuwa kwenye mafuta ya petrol na malighafi za viwanda ambazo ziliongezeka gharama.

Kuanguka kwa gharama za mitambo ni kutokana na kukamilika kwa miradi mikubwa kama Kiwanda cha Saruji cha Dangote Mtwara, ukamilishaji wa miradi ya nishati ya gesi asilia na utafiti wa rasilimali asilia.

Uingizaji mafuta nchini gharama ziliongezeka kwa silimia 14.9 na kuwa na thamani ya dola milioni 3,172.7 ikiongezeka kutokana na kukua kwa kiasi kilichoingizwa.

Gharama za  huduma mbalimbali zilipungua na kufikia  dola milioni 2,136.3 kwa mwaka jana kutoka dola milioni 2,666.7 kwa mwaka uliotangulia 2015 kutokana na kupungua kwa safari za nje kwa amri ya Rais Magufuli ya kudhibiti utokaji wa  nje kwa maofisa wa Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles