25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

WACHINA KUJENGA BARABARA ZA JUU DAR

Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM


FOLENI ni tatizo sugu katika miji yetu na sugu zaidi katika Jiji la Dar es Salaam ambalo linakuwa kwa kasi na lina wakazi wapatao takribani milioni nne na nusu.

Usafiri wa magari na hasa ule wa binafsi ambao unatumika jijini, unaonekana kukuza ufinyu wa barabara zetu na hivi kuhitaji juhudi za ziada za kushughulikia tatizo hilo. Serikali imeliona hilo tatizo na awali ilipanua barabara mbalimbali lakini bila mafanikio ya kumaliza tatizo na sasa imebuni matumizi ya ‘barabara za madaraja’ au ‘flyover’ ili kumaliza tatizo.

Inaaminika kujenga barabara za juu ni suluhisho kwa changamoto inayowakabili wakazi wa jiji hili katika adha ya usafiri na foleni ambazo zimeanza kuwa gharama kubwa katika uchumi wa nchi. 

‘Tazara flyover’ ni mfano halisi  hapa  nchini kujengwa kwa barabara za juu ‘flyover’ tangu tupate Uhuru na wataalamu  wanadai tutaendelea kushuhudia miradi mingi ikijengwa kuanzia hapo. Kuna awamu sita za ujenzi wa flyover jijini Dar es Salaam.

Mradi unaofuata kwa mlolongo ni ule wa Ubungo Flyover ambao utaanza kutekelezwa kuanzia Machi mwaka huu katika makutano ya barabara ya Morogoro, Mandela na Sam Nujoma  ambao unatarajia kuanza.

Mradi huu ni moja ya ahadi za Rais Dk. John Magufuli kujenga barabara za Flyover tano, ujenzi wa barabara nyingine za juu katika makutano ya barabara za Nelson Mandela, Morogoro na Sam Nujoma eneo la Ubungo na ujenzi wa daraja jipya la Salander lenye urefu wa kilomita 6.23 kuanzia Coco Beach hadi Hospitali ya Agha Khan.

Aprili 16 mwaka jana, rais aliweka jiwe la msingi  la mradi wa makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo kuelekea na kutoka uwanja wa ndege na bandarini.

Katika maelezo yake, Rais Magufuli anasema barabara hiyo ya juu itakuwa ya kwanza kujengwa hapa nchini na ujenzi wake umepangwa kugharimu takribani Sh bilioni 100 ambapo kati ya fedha hizo, Sh bilioni 93.44 zitatolewa na Japan kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA) na Serikali ya Tanzania itatoa Sh bilioni 8.3.

“Barabara ya juu itakayojengwa itakuwa na njia nne na urefu wa mita 300 kutokea maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na inatarajiwa kupunguza kero ya msongamano wa magari yaendayo na yatokayo Uwanja wa ndege na Bandari ya Dar es salaam,” anasema Rais Magufuli.

Rais Magufuli anasema barabara hiyo inajengwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali yake ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, ambao kwa mwaka 2013 pekee utafiti umeonesha ulisababisha upotevu wa Sh bilioni 411.

 

Wiki iliyopita, Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), walitiliana saini na Kampuni ya M/S China Civil Engeneering Construction Cooperation kutoka China (CCECC) mkataba wa  ujenzi wa barabara za Juu ‘Interchange’ katika makutano ya barabara ya Sam Nujoma, Mandela na Barabara ya Morogoro  eneo la Ubungo TANESCO jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Mtendaji Mkuu Tanroads, Mhandisi  Patrick Mfugale, alisema zaidi ya Sh bilioni 177.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo utakaowekewa jiwe la msingi Machi mwaka huu.

 Anasema mkataba huo unamtaka mkandarasi wa Kampuni ya CCECC  kutoka China   kukamilisha  mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ndani ya miaka mitatu ambao ni sawa  na miezi 30 hadi kukamilika kwake.

“Hakikisheni mnaanza ujenzi mara moja kwani Serikali imeshakamilisha taratibu zote na tayari kiasi cha Sh bilioni 2.1 zimelipwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo,” anasema Mhandisi Mfugale.

 Anasema Ujenzi wa Ubungo ‘interchange’ unajengwa kwa fedha ya mkopo kutoka Benki ya Dunia  kwa ajili ya  uboreshaji  miundombinu ya  usafiri Dar es Salaam.

Mhandisi  Mfagule anasema ujenzi umelenga katika kupunguza  msongamano  wa magari na foleni  hivyo  kuongeza ufanisi  katika usafirishaji na Serikali iliona umuhimu wa kujenga  barabara zinazopishana kwa kwenda juu katika eneo la Ubungo.

 

“Zaidi ya magari 65,000 yanapita kila siku katika makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo, hali inayosababisha msongamano katika barabara ya Morogoro ambayo ndio lango kuu la kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam,  hivyo ufanisi wa mradi huo utahuisha hali ya usafirishaji katika jiji hili na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisisitiza Mhandisi Mfugale.

Anasema  upembuzi  yakinifu na usanifu wa kina  wa Ubungo  ‘interchange’ ulifanywa na Kampuni ya M/s Hamza Associates ya Misri kwa kushirikiana na Kampuni ya  Advanced Engineering Solution ya Tanzania kwa gharama ya Sh bilioni 951.2 na kazi hiyo ilikamilika Desemba mwaka 2015.

Anasema mhandisi  mshauri  kwa ajili ya usimamizi  wa kazi ya ujenzi  wa mradi huo  ni Kampuni ya M/s DASAN Consultants ya Korea ya Kusini  ilishirikiana na Kampuni ya AFRISA Consulting Ltd ya Tanzania  kwa Sh bilioni 8.2.

 Mhandisi Mfugale  anasema kulingana na usanifu wa barabara za juu katika eneo la Ubungo, zitajengwa kwa safu tatu  ambazo ni chini itatumika kwa magari yanayopita katika barabara ya Morogoro pamoja na  magari yote yanayopinda kushoto.

“Safu ya pili  itajengwa katika urefu wa mita 5.57 kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa magari yote yanayopinda kulia ambayo yataongozwa pia na taa za barabarani na safu ya tatu itajengwa katika urefu wa mita 12.5 kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa magari yanayopita barabara za Mandela na Sam Najumo,” anasema.

Anasema barabara zote zitakuwa  na njia sita za magari, ikiwa ni pamoja na njia mbili za magari ya usafiri  wa mabasi yaendayo haraka.

Aidha, anasema  walitoa tangazo la zabuni  kwa ajili ya mradi huo ambao ulitolewa Januari 20, mwaka jana, jumla ya kampuni 48 zilijitokeza  kuomba  zabuni hiyo  na zabuni 14 zilipokelewa  Agosti 18, mwaka jana.

 Anasema kuwa baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa zabuni zilizowasilishwa, Kampuni ya CCECC ndio iliyokidhi vigezo vya zabuni.

Anasema mradi huo ukikamilika kwa wakati  utasaidia kukua kwa pato la Taifa na kukuza uchumi wa  nchi kupitia usafirishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CCECC, Jiang Yigao, alimhakikishia Mhandisi Mfugale kuwa wataanza maandalizi ya ujenzi huo mara moja na watafanya kazi hiyo kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles