28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji ya Tembo yamepungua nchini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA) imesema kiwango cha Ujangili wa tembo kimeshuka katika hifadhi za Taifa ukilinganisha na hali iliyokuwepo miaka ya nyuma.

Hatua hiyo inachangiwa na juhudi za Tawa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali sambamba na wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi.

Afisa Uhifadhi wa Tawa Kitengo cha Uchunguzi, Tryphone Kanoni akizungumza wakati wa warsha hiyo.

Hayo yamebainishwa Machi 14, 2024 na Afisa Uhifadhi wa Tawa Kitengo cha Uchunguzi, Tryphone Kanoni wakati wa warsha maalumu kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la USAID.

Kwa mujibu wa Kanoni, meno ya tembo yanayokamatwa kwa sasa mengi ni ya miaka ya nyuma, na mapya yamekuwa nadra kuonekana, jambo ambalo linaonyesha kwamba mapambano dhidi ya ujangili yanazaa matunda.

“Tumejitahidi sana ku-contain (kudhibiti) mauaji ya tembo kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana huwezi kuona meno mapya ya tembo. Hata haya mnayoona yamekamatwa, mengi ni ya miaka ya nyuma,” amesema Kanoni. 

Sehemu ya washiriki.

Alisisitiza kwamba mnyama mwingine anayelindwa sana kwa sasa ni faru (weusi na weupe) kwa kuwa wameorodheshwa kama viumbe waliohatarini kutoweka, hivyo serikali imeweka jitihada za makusudi za kuwalinda kila wanapokuwa.

“Tumeelekeza nguvu pia kumlinda faru kwa kuwa ni mnyama aliye hatarini kutoweka. Kwa hiyo, popote atakapokuwepo, nasi tupo. Ulinzi wake ni mkubwa na unaonyesha mafanikio,” alisema ofisa huyo wa Tawa.

Ujangili wa kutumia mapanga

Katika hatua nyingine, Mtaaalamu huyo amezungumzia kuhusu mbinu mpya ya ujangili wa kuua wanyama kwa kutumia mapanga kushika kasi hivi sasa kuliko matumizi ya risasi kama ilivyozoeleka huko nyuma.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo(Kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru.

Alisema wawindaji haramu wanaua wanyama kwa kuwakata na panga miguuni, jambo linalomfanya mnyama ashindwe kukimbia, hivyo wanakuua kwa urahisi pale atakapokuwepo.

“Hawataki kutumia risasi kwa sababu zinatoa mlio na ni gharama kubwa, sasa mlio wa risasi ukisikika utawashitua askari wa Uhifadhi na pia utawashitua wanyama wengine ndani ya hifadhi, jambo ambalo hawapendi kulifanya kwa sasa.

“Tawa tumebaini mbinu hiyo, hivyo nasi tunaimarisha ulinzi kwenye hifadhi zetu kuhakikisha kwamba hakuna majangili wanaofanikiwa katika mbinu zao za kuua wanyama,” alisisitiza ofisa huyo.

Akiwasilisha maada katika warsha hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano (SJMC), Dk. Abdallah Katunzi alisema kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya uhifadhi na umuhimu wake kwa maendeleo ya Taifa.

Alisema jukumu hilo wanalo waandishi wa habari ambao wana wajibu wa kuandika habari zao za kuelimisha jamii kuhusu masuala ya uhifadhi wa Wanyamapori na maliasili nyingine kwa maendeleo yao na vizazi vijavyo.

“Tunapozungumzia uhifadhi, tunalenga kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo navyo vinafaidika na rasilimali zilizopo sasa, lazima uhifadhi tunaoufanya ufikirie zaidi vizazi vijavyo,” amesema Dk. Katunzi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano (SJMC), Dk Abdallah Katunzi, akizungumza wakati wa warsha hiyo.

Akizungumzia mafunzo hayo mmoja wa washiriki, Nyamiti Kayora amesema amejifunza mengi na sasa anatambua wajibu wake wa kuhakikisha anaandika habari za kuelimisha jamii katika masuala ya uhifadhi ili kutengeneza kizazi kinachojali mazingira.

“Nimeongeza uelewa kuhusu tabia za wanyamapori na umuhimu wa kuhifadhi ikolojia yao. Nimejua kwamba mazingira yakiharibiwa, yanasababisha wanyama kuwa na migongano na Binadamu lakini ukifuatikia hayo ni maeneo yao ya asili, binadamu ndiyo wamevamia,” amesema Nyamiti.

Afisa Mawasiliano kutoka JET, Tulinagwe Malopa.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles