25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAUAJI MARA

  • Wawili wauawa kwa kukatwa mapanga, mishale na shoka

NA BENJAMIN MASESE-SERENGETI

MAPIGANO kati ya kabila la Wakurya na Wangoreme yamesababisha vifo vya watu wawili baada ya kukatwa mapanga, kupigwa mishale na shoka na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na ugomvi wa mashamba na mipaka.

Mapigano hayo yalizuka saa moja asubuhi jana eneo la Mentoha, baada ya kundi la Wakurya kutoka Kijiji cha Mekomariro, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, kuwavamia wakulima wa Kijiji cha Remng’orori (Wangoreme) kutoka Serengeti na kuanza kuwashambulia kwa silaha za jadi na kusababisha vifo vya watu hao.

Waliouawa wametambuliwa kwa majina ya Wigesa Kigene na Mwikwabe Nghebo, baada ya kukatwa na mapanga sehemu mbalimbali za miili yao.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, mkazi wa eneo lilipotokea tukio hilo, Moremi Mang’ango, alisema kundi la watu zaidi ya 40 kutoka Mekomariro walivamia wakulima wa Remng’orori na kuanza kuwashambulia kwa silaha za jadi ikiwamo mishale, shoka na mapanga.

Mbali na silaha za jadi, pia alisema kundi hilo lilikuwa na silaha za moto.

“Wananchi wa Remng’orori walikuwa mashambani wanalima, ghafla walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 40 waliokuwa na silaha za jadi na kuanza kuwashambulia kwa mapanga, yaani kila mmoja alianza kukimbia ili kujinusuru na wengine walijificha katika makorongo.

“Kundi hilo la wavamizi lilimvamia Mwikwabe aliyekimbilia katika nyumba moja ya Maswi na kuingia ndani, lakini jamaa hao walimfuata na kumkata kata mapanga hadi kufa, huyu Wigesa yeye aliuawa kule kule shambani.

“Hawa Wakurya inaonekana walijipanga muda mrefu na baada ya kufanya mauaji haya wamekimbia kurudi kijijini kwao, sasa upande wa pili yaani Wangoreme wenyewe hawakutaka kuvuka kwa sababu waliwajulisha polisi kutoka wilayani Serengeti-Mugumu na tayari wamefika eneo la tukio,” alisema.

Naye mkazi wa Mtaa wa Mentoha, Kijiji cha Remng’orori, Nkaira Sagaswe, alisema wameshangazwa kuona Wakurya wakiwavamia katika mashamba yao wakati tayari mgogoro wa mashamba na mipaka kati ya wilaya za Butiama na Serengeti ulikwishatatuliwa na viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Taifa na Mkoa wa Mara.

Sagaswe alisema hivi sasa amani imetoweka katika eneo hilo na wakazi wanaoishi jirani na Mekomariro wanahofia kuvamiwa tena usiku katika makazi yao.

“Hapa ni hofu tupu na kila mmoja anaonekana kuwa na hasira kutokana na vifo hivi, lakini tunashukuru askari wamefika saa sita mchana wakati tukio limetokea asubuhi saa mbili, polisi wanaendelea kuchukua maelezo ya upande wa Remng’orori, sasa hatujui kama watakwenda upande wa pili,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Remng’orori, Hezron Ng’anyi, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema ni hali ya kusitikisha huku akiwatupia lawama viongozi wa wilaya na mkoa kwa kushindwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa takribani miaka 15.

Ng’anyi alisema wavamizi hao walifika eneo lake wakiwa na silaha za moto na jadi zikiwamo mishale, shoka na mapanga na waliouawa wamekutwa na mishale na majeraha makubwa ya kukatwa na mapanga na shoka.

Pia alisema tukio hilo lilikuwa la kushtukiza ndiyo maana wamefanikiwa kuua raia waliokuwa mashambani na kufanikiwa kutoweka na aliviomba vyombo vya dola kuingilia kati na kusuluhisha kwa kuonyesha mipaka ya wilaya hizo.

“Tunashukuru polisi wamefika kutoka wilayani na mkoani, wametuliza hali na kututoa wasiwasi, lakini wanapaswa kulinda raia na mali zao, hatujui usiku wa leo kama wavamizi watarejea, ila tunaomba kila mmoja achukue hatua ya kujilinda ili hali hii isiweze kujirudia,” alisema.

Alipoulizwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, alikiri tukio hilo kutokea na alidai kuwa mgogoro ulikuwa ukishughulikiwa na ulisimama kidogo baada ya viongozi wa mkoa na wilaya kuhudhuria mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma.

MTANZANIA Jumamosi lilifanya jitihada za kuzungumza na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Serengeti (OCD), Mathew Mgema, aliyekuwa eneo la tukio kwa njia ya simu lakini alikataa kuzungumza chochote.

Pia lilimpigia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Henry Mwaibambe, lakini hakupokea simu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles