31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji Kigoma yamuweka Zitto matatani

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM



MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amehojiwa kwa saa nne katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam kwa tuhuma za uchochezi na baadaye kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi.

Kiongozi huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo alikamatwa jana saa 5:26 asubuhi nyumbani kwake Masaki na kupelekwa katika kituo hicho kwa mahojiano.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Murilo, alithibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo.

Kamanda Murilo aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanamhoji mbunge huyo kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu mauaji ya wananchi katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

“Ni kweli tumemkamata Zitto, tunaendelea na mahojiano naye, tunataka atueleze na ushahidi kuhusu taarifa yake aliyoitoa kwamba wananchi 100 wameuawa huko Uvinza mkoani Kigoma.

“Kwa sasa naomba mniache niendelee na kazi ya kumhoji na taarifa zaidi nendeni Central (Kituo Kikuu cha Polisi) maana sisi tutakuwa tunawapelekea kila kitu kinachoendelea hapa,” alisema Kamanda Murilo.

Ilipofika saa 9:36 alasiri Zitto alitoka katika kituo hicho akitumia gari aina ya Toyota IST yenye namba T 855 CSA na kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi.

Wakili wa mbunge huyo, Jebra Kambole, aliliambia MTANZANIA kuwa mteja wake anatakiwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema kiongozi wao amehojiwa kutokana na taarifa aliyoitoa kwa waandishi wa habari kuhusu mauaji ya wananchi 100 yaliyotokea katika Wilaya ya Uvinza mkoani wa Kigoma.

“Baada ya saa nne ya kuhojiwa, sasa amepelekwa Central kwa mahojiano zaidi. Wakati wanakwenda kumchukua nyumbani kwake kumhoji walieleza kuwa wanakwenda kumhoji kwa makosa ya uchochezi kuhusu taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari ya mauaji ya wananchi 100 huko Uvinza mkoani Kigoma.

“Sasa hivi amepelekwa Central kwa mahojiano zaidi, sasa tunasubiri kama watampeleka mahakamani ama laa,” alisema Shaibu.

Juzi, Jeshi la Polisi mkoani Kigoma ilimtaka Zitto kuwasilisha vielelezo juu ya kauli aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari Jumapili iliyopita kuwa ana taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi Wilaya ya Uvinza mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno alisema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumapili ya wiki iliyopita, Zitto alisema wiki chache zilizopita yalitokea mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Mto Malangarasi, Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza ambako Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka aliuawa na wanaodaiwa kuwa ni wananchi.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yote yanayojiri huko Uvinza tangu kuuawa kwa askari polisi wetu. Tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno.

“Kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi limekalia kimya suala hili, pamoja na IGP kutembelea eneo hilo la maafa. Haiwezekani kamwe tukio kubwa namna hii kutokea halafu Serikali ibaki kimya bila kutoa maelezo yoyote kwa wananchi. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanywa ili kutambua nini kimetokea pale Mpeta,” alisema Zitto.

Alisema chama chao kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na kitaweka wazi taarifa husika.

“Kwa sasa tunaitaka Serikali ieleze nini hasa kimetokea, maelezo hayo yawe ya kina na yawe ya ukweli. Chama chetu kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na kitaweka wazi taarifa husika,” alisema Zitto.

Juzi Zitto alipoulizwa kuhusu wito wa polisi Kigoma, alisema bado hajaupata na kwamba katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari jambo la kwanza alitaka polisi kutoa taarifa kwa umma kuhusu mauaji hayo.

“Sijapata wito huo. Kauli yangu ilikuwa wazi kabisa kuwa polisi watoe taarifa kwa umma. Wametoa taarifa ambayo hawakuwa wametoa. Tunatafakari,” alisema.

Alipoulizwa anatafakari wito wa polisi au taarifa iliyotolewa na jeshi hilo, alisema chama chake kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na kitaweka wazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles