Na Mwandishi Wetu,
Uchumi wa dunia umevia na hivyo kufanya miradi mipya ya rasilimali kuwa katika hali ya sintofahamu, ingawa wahusika wanajikaza kisabuni na kusema mambo bado ni shwari.
Ukweli ni kuwa miradi ya gesi na mafuta si kitu kwa sasa kwani bei ya bidhaa imeanguka vibaya na kuwa na thamani kama ya theluthi yake ya miaka mitatu iliyopita.
Habari toka Kampala zinasema kuwa uwezekano wa Uganda kusafirisha nje mafuta yake yanakabiliwa na matatizo ya kifedha kama ilivyo kwa Tanzania na Msumbiji. Habari hizo ni mwiba kwa wawekezaji ingawa ni habari njema kwa wenye mitaji na wanaotafuta hisa kwenye kampuni za mafuta kwani hununua inapokuwa bei chini na kuuza hisa bei inapokuwa juu.
Nchini Tanzania, Kampuni ya Statoil inayoongoza kwa uchimbaji mafuta na gesi nchini, imesema itachukua miaka mitano kujadili faida za mafuta kwa nchi na haswa maudhui ya taifa (local content) kwa mtambo wa kuchakata LNG.
Kutoka Uganda, Tullow Oil, Total SA na CNOOC wanatafuta fedha za uwekezaji ikiwamo ya kujenga miundombinu ikiwamo bomba kutoka Hoima kule Uganda hadi Bandari ya Tanga ambapo itajengwa mitambo ya kituo cha kujazia mafuta katika eneo la Tongolani.
Kiasi cha Dola bilioni 4.0 zinahitajika za kujenga kilomita 1430 kwa muda wa miaka mitatu ambapo Tanzania imepewa jukumu hilo baada ya ushindani na kuipiku nchi ya Kenya .
Mchambuzi wa Bloomberg Intelligence ya London, Will Hares, anasema shida kubwa kwa Uganda ni kwamba kila kitu ni kwa mara ya kwanza na hivyo ina hatari kubwa kiuwekezaji.
“Ratiba zinawezwa kukiuka na kuweka kila mtu kwenye wasiwasi na hivyo kufanya mradi uwe na gharama kubwa, kwani wadau wote wataathirika ikiwa mradi utacheleweshwa,” anasema.
Uganda ina hazina ya mafuta inayokisiwa kufikia mapipa bilioni 1.7 katika Ziwa Albert na Serikali inategemea kuanza uzalishaji wa mafuta mwaka 2021 na inategemea kupata mapato ya Dola bilioni 43 katika miaka 25 ya uendeshaji mradi.
Kuendeleza uzalishaji wa mafuta zinahitajika Dola bilioni 8 ingawa michoro ya kihandisi haijaanza kutengenezwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa George Cazenove, msemaji wa Tullow, zinasema Tullow inatakiwa ifanye uamuzi wa mwisho wa kuwekeza inapofikia mwaka 2018 na ujenzi utakamilika ndani ya miaka mitatu,
na kuhimiza mradi kiwanja cha ndege kinachotegemewa kujengwa kwenye eneo la mradi kurahisisha mawasiliano. Kwa maelezo ya Robert Kasande, Mkuu wa Kitengo cha Mafuta cha Serikali ya Uganda katika mahojiano ya Novemba 10 mwaka huu, msemaji wa Total Ahlem Friga Noy na Msemaji wa CNOOC, Aminah Bukenya, hawakusema chochote walipoulizwa mipango yao ya uwekezaji.
Kwa ujumla, Waganda wamekuwa watatanishi kidogo kuhusu uendelezaji wa sekta ya mafuta ambapo imechukuwa takriban miaka 10 kutoa leseni, wakati Ghana ilichukua miaka mitatu tangu ilpogundulika hadi kuanza uzalishaji mafuta.
Vilevile Uganda ni kigeugeu kwani baada ya kuahidi kwa muda mrefu kuwa itaipa Kenya fursa ya kupitisha bomba huko, ikabadili na kulipitisha Tanzania dakika za mwisho na hivyo ni jambo la kulizingatia na kutafakari kwa kina kwani linaweza kujirudia.
Ujumbe wa Uganda uliofuatilia suala hilo, walifurahia namna Tanzania ilipolifikisha kwa marefu na mapana na kujua kweli ina nia na uwezo wa kukamilisha ujenzi kwa muda uliopangwa.
Kenya nayo inaonekana kukumbwa na matatizo ya uwekezaji katika mradi wake mkubwa wa LAPSETT kwa kukimbiwa na wawekaji wa Sudan Kusini na Ethiopia na hivyo kuvurugwa kwa mwelekeo wa mwenendo wa mradi huo, lakini tarehe za utekelezaji wa mradi itabidi zipangwe upya kuzingatia mabadiliko hayo. Mapato ya Sudan kwa asilimia 95 ni mafuta na hivyo kudorora kwa bei kumeifanya taifa hilo changa kuchanganyikiwa.