28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Naiko: Uchumi wa kati wataka mipango sahihi

naiko

Na LEONARD MANG’OHA,

SHAUKU kubwa miongoni mwa Watanzania walio wengi ni kuliona taifa likifikia malengo ya kuwa taifa la uchumi wa kati linalohubiriwa kwa muda mrefu sasa likichagizwa zaidi na ahadi za rais aliyepo madarakani ambazo amekuwa akizitoa tangu wakati wa kampeni mwaka uliopita.

Ni imani yangu kuwa kila mwenye nia njema na taifa hili anatamani kuona jambo hilo likifanikiwa katika enzi hizi, akiwa bado ana nguvu na utashi wa kufanya mambo mbalimbali na pengine kuyaishi maisha ambayo yamekuwa yakisimuliwa na wale waliobahatika kufika katika mataifa yenye uchumi wa kiwango hicho na hata zaidi.

Si dhambi kuwaza kufikia hatua hiyo ya maisha kwa sababu hata waliofika huko walikuwa nchi masikini kama vile Afrika Kusini, Japani na India, nchi ambazo zimekuwa na ukuaji mzuri wa uchumi katika kipindi cha miaka kati ya 30 na 40.

Hadi sasa, pamoja na matatizo kadhaa yanayozikumba nchi hizo zimeendelea kustawi kiuchumi na kupunguza kiasi cha umasikini miongoni mwa wananchi wake na hii inatokana na mataifa hayo kuweka mazingira bora ya uwekezaji na wananchi wake kupewa fursa za kutumia rasilimali zilizopo kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na nchi kwa ujumla wake.

Katika kila taifa, ziko sekta ambazo hupewa kipaumbele zaidi kwa kuzingatia umuhimu wake katika nchi husika na shughuli hizo ni zile zinazoliingizia taifa kiasi kikubwa cha pato lake, hapa ndipo taifa hujipambanua na kuweka nguvu zaidi katika maeneo hayo ili yaendelee kuchangia zaidi bila kuziacha sekta zinazochangia kidogo kwa kuzifanya ziongeze uchangiaji kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta hizo.

Kwa Tanzania, sekta ya utalii, madini na kilimo ndizo sekta zinazotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa, huku kilimo ambacho ndicho kinachohusisha takribani asilimia 75 ya Watanzania wote.

Licha ya kuwa wananchi wengi hujihusisha na kilimo nchini, bado kilimo hakijaweza kuchangia vya kutosha ukilinganisha na idadi ya watu wanaojihusisha na shughuli za kilimo na hii inatokana na wakulima walio wengi kulima kilimo cha mazoea cha kujipatia chakula tu na si kinacholenga kupata ziada ya kutosha kufanya biashara.

Emmanuel Ole Naiko ni Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), anasema Serikali inapaswa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili wawekezaji wa ndani na nje waone fursa ya kuwekeza katika kilimo na kukifanya kuwa chenye faida.

Alisema hadi sasa Tanzania haijafanikiwa kufika huko kwani bado wakulima wanakiona kilimo kama suala la utamaduni na si kazi inayoweza kuwaletea manufaa na kuwasaidia kuepuka umasikini.

“Tunapaswa kukienzi kilimo kwa kuhakikisha kinatulisha na kukifanya kuuzika kibiashara na kuwa kazi ya staha kama kazi nyingine si kukiona kama suala la utamaduni na kuwa ni kitu duni,” anasema Ole Naiko.

Anasema kilimo bado kinaathiriwa na mambo mbalimbali ikiwamo ukosefu wa miundombinu, pembejeo na masoko ya uhakika, hivyo mambo hayo yanapaswa kuboreshwa na kukifanya kuwa sehemu yenye tija ambayo mtu akiingia kuwekeza asitamani kutoka.

Upatikanaji wa masoko kwa mazao yanayozalishwa ni suala muhimu linalopaswa kutiliwa mkazo ili wakulima wawe na uhakika wa kuuza mazao wanayoyazalisha na kuwatia hamasa wazalishe zaidi.

Matumizi duni ya teknolojia bado ni kikwazo kwa wakulima walio wengi kutokana na kuendelea kutumia jembe la mkono, utaratibu ambao ni kama mchezo wa maigizo tunapozungumzia kilimo cha kuhudumia viwanda na kinacholenga biashara zaidi kuliko mahitaji ya chakula.

Pia kuanzishwa kwa skimu za umwagiliaji wa mashamba makubwa na yasiyotegemea mvua za misimu ili kuzalisha badala ya mkulima awe na uwezo wa kuzalisha mwaka mzima na hili lazima liende sambamba na ujenzi wa mabwawa na mifumo ya umwagiliaji katika maeneo yanayofaa kwa kilimo hususan vijijini ambako wakulima wengi wanapatikana.

Pamoja na kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii kama vile mbuga za wanyama, milima mirefu kama Kilimanjaro, mapango ya kale, mchanga unaohama huko mkoani Manyara, mbege na nyani wasiopatikana sehemu nyingine ya dunia, vyura wa ajabu kule Kihansi, fukwe za bahari na maziwa makuu, bado havijatuwezesha kujipatia fedha za kutosha kupitia utalii wa ndani na wa nje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles