Na SAMWEL MWANGA-MASWA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imetoa siku 90 kwa watu wote waliojimilikisha mali zake bila kufuata utaratibu kuzirejesha mara moja vinginevyo watashtaki kwa makosa ya wizi.
Wito huo umetolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dk. Fredrick Sagamiko wakati akizungumza na MTANZANIA wakati akielezea utekelezaji wa zoezi la urejeshaji mali za wananchi wa wilaya hiyo zilizochukuliwa na baadhi ya watu bila kufuata taratibu.
Alisema Serikali inaendelea kusimamia urejeshaji wa mali za umma zilizopatikana kwa njia ya kihalifu kupitia mpango wa kupambana na uhalifu wa mali za serikali ulioanzishwa mwaka 2012 kwa kuwashtaki na kutaifishia mali hizo pindi ushahidi unapopatikana.
“Huu ni mpango wa kurejesha mali za serikali haukuanza leo ni tangu mwaka 2012 upo sisi kama halmashauri tunachokifanya na kuuendeleza tu ni lazima tupambane na uhalifu tutakachokifanya ni kuwashitaki na kisha tutataifisha mali zao hizo walizopewa wakishindwa kuzirejesha kama tulivyoagiza,”alisema.
Alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali wilayani humo kuunda timu ya kufuatilia mali za halmashauri na kubaini mali nyingi zikiwemo vituo vya mafuta,viwanja na nyumba zikiwa zinamilikiwa na baadhi ya wafanyabiashara, wanasiasa na watumishi wa Umma bila kufuata utaratibu na tayari wahusika wameshajulishwa kwa barua.
Dk Sagamiko aliongeza kwamba mhusika ambaye atakaidi agizo hilo atashitakiwa na mali aliyoipata kinyemela kutaifishwa kulingana na kosa lake pia suala hili litamgusa kila mtu wakiwemo watumishi wa umma.
Aidha alisema kurejeshwa kwa mali hizo kutawasaidia wananchi wa wilaya hiyo katika shughuli za kujiletea maendeleo na siyo kama ilivyo sasa kuwa baadhi ya watu wachache wananufaika na raslimali za umma.
“Ni kweli nimepokea barua toka halmashauri ya Wilaya ya Maswa ikinitaka ndani ya siku 90 niwe nimerejesha kiwanja cha halmashauri ambacho ninafanya biashara ya kuuza mafuta pale nimeweka kituo cha kuuzia mafuta kwa kile kinachodaiwa kuwa nilikipata kwa njia zisizo halali,” alisema.