23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

MADIWANI WAMKALIA KOONI DED

Na Upendo Mosha, Rombo

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, wamemtuhumu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Magerth John, kwa kushindwa kufuata kanuni na  maadili ya utumishi wa umma na kusababisha kushindwa kutekeleza maazimio ya baraza la madiwani, jambo linalokwamisha shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo.

Mbali na tuhuma hizo, pia mkurugenzi huyo anatuhumiwa kuwa na uhusiano mbaya na watendaji, huku akiwahamisha vituo vya kazi kwa kile kinachodaiwa kuwa na chuki binafsi.

Akiwasilisha hoja binafsi ya utovu wa nidhamu wa mkurugenzi huyo katika kikao cha Baraza la Madiwani juzi, Diwani wa Kata ya Makiidi, Simon Kinabo, alisema tangu mkurugenzi huyo ateuliwe kuongoza halmashauri hiyo, amekuwa na utendaji mbovu unaolalamikiwa na watendaji, wananchi na madiwani.

 

Alisema utovu wa nidhamu umekuwa  kikwazo kwa watendaji, wananchi na madiwani, jambo linalochangia kuwapo na mpasuko mkubwa.

“Muda sasa umepita tangu mkurugenzi aripoti hapa, amekuwa na utovu wa nidhamu wa hali ya juu na hili lilidhihirika alipopata ugeni wa mwananchi mmoja akihitaji huduma kwake, badala ya kumsikiliza na kumsaidia aliketi juu ya meza kwa dharau, huku akiongea na simu, ni jambo la ajabu sana,” alisema Kinabo.

 

Alisema amekuwa akiendesha halmashauri hiyo kwa mabavu na kushindwa kutoa ushirikiano kwa watendaji, huku wale walioonekana kutoa ushauri na kumpinga, waliandikiwa barua za uhamisho mara moja.

“Kuna watendaji wetu wa halmashauri ambao wameonekana wakitoa ushauri na kumpinga kwa vituko anavyovifanya, wameandikiwa barua za uhamisho na ninaweza kuwataja watendaji hao kwa majina mbele ya baraza hili,” alisema.

Kinabo alisema amekuwa akipuuza maagizo  mengi yanayotolewa na baraza la madiwani, jambo ambalo halikubaliki.

Alisema mpaka sasa kuna maagizo mengi yamepuuzwa na kutokufanyiwa kazi kutokana na kuingiza masuala ya utendaji na siasa, ikiwa  ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Naye Diwani wa Kata ya Kyelamfua, Mokala Lubega, alisema mbali na tuhuma mbalimbali anazokabiliwa nazo, pia ameshindwa kusimamia vema vyanzo vya mapato kwa kutowalipa vibarua.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Evaristy Silayo, alisema hoja binafsi iliyoletwa na diwani huyo ni ya msingi  na inapaswa kufanyiwa kazi na kujadiliwa ili kuinusuru halmashauri hiyo.

“Kutokana na uzito wa hoja hiyo, ni lazima tutumie kanuni zetu zinazotuongoza, hatutaijadili hapa badala yake tutatafuta siku maalumu ya kumjadili, baraza litajigeuza kamati na kupata nafsi  ya kuijadili ili tufikie mwafaka kwa lengo la kuinusuru halmashauri yetu,” alisema Silayo.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, mkurugenzi huyo aliwataka madiwani kuacha kuitisha kikao maalumu cha kumjadili, badala yake watumie kikao hicho hicho kumjadili kwa kigezo cha kubana matumizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles