26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mashtaka mapya kwa Lissu yagonga mwamba

LISSUNa Kulwa Mzee

– DAR ES SALAAM

JAMHURI imeshindwa kuwasomea mashtaka mapya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema)   na wahariri wa gazeti la Mawio baada ya upande wa utetezi kudai wanayarudisha mashtaka yaliyofutwa kivingine.

Hoja za kupinga kusomewa mashtaka hayo ziliwasilishwa jana na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hoja hizo ziliibua mvutano mkali uliosababisha Hakimu Simba,  kuwaonya mawakili wa pande zote mbili na kuwaambia anaweza kuwachukulia hatua kwa kuisumbua mahakama.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi uliwasilisha maombi wakitaka kusoma hati mpya ya mashtaka dhidi ya washtakiwa wanne akiwemo Lissu.

Mahakama ilipokea hati hiyo ya mashtaka na kuruhusu Jamhuri kuisoma lakini Wakili Kibatala,  alipinga mashtaka hayo kusomwa kwa madai kwamba hayatofautiani na yaliyoondolewa na mahakama hiyo Juni 28 mwaka huu.

“Mheshimiwa hakimu shtaka la kwanza na la tano lililopo katika hati ya mashtaka ni sawa na lile shtaka la kwanza na la tano liloondolewa na mahakama baada ya kupinga na kuonekana kwamba hayakustahili kisheria.

“Wakili wa Serikali Paul Kadushi alikubaliana na hoja za utetezi na mahakama iliamua kuyaondoa hivyo haiwezekani mashtaka yaliyoondolewa leo yarudishwe kwa mtindo mwingine.

“Upande wa Jamhuri ulichotakiwa kufanya ni vitu viwili tu, kukatia rufaa uamuzi uliotolewa ama kuomba kufanya mapitia ya uamuzi huo na si kurudisha mashtaka yaliyoondolewa,”alidai Kibatala.

Baada ya kuwasilisha hoja hizo Wakili Kishenyi aliomba kuahirisha kesi kwa muda ili aweze kujibu hoja za utetezi, kesi iliahirishwa hadi mchana ambapo Jamhuri ilijibu hoja hizo.

Akijibu hoja Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la tano ni kama hayakuwepo mahakamani na kwamba kuondolewa haikatazi kuyarudisha tena.

Alidai mashtaka yalipofunguliwa awali yalikuwa hayana kibali cha DPP lakini sasa hivi yamerudishwa yakiwa na kibali.

“Tusingeweza kuyakatia rufaa tunakata rufaa kwa kesi ambayo ilishasikilizwa ikamalizika, hii tungekatia rufaa kitu gani,”alidai.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja aliamuru uamuzi wa hoja hizo utatolewa Septemba 8 mwaka huu na kuruhusu upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa shtaka la pili, tatu na nne ambayo hayabishaniwi.

“Nimesema mashtaka yasiyobishaniwa yasomwe, mkikataa kuyasoma nikiahirisha kesi bila kuwasomea mashtaka mtawashika na nini,”alisema Hakimu Simba.

Wakili Kishenyi alikubali kuwasomea washtakiwa mashtaka yanayowakili kuanzia shtaka la pili, tatu na la nne ambapo alidai washtakiwa katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa, Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob na Lissu.

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa‎ za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho. ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili walidai washtakiwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam,  walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles