Na Malima Lubasha, Serengeti
MKUU wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Dk. Vicent Mashinji ameipongeza Serikali na Wadau wa Utalii kwa kuendelea kutekeleza miradi yenye thamani ya Sh bilioni 1.5 katika Kijiji cha Robanda kinachonufaika na miradi ya elimu, afya na maji.
Dk. Mashinji amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika kijij hicho inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na nguvu za wananchi na wadau ikiwa ni fedha zinazotokana na utalii.
Mkuu huyo wa Wilaya ameitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa maji wenye thamani zaidi ya Sh milioni 600 unaotekelezwa na RUWASA, ujenzi wa nyumba katika zahanati ya Robanda 2:1 ili kupunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa afya yenye thamani zaidi ya Sh milioni 100 fedha zilizotolewa na serikali.
Aidha, Dk. Mashinji ameipongeza kampuni Thomson Safari’s inayoshughulika na shughuli za Utalii na kuwekeza katika pori la akiba Grumeti na Hifadhi ya Serengeti kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa bweni na nyumba ya walimu 2:1 katika shule ya sekondari Robanda yenye thamani ya Sh milioni 340.
Amesema kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake pia inajenga vyumba vinne vya madarasa katika shule ya msingi Robanda kati ya hivyokimoja kikiwa ni kwa ajili ya TEHAMA kwa thamani ya Sh milioni 130.
“Tunashukuru serikali ya awamu ya sita ya Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi nzuri ya kutupatia fedha zilizotuwezesha kutekeleza miradi hii katika kijiji hiki cha Robanda tutaendelea kusimamia vizuri fedha zote zitakazoletwa kwa ajili ya miradi mingine,” amesema Dk. Mashinji.
Baada ya mwekezaji wa masuala ya Utalii Kampuni ya Thomson Safari’s kama mdau kujenga bweni na nyumba katika Shule ya Sekondari Robanda, Serikali imeridhia shule hiyo kuwa na kidato cha 5 na 6 katika masomo ya Sayansi PCM na PCM kwa wasichana kuanzia Julai mwaka huu lengo likiwa ni kuandaa kupata wataalam mbalimbali.
Akizungumzia mradi wa maji katika kijiji hicho ambao amesema ni wa fedha kubwa zilizotolewa na serikali tangu mwaka 2021 ulipoanza kutekelezwa, amehoji sababu ya kushindwa kutoa maji.
Hivyo ameutaka uongozi wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wilayani humo kuhakikisha wanasimamia vyema mradi huo ukamilike haraka ili ifikapo mwisho wa mwezi huu wananchi wapate maji safi na salama.
Dk. Mashinji akiwa katika mkutano wa hadhara kijijini Robanda kupokea kero za wananchi baada ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ameitaka RUWASA kuhakikisha changamoto zote zinazokabili mradi huo kutoka chanzo kilometa 7 hadi kijijini kwenye tenki za bomba kupasuka, mashine ya kusukuma maji kuwa nguvu kidogo zinakwisha.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mrobanda Japani amethibitisha kuwa kutokana na kijiji kupata mradi wa maji ya bomba kaya zaidi ya 400 zimenunua mita lengo ikiwa ni kudhibiti matumizi ya maji na kuomba uongozi wa wilaya kusaidia malalamiko kukosa maji muda mrefu unakwisha wananchi wapo tayari kuupokea mradi huo.