22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Masheikh waikataa Rasimu ya Sitta

Sheikh Rajabu Katimba
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba

NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

SHURA ya Maimamu Tanzania imetangaza hatua za kuikwamisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, kwa kwenda kuwaeleza waumini wa dini ya Kiislamu kupiga kura ya hapana.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iliyowasilishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, kuiweka kando Mahakama ya Kadhi.

Akizungumza na MTANZANIA jana mara baada ya kumalizika kikao cha maimamu wa nchi nzima, Msemaji wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba, alisema hatua ya kupiga kura ya hapana ni moja ya azimio lililoafikiwa na kikao hicho.

“Msimamo wetu kwa asilimia 100 ni hapana, hatuungi mkono, tunalaani vikali jinsi mchakato huu wa Katiba ulivyovurundwa kwa sababu maoni ya Waislamu hayakuzingatiwa.

“Leo (jana) tulikuwa na kikao kilichojumuisha maimamu wote kutoka Tanzania na msimamo wetu katika hilo ni hapana,” alisema Sheikh Katimba.

Mbali na msimamo huo, Sheikh Katimba alisema mkutano huo pia umejadili mambo mengine mazito ambayo yatawekwa wazi hivi karibuni.

Sheikh huyo alisema wiki hii watakutana na vyombo vya habari ili kutoa tamko lao rasmi kuhusu Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Juzi na jana kumekuwa na ujumbe mfupi wa maneno (sms) uliokuwa ukisambazwa ambao ulisomeka hivi; ‘Assalam Alaykum, ndugu Muislam baada ya kukataliwa Mahakama ya Kadhi katika mchakato wa Katiba Mpya, Umoja wa Maimamu Tanzania (SHURA) wanakutana ili kujadili msimamo wa Waislamu kuipigia kura ya Ndiyo au Hapana mapendekezo ya Katiba Mpya’.

Katika rasimu hiyo inayopendekezwa, Ibara 28 zilizokuwamo katika Rasimu ya Pili iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba zimefutwa huku Ibara 186 zikifanyiwa marekebisho na kuingizwa Ibara mpya 41.

Maimamu mikoani

Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina lake, kilieleza masuala mengine mbali na azimio hilo la kukwamisha rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kila imamu katika mkutano huo amepewa jukumu la kwenda kuzungumza na waumini wa msikiti wake na kuwaeleza ukandamizaji wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

“Pamoja na hali hii, lakini kila mmoja wetu sasa tunakwenda kuwasha moto mikoani maana hili Bunge la Katiba limebeba ajenda zote zenye masilahi yao kisiasa kuliko hali halisi.

“Kwa hali hii kuanzia sasa unyonge umefika mwisho, maana kila mara Serikali imekuwa ikitumia ngao ya Watanzania wanyonge hasa Waislamu kupitisha mambo yao…. Kwa sasa kwa Katiba hii tutaikwamisha tu,” kilisema chanzo hicho.

Wiki iliyopita, Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC), nalo lilitangaza kurudi kwa Watanzania na waumini wao kuwaambia cha kufanya baada ya maoni yao yaliyotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) juu ya Bunge Maalumu la Katiba kutupwa.

Akizungumza na gazeti hili, Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severin Niwemugizi ambaye pia ni mjumbe wa TCF, alisema tamko lao walilolitoa mwezi uliopita halijafanyiwa kazi ipasavyo na sasa wanajiandaa kurudi kwa waumini wao.

“Tunaona Bunge bado linaendelea na Serikali iliyopo madarakani inaendelea na mipango yake, haiheshimu wala haitekelezi ushauri unaotolewa na viongozi wala taasisi za dini.

“Sauti nyingi haziridhiki na yale yanayotendwa na Bunge Maalumu la Katiba, hawajui ni kiasi gani Watanzania wameshapevuka na wanatambua haki zao,” alisema.

Alisema wamejipanga kurudi kwa Watanzania kuwafahamisha na kuwafundisha ili watambue haki na wajibu wao hali itakayowasaidia kujua njia sahihi ya kufanya.

“Wanaweza kutudharau kwamba sisi hatuna chochote, kwakuwa hawajali tuliyopendekeza tutarudi kwa watu wetu tunaowaongoza, kitakachotokea hatujui.

“Sisi tunaamini kurudi kwa Watanzania ni sehemu pia ya injili kwa sababu kuna injili ya jamii na tutawafundisha watambue haki na wajibu wao na namna sahihi ya kufanya,” alisema.

Askofu huyo alisema wanachotaka Watanzania ni kuona mambo yakienda vizuri, hivyo kama viongozi wanakataa ushauri unaotolewa na wananchi wataamua cha kufanya.

“Wamewezesha maoni na masilahi ya chama tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba Mpya kwa nia ya kulinda masilahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora,” inasema sehemu ya tamko hilo.

Kauli ya Sheikh Jongo

Juzi wakati wa mjadala wa kuchangia Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, Mjumbe kutoka kundi la 201 Sheikh Himid Jongo, alitangaza kupiga kura ya Hapana endapo Mahakama ya Kadhi haitatambuliwa kikatiba.

Taarifa hiyo aliitoa bungeni alipokuwa akitoa maoni yake juu ya rasimu hiyo. Kauli ya Sheikh Jongo ilitokana na kauli iliyotolewa na mjumbe wa Bunge hilo ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, kwamba ana maoni yake juu ya mahakama hiyo, lakini hawezi kuyatolea bungeni kwa kuwa si mahali pake.

Pamoja na kusema hayo, Kingunge alisema kama Waislamu hawaridhishwi na Rasimu ya Bunge hilo kutotambua mahakama hiyo, kuna kila sababu ya kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa Watanzania hawawezi kugawanyika kwa sababu ya mahakama.

Mtatiro, Lissu na kura mtandaoni

Katika hatua nyingine Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Katibu wa UKAWA ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, Julius Mtatiro, wameanza kuhamasisha umma namna ya kupiga kura ya maoni kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii, Lissu na Mtatiro walianza kuhamasisha umma juu ya upigaji kura ya maoni.

Katika ukurasa wake wa Facebook, Mtatiro aliandika; ‘Piga kura ya maoni sasa; Rasimu ya Warioba na TMK = ‘A’ au Rasimu ya Sitta, Chenge na BMK = ‘B’.

“Piga kura yako kwa kuandika neno A au B au unaweza kuandika Warioba au Sitta ama unaruhusiwa kuandika (TMK – Tume ya Mabadiliko ya Katiba) au (BMK – Bunge Maalumu la Katiba). Mwisho ni Oktoba 15, 2014,” hayo ni baadhi ya maneno yaliyoandikwa katika ukurasa wa Mtatiro.

Katika ukusara wa Lissu aliandika; ‘Piga kura ya maoni hapa’, A Rasimu ya Jaji Warioba na B Rasimu ya Sitta na Chenge.

Katika ukurasa wa Mtatiro, watu wote waliotoa maoni yao walionekana kuunga mkono rasimu iliyopendekezwa awali na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wengine waliandika ‘Jaji Warioba na TMK ndio kila kitu na wengine waliandika afadhali TMK.

Katika ukurasa wa Lissu, watu wengi pia walionekana kuunga mkono rasimu iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wengine waliandika; “Mimi ni A anayesema B ni kati ya wale wanaonufaika na keki ya taifa hili asiyejua atasuport kwa kupewa vijisenti kiduchu huku watoto wake wakipata elimu mbovu.

- Advertisement -

Related Articles

8 COMMENTS

 1. Ni wakati sasa kutimiza ahadi..hayo mambo ni ya msingi ya waislamu na haziwezi kuleta matatizo maana ni mambo yakifamilia zaidi mambo ya ndoa talaka na mirathi..ili wapate haki kutokana na imani zao..zanzibar mbona ipo na inaendelea vizuri kabisa..

 2. Mabadiliko lazima yaonyeshe kubadilika. Mabadiliko yasiyoonyesha kubadilika ni dalili ya ubinafsi.Hivi sasa tu tunapiga mark time katika maendeleo ya nchi hii. Hatuna jipya katika rasimu ya Sita. Tusiogope mabadiliko. Njia ya maendeleo ni kubadilika. Siamini kuwa nchi itachafuka kwa kuwa na rasimu ya Warioba.Sisi tumezoea amani. Hebu tujaribu rasimu hii bila woga. Waoga hawashindi vita. Tuko kwenye vita vya maendeleo. Nashauri tubadilike kwa kuwa hakuna mafanikio bila ya mabadiliko. Wanaosisitiza rasimu ya Sitta ni waoga na hawajajifunza wenzetu wengine walifanya nini hata wakasonga mbele kimaendeleo. Tusiogope wala tusitishane kwa kuwa nina uhakika 100% hatutagombana. Ikishindikana basi tutakaa tena tuone tuboreshe wapi lakini change is inevitable. No way out if we want to make a step. Alicholeta Warioba ndicho wanachofanya Marekani. Jiulize wako wapi? Mbona hawajapigana wenyewe kwa wenyewe? Hizi ni siasa za kukandamiza maendeleo kwa kuwa wapo wasiotaka waondoke madarakani ili jambo jipya liingie lilete tofauti.Fear is the door for the devil. Close it and he will find no way.
  Regards to you all.

 3. Kumekucha sasa Tz, wananchu acheni kulala, amkeni kuitetea nchiyenu. “Tumepuuzwa vyakutosha, tumenyanyaswa na kukandamizwa na CCM vya kutosham unyonge wetu ndiyo uliotufanya tufike hapa, sasa kila Mtanzania aliyejitambua aseme, sasa inatosha” isipokuwa wale waliopewa vijisenti na wakauza uhuru na haki yao. Kumbuka Mwl. Nyerere daima alisema ” wakati ni huu.” Hii rasimu haramu ya CCm iliyopendekezwa na BMK imeleta mwelekeo mbaya wa Taifa. Naungana na wote wanaopinga rasimu hii asilimia 200%. Pa,pja na kupoteza mabilioniya Pesa, hakuna sababu yakupitisha uozo kama huo. Nchi nyingi tu suala la katiba linachukua miaka, na pesa nyingi zinatumika, Tz si nchi yakwanza kuandika katiba mpya, kenya walitumia pesa nyingi na walitumia karibu miaka 20 mpo hapa watanzania mnaopenda ushabiki bila kujua nchi nyingine zimefanya nini? Msidanganywe na CCM, afadhalikuchelewa kupata katiba nzuri, kuliko kulipua lipua na kuishia na katiba mbaya. Mtadanganywa Oh tuipitishe, lakini tutafanya mabarekebisho baadaye, ujue huo ni uwongo. Kenya hapo walisema mambo fulani yatawekwa sawa, je lipo wapi sasa? Kwa hivi Watanzania tujifunze kutoka kwa nchi jirani, kama mambo hayajakaa vemA NI HERI WOTE KWA SAUTI NA NGUVU MOJA “tUIKATAE KWA KUPIGA KURA YA ” HAPANA.” Mungu awatie nguvu na ujasiri Watanzania wote kusema “Hapana’ siyo kwa misingi ya udini, bali kwa misingi ya kuandaa katiba inayotenda haki na kuendeleza uhuru wa kuabudu na hakikwa kila dini. Mimi sitetei Ukristu, bali natetea utaifa na uzalendo. Suala la kuchomeka masuala ya dini au imani katika katiba mpya tuachane nalo, litaleta migogoro huko mbele. Waislamu mmeambiwa anzisheni mahakama zenu kama madhehebu mengine, mbona hamtaki? Kwa nini mnang’ang’ania iweke ndani ya katiba? Waiweka kwa misingi ipi sasa? na madhehebu mengine vipi? hayo mambo tuyaache chini a uangalizi wa madhehebu yenyewe. Mungu wabariki watanzania.

 4. Jamani inatosha sasa kusema hapana, hivi ni kwanini viongozi wanadharau maoni ya wananchi kiasi hiki? hivi sisi watanzania tumekosa nini? kosa letu ni nini chini ya jua.

  Mungu alituumba kuteseka? na kama mlikuwa hamtaki kwanini mlianzisha mchakato wa katiba? kwanini mmetupotezea muda wetu hivi? YAONYESHA MNATUONA SISI NI WAJINGA NA WAPUUZI.

  Maoni yetu ya rasimu ya pili yalikuwa mazuri na kueleweka nyinyi watu wachache hapo bungeni ni kina nani?? na mmepata wapi mamlaka ya kutuandikia mnachotaka… MIMI NINA AMINI HII RASIMU YENU HAITAPITA. PIA MZEE SITA ANAZEEKA VIBAYA HUYU BABA NA HAFAI. Mi naomba ajitazame na amrudie Mungu.

  Ndugu zangu Waislam, mimi ni mkristo ila nawashauri nyinyi anzisheni mahakama yenu wala msirudi nyuma na msipoteze muda. Kama inakuwa inaweka maadili ambayo kwenu mnaona yamepotea tatizo nini? Msisononeke wengine nafsi zetu zinajisikia vibaya nyinyi ni ndugu zetu nasi ni watoto wa baba mmoja.

  MUNGU awatangulie na hakika tutashinda. TANZANIA na taifa letu MBELEEEEEEEEEE.

 5. Ikiwa mtu anafanya kitu kile kile kila siku, kila mwezi hadi kila mwaka na akatarajia mabadiliko basi huyo ana wazimu ! Chama cha CCM kwa miaka nenda rudi, idadi wanaijua, kimekuwa kikifanya madudu yaleyale bila kuleta maendeleo kwa wananchi. Mabadiliko kwa maendeleo ni inevitable.
  Watanzania tusihofishwe (intimidated) kuwa mabadiliko yanaleta fujo. Hizo ni propaganda za mafisadi ambao wame-loot utajiri wa nchi yetu na kutuacha hoi kwa miaka zaidi ya hamsini.
  TUKATAE mbinu za CCM .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles