26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa nzito ulinzi shirikishi Ubungo

Eneo la Ubungo jijini Dar
Eneo la Ubungo jijini Dar

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo maarufu kama ‘wamachinga’ wa eneo la Ubungo, Manispaa ya Kinondoni, wamegeuzwa kitega uchumi na kikundi kinachojiita cha ulinzi shirikishi kwa kuwatoza ushuru kinyume na sheria.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA umebaini kikundi hicho kimekuwa kikikusanya fedha kwa wafanyabiashara hao kati ya Sh 1,000 na 5,000 kutegemea aina ya biashara, ushuru ambao unaingia mifukoni mwao bila halmashauri kujua.

Mbali na kikundi hicho, pia walinzi wa Kampuni ya kuzalisha umeme wa gesi ya Songas wanadaiwa kujihusisha na ukusanyaji wa fedha kwa wamachinga wanaopanga biashara karibu na lango kuu la kuingilia.

Uchunguzi wa kina umebaini kiasi kinachokusanywa na makundi hayo mawili ni zaidi ya Sh milioni 2 kila siku kutokana na wastani wa wafanyabiashara 500 waliopo katika eneo hilo.

Mwaka jana, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilifanya operesheni maalumu ya kuwaondoa wafanyabiashara hao katika eneo hilo kwa madai kuwa ni hatarishi linaloweza kusababisha maafa kutokana na kuwa karibu na mitambo ya umeme ya Songas na Tanesco, lakini hivi sasa wamerudi kwa kasi.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda, alisema eneo hilo halipo kwa ajili ya biashara na wanaofanya hivyo wapo kinyume na sheria.

“Hakuna kituo cha biashara katika maeneo yale na wanaotoza ushuru ni wezi na wanaowapa watambue kuwa wanaibiwa, manispaa haiwatambui na wala haibariki wizi huo na tutachukua hatua,” alisema Mwenda.

Mmoja wa wafanyabiashara, George Manisha, alisema wanapenda maeneo ya Ubungo, Mwenge na Kariakoo kwa kuwa ni sehemu ambazo kuna wateja wa kutosha.

Alisema eneo lililotengwa kwa ajili yao la Machinga Complex lililopo Ilala ni gumu kibiashara kwa sababu hakuna wateja wa uhakika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles