Hadija Omary, Lindi
Jumla ya mashauri 161 ya utelekezwaji wa watoto yameripotiwa katika Shirika la usaidizi wa kisheria mkoani Lindi, Lindi Women Paralegals (LIWOPAC) katika kipindi cha mwaka 2019/2020.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Cosma Bullu mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa anazungumza na MTANZANIA DIGITAL ofisini kwake.
Bullu alisema kati ya mashauri 558 yaliyopokelewa katika shirika hilo mashari 430 yaliripotiwa na wanawake huku mashauri 161 yalihusiana na wanaume kutelekeza familia na watoto wadogo hasa watoto wachanga.
Alisema kwa zaidi ya asilimia 78 ya mashauri hayo wanaoongozwa kulalamikiwa ni wanaume ambao wamezaa nje ya ndoa.
Bulu pia alisema kuwa hali ya baadhi ya wanaume kutelekeza watoto na kulelewa na mzazi mmoja kwa kiasi kikubwa hupelekea uwepo wa watoto wa mitaani.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Lindi, Richard Kimaro alisema kuwa ushirikiano katika malezi ya mtoto kati ya wazazi, walezi pamoja na jamii unahitajika kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha kunakuwa na ulinzi na usalama wa mtoto.
Kimaro aliongeza kuwa Suala la ulinzi wa mtoto ni jukumu la jamii nzima, mlezi na mzazi mmoja mmoja kwa nafasi yake katika ngazi ya familia pamoja na serikali kwa ujumla.
Alisema mzazi, jamii na serikali wakishirikiana hawataweza hata siku moja kuwaona watoto wakiwa mitaani wanazurura muda ambao wanatakiwa kuwa shuleni nasi tubaki kimya.