25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Masharti mapya kuingia mtaani

Na BRIGHITER MASAKI-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuanzia Jumatatu wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, hawataruhusiwa kutoka kwenda popote wala kupanda daladala bila kuvaa balakoa (mask).

Pamoja na hilo Makonda ameagiza biashara zote kuanzia kesho zianze kufanyika kwa njia ya kufunga (take away).

Makonda ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema hali ya mkoa huo si nzuri tena.

“Anayekwenda eneo la manunuzi yeyote yale lazima awe amevaa barakoa ununue ukate leso ukate khanga utafute rababendia lazima uwe umevaa,” alisisitiza na kuongeza; 

“La pili kuanzia Jumatatu biashara zote zifanyike  kwa mfumo wa ‘take away’ ukienda sehemu kanunue ondoka.

 “La tatu lazima kuwe na hatua au mita mbili katika kila mahala unapokwenda kwenye msongamano wa watu, la nne wafanyabiashara wote tafuteni mfumo mzuri wa kusimamia masoko yenu” alisema.  

Alisema wanapambana na  mdudu asiye onekana na kwamba wangemuona wasingebadilisha haya na kusisitiza kwamba takwimu za juzi kuhusu maambukizi ya corona nchini si nzuri.

Juzi Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitangaza ongezeko la wagonjwa wapya wengine 53 na kufanya jumla kufikia 147.

Idadi hiyo inafanya katika kipindi cha ndani ya wiki moja Tanzania kuwa na ongezeko la wagonjwa 115.

Juzi Shirika la Afya duniani (WHO) lilishtushwa na kuonya  kasi ya maambukizi barani ya Afrika katika kipindi cha wiki moja  kwamba inaweza kufanya bara hilo kuwa kitovu ya maambukizi mapya kuzidi yale ya China ulikoanzia ugonjwa huo.

Kauli ya sasa ya Makonda  ambayo inaonekana kujaa maonyo na tahadhari inatofautiana kwa kiasi kikubwa na ile aliyoitoa wiki mbili zilizopita ambapo mbali na kutumia muda mwingi kuwashutumu waandishi wa habari kwa kuandika habari alizoiita za kutisha kuhusu virusi corona pia aliwashangaa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam baadhi yao kujifungia ndani kwa kuogopa virusi hivyo na kuwaita wavivu na kwamba watakufa njaa.

Tofauti kabisa na sasa ambapo Makonda anakiri kwamba hali ni mbaya, wiki mbili zilizopita alikaririwa akisema kuwa hakuna hali ya shaka na  anashangaa watu kuogopa corona wakati yamekuwepo magonjwa mengine kama kipindupindu na ukimwi ambayo yamekuwa yakiua watu wengi.

Jana Makonda alionekana kujitenga mbali kabisa na kauli hizo za nyuma na zaidi akienda mbali kwa kusema kuwa kila familia ya Mkoa wa Dar es Salaam wafanye vikao wajadiliane na wakubaliane kama wameamua kufa kwa virusi vya corona.

“Familia zifanye vikao vya ndani kupanga mkakati wa kujikinga na Corona na wajitafakali kama wapo tayari kufa na Corona au watajikinga.

“Haiwezekani baa zimefungwa lakini mtu mzima na akili zako unatoka unakwenda baa kunywa pombe unataka tufikie hatua tukuchape bakora hauna akili wewe kweli unataka hadi upigwe ndio ujuwe Corona inauwa?.

“Virusi hawa ni rahisi sana kuwapata, sasa ukate kitambaa, ukate kanga au ununue bila barakoa hakuna kutoka nyumbani kwako” alisisitiza Makonda.

“Wananchi wa jiji la Dar es salaam ifikapo siku ya jumatatu kila mmoja atumie barakoa kila mahali anapokwenda kuanzia sokoni, kwenye usafiri wa umma na maeneo mengine ya kazi zao za kila siku kama hauna usitoke.

“Biashara zote zifanyike kwa mfumo wa kufunga hakuna mtu kununua kitu na kukaa hapo hapo, funga nenda nyumbani kwako” alisisitiza

“Wenye masoko yenu mtafute namna ya kuendesha masoko yenu, jitafutieni utaratibu sio kila mara mnasubiri tamko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa kasemaje”

“Sitaki kuona tunafika hatua ya kupigana bakora kutokana na kupinga maambukizi ya Corona kila mtu atumie akili yake na ajue Corona sio ugonjwa wa kuchezea.”alisema Makonda

Aidha alitoa wito kwa  kampuni za simu zitumie  miito ya simu(ringtone) kwa ajili ya kutoa elimu dhidi ya ugonjwa huu hatari wa Corona badala ya kuweka nyimbo za kawaida ili kusaidia kupambana na ugonjwa huo.

Maagizo hayo mapya ya Makonda tayari yamezua mjadala ndani ya jamii kupitia mitandao ya kijamii na kuacha maswali hasa kwa makundi ambayo yamekuwa yakitafuta ridhiki kwa njia kujiajiri.

Makundi hayo ni kama mama ntilie, vinyozi, saluni za kike, machinga wanaotembeza vitu barabarani na wengine.

Mjadala mkubwa ni namna watakavyoendeleza biashara zao pasipo kuvunja maagizo hayo, hali kadhalika namna watakavyojipatia vipato vyao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles