31.5 C
Dar es Salaam
Sunday, February 5, 2023

Contact us: [email protected]

Teknolojia itumike kupunguza tatizo la ajira nchini

Na MWANDISHI WETU

MOJA ya changamoto kubwa zilizopo Afrika ni ajira ambayo kwa nchi ya Tanzania ina zaidi ya asilimia 60 ya vijana wanaoishi mjini, lakini hawana ajira rasmi zinazoweza kuwaingizia kipato cha uhakika kila siku. 

Zimekuwapo jitihada huko nyuma kuhakikisha tunapunguza tatizo la ajira lakini bado kuna fursa ambazo hazijatumika vizuri katika kuhakikisha ajira zinapatikana kwa urahisi kwa watu wengi hasa wanawake na vijana.

Pia kumekuwapo na malamiko mengi kutoka kwa wanasiasa na watu mbalimbali kuwa kama tusipochukua hatua basi tatizo la ajira linaweza kuwa ni bomu siku sijazo. 

Ni wachache kati ya hawa walalamikaji walioweza kutoa mawazo ya kupunguza tatizo la ajira ambalo litachangia kupunguza umasikini na kukuza uchumi.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35 ni asilimia 70 ya Watanzania wote.  Asilimia kubwa ya hawa vijana wanatumia mitandao ya kijamii kuhabarishana na kwa matumizi mbalimbali ikiwamo huduma za kifedha. 

Takwimu za  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha asilimia 52 ya Watanzania wenye simu za mkononi wanatumia huduma za intaneti na hii ni dalili ya wazi kuwa ukuaji wa sekta ya mawasiliano unaweza kutoa ajira kwa Watanzania wengi.

Kati ya mwaka 2010 na 2015 idadi ya watumiaji wa simu za mkononi imeongezekwa kwa zaidi ya milioni 300 na inakadiriwa kuwa, hadi kufikia mwaka 2020 idadi itaongezeka kwa zaidi ya bilioni moja. Hadi mwaka 2020 dunia inakadiriwa kuwa na watu bilioni tatu ambao watakuwa wanatumia simu janja (smartphone) hivyo kutoa fursa zaidi kwa vijana nchini.

Kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2010 Tume ya Tanzania ya Sayansi na Mawasiliano (COSTECH) iliona fursa hii kuanzisha kitengo cha kutambua fursa zitokanazo na teknolojia ( Dar Teknohama Business Incubator). Kitengo hiki kimesaidia ukuaji wa teknolojia ya habari mawasiliano kwa kutambua vipaji, kutoa elimu ya biashara, kuwafutia fedha za kuendesha miradi ya vijana mpaka kutengeneza ajira.

Vijana hawa wametengeneza mifumo ya mtandao kupitia simu (Mobile Apps) ambazo zitatumika kutoa huduma mbalimbali kama afya, elimu na za kibiashara kwa wananchi. Kasi ya ukuaji na ubunifu bado ni ndogo ila kuna fursa kubwa ambayo kama ikisimamiwa vyema itawasaidia vijana wengi.

Ni wazi kuwa kitengo hiki hakikuweza kuwapa vijana maarifa na nyenzo za ziada ambazo zinaweza kuwafanya waweze kusimama na kuendesha biashara zao. Taasisi ya Financial Sector Deepening Fund (FSDT) kupitia programu ya Findsrupt imeweza kutatua changamoto hii ambapo wameweza kuendesha ‘boot camp’ iliyopata vikundi vya vijana ambao sasa wanawapa elimu ya biashara itakayofungua fursa za kibiashara.

FSDT pekee haitoshi kutatua changamoto walizonazo vijana wetu hasa katika eneo la teknohama hivyo basi, serikali na kampuni binafsi wanapaswa kujitokeza na kuwa katika mstari wa mbele. Kwa kuanzia ningependa kuona kampuni za simu zikishiriki kwa ukaribu katika kusaidia vijana na wakati huo huo kufanya biashara.

Kutokana na mapinduzi ya intaneti nchini, mafanikio haya ya COSTECH, FSDT na wengineo yanaweza kuwa na mafanikio makubwa zaidi kama watashirikiana na kampuni ya mawasiliano ya simu  kama Vodacom, TTCL, Airtel n.k. Serikali pia nafasi  kwa kutumia kituo cha kuhifadhi data (Data centre) kujitanua zaidi kibiashara pamoja na kuongeza mapato.

Kampuni za simu wanaweza kushirikiana na vijana ambao tayari wametengeneza programu za simu yaani Mobile Apps au mifumo ya kieletroniki ambayo itawasaidia wafanyabiashara wadogo kuendesha biashara zao. Kuanzia mifumo ya utunzaji wa taarifa za mauzo, kuwapa fursa Watanzania kununua vitu kupitia mitandao pamoja na kufanya malipo baada ya manunuzi. 

Mifumo hii na kieletroniki na mobile apps ziwe zinatolewa bure kwa wafanyabiashara watakahohitaji lakini kwa malipo kidogo kila mwezi kwa ajili ya kuhifadhi taarifa kwenye kituo cha kuhifadhia data ambacho ni cha serikali kinachomilikiwa na TTCL.

Hatua hii itawawezesha vijana kupata ajira, pia kampuni ya TTCL kuingiza kipato na ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini. Jambo hili pia litasaidia ongezeko la matumizi ya malipo ya kielekrotoniki sababu mifumo ya utoaji huduma inaweza kunganishwa na sekta za kifedha pamoja na mitandao ya simu.

Kwa namna nyingine, mifumo hii pia itaweza kusaidia mamlaka ya mapato nchini katika ukusanyaji wa kodi mbalimbali ikiwamo kodi la ongezeko la thamani. Hili linawezekana kwa kuhakisha mifumo hii ambayo itatolewa bure kwa wafanyabiashara mbalimbali kuunganishwa na mfumo wa malipo wa TRA.

Kwa muuunganiko huu basi, serikali itaweza kufahamu mwenendo wa biashara mbalimbali nchini sababu watakuwa na takwimu za kutosha kupitia mifumo hii itakayotolewa bure kwa wafanyabiashara. Taarifa hizi zinaweza kutumika kwa ajili ya kutoa msamaha wa kodi au kupanga mikakati ya kuongeza mapato ya serikali. 

Kwa kutumia taarifa hizi itakuwa ni rahisi kwa wamiliki wa biashara kuweza kupata mikopo mbalimbali ya biashara sababu taarifa zao zitakuwa zimehifadhiwa sehemu salama na taasisi za kifedha zinaweza kuzipata wakati wowote.

Ni wazi kuwa kampuni ya TTCL pia itafaidika kwa kuuza intaneti kwa wateja ambao watakuwa wameunganishwa kutumia mifuo hii. Jambo hili litaweza kuwapunguzia gharama wamiliki wa biashara sababu hawatahitaji kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kujenga mfumo wa kuhifadhi data maana watalipia gharama za mwezi kutokana na ukubwa wa biashara. 

Hii ni moja ya fursa mojawapo inayoweza kutengeneza ajira za kutosha kwa vijana ambao wapo mijini na hawana ajira rasmi. Pia jambo hili litasaidia ongezo la mapato kwa TRA sababu watakuwa wanapata taarifa za uhakika kuliko kutumia makadirio ya kodi unaotumika sasa.

Natoa wito kwa serikali kupitia taasisi zake TTCL, TRA na COSTECH kushirikiana katika jambo hili ili kuweza kusaidia malengo ya serikali ya kuondoa umasikini na kutoa ajira nyingi kwa vijana. Jambo hili linarandana na rai aliyoitoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa mashirika ya umma kushirikiana katika kufanikisha mpango wa serikali wa maendeleo wa miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2022.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles