24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Mashabiki wamuaga Joe Hart, Etihad

Joe Hart
Joe Hart

MANCHESTER, ENGLAND

MLINDA mlango ambaye ameipa klabu ya Manchester City mafanikio makubwa, Joe Hart, usiku wa kuamkia jana aliagwa na mashabiki ambao walijitokeza kwenye mchezo dhidi ya wapinzani wao, Steaua Bucharest, huku Man City ikishinda bao 1-0.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa kipa huyo msimu huu tangu kuwasili wa kocha mpya, Pep Guardiola, ambaye amechukua nafasi ya Manuel Pellegrin.

Guardiola aliweka wazi kuwa hataweza kumtumia mchezaji huyo katika kipindi cha msimu wa Ligi Kuu kutokana na kushindwa kuonesha kiwango kizuri katika ziara ya maandalizi ya msimu mpya.

Tayari kocha huyo anataka kumpa nafasi mlinda mlango wa Barcelona, Claudio Bravo, ambaye amewasili jijini Manchester kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake.

Kutokana na hali hiyo ya kuwasili kwa kipa huyo, Hart aliamini kuwa hana nafasi tena ya kuitumikia timu hiyo na alianza kuwaaga wachezaji wenzake ndani ya kikosi hicho.

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Steaua Bucharest, Hart alipata nafasi ya kulinda lango na inadaiwa kwamba inawezekana kuwa ni mchezo wake wa mwisho katika kikosi hicho.

Mashabiki ambao walijitokeza katika uwanja huo wengi wao walionekana kuwa na mabango yenye ujumbe wa kumuaga pamoja na kuimba nyimbo mbalimbali.

Dakika ya 66 ya mchezo huo, mashabiki walisikika wakiimba wimbo ambao ulikuwa unajulikana kwa jina la ‘Simama kama unampenda Joe Hart’, ambapo walikuwa wanaimba wimbo huo huku wakiwa wanatikisa kichwa na kushika nembo ya klabu hiyo kwenye T-shirt zao.

Hata hivyo, wakati wimbo huo ukiendelea kuimbwa na mashabiki hao, Camera zilimuonesha mchezaji huyo akitokwa na machozi.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Hart alidai kuwa siku hiyo itakuwa ya kukumbukwa katika maisha yake kutokana na mashabiki walivyoonyesha hisia zao.

“Ulikuwa ni usiku maalumu kwangu, naweza kusema kwamba ulikuwa usiku wa kukumbukwa kwangu katika maisha ya soka, najua kila mmoja alikuwa anajua nini kinaendelea ndani ya klabu, lakini japokuwa yote hayo yalikuwa yanaendelea ninashukuru kuwa kila kitu kipo sawa na nitapaacha tulivu pakiwa na uongozi bora.

“Nimekuwa na furaha kwa muda mrefu ndani ya klabu hii, hivyo nitaendelea kuipenda kwa kuwa bado nilikuwa na lengo la kuwa hapa kwa muda mrefu, lakini kutokana na mambo ambayo yalikuwa yanaendelea nilikuwa sina sababu ya kuwa hapa.

“Nitawakumbuka sana watu wa Manchester City kwa kuwa walikuwa wananikubali sana, hivyo nina amani sasa,” alisema Hart.

Hata hivyo, kwa upande wa Guardiola naye alisema: “Najua kwamba Joe ni mfalme hapa. Najua umuhimu wake katika klabu hii. Najua nini amekifanya hapa. Yeye ni sehemu ya historia ya mafanikio ya klabu, lakini kwa sasa amekuwa na kiwango cha chini tofauti na zamani.

“Nilikuwa najua wakati ninajiunga na klabu hii, maamuzi yangu yalikuwa kwenye nafasi hii ya mlinda mlango, hata hivyo, nimefurahishwa na kiwango chake dhidi ya Steaua na nimependa jinsi mashabiki walivyoonyesha ushirikiano wao,” alisema Guardiola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles