Na Mwandishi Wetu- Zanzibar
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amewaonya wamiliki wa shule ambao wanatumia magari mabovu kubebea wanafunzi.
Alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni maalumu ya usalama barabarani na udhibiti wa ajali katika Shule ya Jang’ombe.
Masauni aliwataka wamiliki wa shule kuhakikisha wanatumia mabasi imara kuepusha ajali.
“Wamiliki wa shule wanatakiwa wafuate sheria kwa kuacha kutumia mabasi mabovu na kujaza wanafunzi kupita kiasi.
“Tutatumia kikosi cha usalama barabarani kuhakikisha wanafunzi wanakua salama muda wote wakiwa wanaenda shule na kurudi nyumbani.
“Nawaagiza askari wa usalama barabarani kusimamia sheria wamiliki watakaokiuka sheria hizo waweze kuchukuliwa hatua na madereva watakaobainika kuendesha magari mabovu ambayo ni hatarishi kwa wanafunzi,” alisema Masauni.
Akitoa ripoti ya matukio ya ajali za barabarani, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Shukuru Amir Ally, alisema ajali 229 zimeripotiwa ndani ya mwaka huu tofauti na mwaka 2017 ambako zilikuwa 391.