25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Masaburi afuta kesi dhidi ya Kubenea

Pg 2Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imefuta kesi ya madai ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Ubungo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas Masaburi dhidi ya mbunge wa jimbo hilo, Saed Kubenea (Chadema).

Uamuzi wa maombi ya kufuta kesi hiyo uliwasilishwa mahakamani hapo jana na wakili wa Dk. Masaburi, Clement Kihoko mbele ya Jaji Lugano Mwandambo.

Wakili Kihoko alisema kuwa mteja wake hana nia ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo ya kupinga matokeo.

Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Jaji Mwandambo alisema mahakama imepokea maombi hayo ya kuifuta kesi hiyo.

 

GHARAMA

Baada ya jaji kukubali ombi hilo, Wakili Kihoko aliiomba mahakama kuwapunguzia gharama za uendeshwaji wa kesi ya msingi pamoja na fidia ya usumbufu.

Hata hivyo, Wakili wa Kubenea, Nyaronyo Kicheere, alisema licha ya upande wa utetezi kuomba punguzo hilo, lakini wanapaswa kulipa gharama hizo.

Kutokana na hali hiyo, kuliibuka mvutano wa sheria, jambo lililomlazimu Jaji Mwandambo kuahirisha kesi hiyo kwa muda mfupi, aweze kupitia hoja hizo kabla ya kurudi mahakamani.

Baada ya kurudi, Jaji Mwandambo alisema katika kesi ya msingi mdai anatakiwa kulipa asilimia 50 ya gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.

Alisema katika maombi ya punguzo la uendeshaji wa kesi hiyo, kila upande utalipia gharama zake.

 

KUBENEA ANENA

Akizungumza baada ya kutoka mahakamani, Kubenea aliwashukuru wanachama wa Chadema kumsindikiza mahakamani wakati kesi hiyo ikiendelea.

Hata hivyo, alisema kitendo cha Dk. Masaburi kufuta kesi hiyo kinaonyesha wazi kuwa yeye ni mshindi na   ataliongoza jimbo hilo katika miaka mitano.

“Wagombea wengine waliofungua kesi kama ya Dk. Masaburi wakati hawana uhakika wa kushinda wanapaswa kuzifuta ili waendelee na kazi nyingine,” alisema Kubenea.

Dk. Masaburi alifungua kesi hiyo namba 8 /2015  kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu kwa mbunge wa Ubungo, Kubenea akidai kuwa yeye na mawakala wake hawakuruhusiwa kuona vifaa vya kupigia kura kama ilivyofanyika kwa Kubenea na mawakala wake.

Vilevile alidai Kubenea alitoa rushwa ya jenereta katika Hospitali ya Mavurunza  iliyopo Kimara, zawadi ya meza ya mchezo wa pool  kwa vijana wa Makuburi na kujenga barabara ya Matete huko  Kimara akiwashawishi kumchagua.

Dk. Masaburi pia alimlalamikia msimamizi kukataa kuhakiki kwa mara ya pili matokeo yake ikiwamo na watu kadhaa wa maeneo ya Mizizini, Mianzini, Kilimahewa, Mizambarauni, Shule ya Mugabe na Kanuni, kutokupiga kura.

Pamoja na Kubenea, washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ubungo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mawakili wengine kwa upande wa Kubenea walikuwa Tundu Lissu, Mabere Marando, Peter Kibatala, Method Kimomogolo na Frederick Kihwelo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles