Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Shirika la Afya Marie Stopes imezindua huduma za mbalimbali zinazotolewa bure jijini Mwanza ikiwamo huduma ya afya ya uzazi, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti, upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kupatiwa ushauri wa daktari.
Huduma hizo zilizoanza kutolewa kuanzia Novemba 15 hadi 19, ni sehemu ya uzinduzi wa kituo kipya kulichopo Ghana mkabala na Jengo la Rock City jijini Mwanza baada ya kutoka katika kituo kilichokuwa Nyegezi mkabala na kituo cha mabasi.
“Sasa tumehamia mtaa wa Ghana Mkabala na Rock City Mall. Hivyo tunachukua fursa hii kuwakaribisha wateja wetu katika makazi mapya yaliyoboreshwa zaidi . Huduma zote zinaendelea kama kawaida na tumeongeza wigo kwa upande wa wataalamu tunategemea kuwa na daktari bingwa wa watototo na daktari bingwa wa akina mama ambao watakuwa wakitoa huduma kwenye kituo hiki.
“Huduma nyingine ni huduma za afya ya uzazi , afya kwa ujumla , kliniki kwa akina mama na Watoto, vipimo vya ultra sound na vipimo vya maabara, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matibabau ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi , chanjo na uchunguzi wa homa ya ini,” imesema taarifa iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wa Marie Stopes, Ester Shedapha.
Aidha shirika hilo limeiishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto, Wizara Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano na kuhakikisha wanawafikia wananchi wa Mwanza kwa elimu na huduma za afya ya uzazi na afya kwa ujumla.
Pamoja na Marie Stopes imeazimia kupanua wigo wa huduma zake kimawasiliano kwa wateja kwa kuwaweka karibu ambapo kupitia namba ya bure mteja anaweza kuhudumiwa wakati wowote kupitia 0800 753 333 .