Na Waandishi wetu – dar es salaam
UBALOZI wa Marekani nchini, umeeleza kusikitishwa na vurugu na ukiukwaji wa sheria, vilivyojitokeza wakati wa uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita Jimbo la Buyungu na katika kata 36.
Taarifa iliyotolewa jana na ubalozi huo, ilisema; “Marekani imesikitishwa na uendeshaji wa chaguzi ndogo zilizofanyika nchini Tanzania Agosti 12, 2018.
“Taarifa za kuaminika zinaonyesha kuwa chaguzi ziligubikwa na vurugu zilizohusiana na uchaguzi, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kukataa kwa baadhi ya watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwasajili wagombea kutoka vyama vya upinzani, vitisho vya polisi dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani, watu kukamatwa kiholela bila kuwepo vibali vya ukamataji na kukandamizwa kwa uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni katika kipindi chote kuelekea chaguzi hizo.
“Mambo haya yanakwaza haki ambazo Katiba ya Tanzania imewapa raia wake na kuhatarisha amani, utulivu na usalama nchini na katika eneo lote la kanda.”
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Athuman Kihamia, alisema bado hajaliona tamko hilo ila wanajipanga kuelezea hali ya uchaguzi huo wa marudio ikiwamo kulijibu tamko hilo.
“Naomba uvute subira, bado sijaliona hilo tamko, na suala la uchaguzi, tutaeleza vyote ikiwa ni pamoja na kujibu tamko hilo la Marekani,” alisema Kihamia.
MTANZANIA lilimtafuta bila mafanikio Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Suzan Kolimba, kupata ufafanuzi wa wizara kuhusu masikito hayo ya Marekani.
Licha ya kupigiwa simu mara kadhaa hakupokea, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakuujibu.
Naye Ofisa Habari wa Wizara hiyo, Mindi Kasiga, alipotafutwa alisema yupo likizo, hivyo hawezi kuzungumza lolote.
CHADEMA
Juzi Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, ambaye alikuwa Buyungu kuendesha kampeni za uchaguzi huo, alisema wanaendelea kukusanya fomu za matokeo kutoka kwa mawakala wao.
Alisema hadi wakati huo walikuwa na matokeo ya kata tisa, ambayo alidai kuwa yalionyesha walipata kura zaidi ya 18,000, wakati zilizotangazwa ni 16,000.
“Matokeo haya ni tofauti kabisa na waliyotangaza, katika hizi kata tisa ambazo tulifanikiwa kupata matokeo yake, ukijumlisha kata tisa tu, sisi tuna zaidi ya kura 18,000 na CCM wana 19,000.
“Haya matokeo hayajumuishi kata ambazo ni ngome yetu, ambazo mawakala wetu walinyimwa fomu za matokeo, kwenye kata yetu ya Katanga, huko ofisi iliunguzwa, mtendaji akatokomea na fomu, sasa waambieni CCM wawaambie wawaonyeshe hizo fomu,” alisema Mrema.
CCM
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema licha ya kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 58 Buyungu, lakini walishinda kwa tabu.
“Buyungu tulipata tabu kidogo kwa sababu mgombea aliyekuwapo alikuwa anapendwa sana na wananchi, alikuwa ni mwalimu, wanampenda tu na wamemtumia wale watu,” alisema.
Alisema wakati wa kampeni kila kata ilipangiwa mbunge maalumu wa CCM na wote walifanya kazi nzuri kwa kufanya mikutano zaidi ya 25, kuzungumza na viongozi wa dini zaidi ya 12, walimu wa sekondari na shule za msingi, bodaboda na wafanyabiashara wadogo wadogo.
UCHAGUZI ULIVYOKUWA
Uchaguzi wa udiwani katika Kata ya Kaloleni Jimbo la Arusha Mjini, uliingia dosari baada ya kuibuka vurugu huku baadhi ya watu wakiripotiwa kuchomwa visu.
Pamoja na vurugu hizo, gari la mgombea udiwani wa Kata ya Daraja Mbili, Masud Sungwa (Chadema), lilidaiwa kuchomolewa tairi, huku watu waliokuwa ndani walilazimika kushuka na kukimbia kunusuru maisha yao.
Katika vurugu hizo, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kaloleni, lddi Mussa, alidai kuchomwa kisu begani na kujeruhiwa maeneo ya mwili wake na mmoja wa watu aliyekuwa katika kundi la wafuasi wa Chadema waliokuwa wamemzingira.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’anzi, alisema mgombea wa Chadema alishambuliwa na watu wasiojulikana.
“Amekwisha kufungua kesi tayari kituo cha polisi kwa ajili ya kuanza uchunguzi. Aliyechomwa kisu ni mwanachama wa CCM alikuwa eneo la Mianzini jijini hapa,” alisema.
ACT WATOA TAMKO
Katika hatua nyingine, jana Chama cha ACT-Wazalendo kimemvaa Dk. Bashiru, kikidai amepotosha umma kwa kusema CCM imeshinda uchaguzi huo.
Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Doroth Semu, alisema Agosti 13, mwaka huu katika mkutano na waandishi wa habari, Dk. Bashiru alifanya upotoshaji wa wazi ambao hawakudhani kama ungetolewa na mtu wa hadhi yake.
Aliyataja baadhi ya maeneo aliyodai kuwa yalipotoshwa na Dk. Bashiru kuwa ni pamoja na kuvurugwa kwa uchaguzi wa marudio, utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Katika taarifa yake, Dk. Bashiru alizungumzia aliouita ushindi wa ‘mia kwa mia’ wa CCM kwenye uchaguzi wa marudio. Ukweli wa mambo ni kwamba CCM haijashinda kwa haki Buyungu na kwenye kata nyingi katika uchaguzi huu.
“Mfano wa wazi ni wagombea wanane wa vyama vya upinzani kwenye kata za Tunduma kutangazwa kuwa si raia ili CCM iweze kupita bila kupingwa kwenye kata hizo.
“Wapinzani tulibughudhiwa na mikutano yetu kuvamiwa na polisi. Mfano halisi ni wa wagombea wote wa vyama vya upinzani katika Kata ya Turwa wilayani Tarime kuzuiwa kufanya kampeni siku mbili za mwisho ili kutoa mwanya kwa CCM kushinda,” alisema Doroth.
Alisema pia katika uchaguzi huo wa Agosti 12, licha ya mgombea wa upinzani katika Jimbo la Buyungu kushinda, matokeo yaliyotangazwa na tume yalimpa ushindi mgombea wa CCM.
Doroth alisema kutokana na hali hiyo, yanapaswa kufanyika mabadiliko kwenye mfumo wa siasa na vyombo vya dola, ikiwamo kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.
“Tunasisitiza mapendekezo haya yafanyiwe kazi kwa salama ya nchi yetu. Vinginevyo nchi inakwenda kupata tabu sana kuelekea 2020,” alisema Doroth.
Katika uchaguzi wa Buyungu, mgombea wa CCM, Christopher Chiza alitangazwa mshindi, huku chama hicho kikishinda udiwani katika kata 36 na nyingine 41 kikipita bila kupingwa baada ya wagombea wa upinzani kuenguliwa kwa sababu mbalimbali.
MSEMAJI WA SERIKALI
Baada ya taarifa hiyo ya Marekani kuanza kusambaa mitandaoni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, kupitia ukurasa wa Twitter, alisema wanajiridhisha juu ya uhalali wa tamko hilo kisha watatoa tamko.
Maelezo hayo ambayo Dk. Abbasi aliyasambaza mwenyewe kwenye makundi mbalimbali ya mtandao wa Whatsapp, yalisema; “kuna taarifa inasambaa kuhusu kinachodaiwa ni taarifa ya ubalozi mmoja kuhusu masuala ya ndani ya nchi. Tunajiridhisha, tutatoa tamko punde.”
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, Dk. Abbasi alikuwa hajatoa tamko lolote.
Habari hii imendaliwa na GABRIEL MUSHI, ZAKIA NDULUTE (UOI), FRANK KAMUGISHA (SAUT) NA LEONARD MANG’OHA