WASHINGTON, MAREKANI
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema nchi yake haitakubali kutoa msaada wowote wa ziada wa kuijenga upya Syria ikiwa vikosi vya Iran vitaendelea kuwepo nchini humo.
Akizungumza mbele ya kundi la wabunge wanaoiunga mkono Israel, Pompeo ameahidi ataendelea kushinikiza Iran itengwe na kuwekewa vikwazo vikali kabisa kuwahi kushuhudiwa.
“Jukumu la kuifukuza Iran linaangukia mikononi mwa Serikali ya Syria, ambayo ndiyo inayobeba dhamana ya kuwepo kwa wanajeshi wa nchi hiyo nchini humo.
“Ikiwa Syria haitohakikisha wanajeshi wa Iran wanaihama nchi hiyo, basi haitopokea hata dola moja kutoka Marekani,” alisisitiza Pompeo.
Hata hivyo, hakuzungumzia umuhimu wa kuondolewa pia kwa wanajeshi wa Urusi nchini humo.