30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani yajitoa katika mkataba wa nyuklia na Urusi

WASHINGTON, MAREKANI

MAREKANI imejitoa rasmi katika mkataba wa nyuklia na Urusi, hatua inayozusha hofu kuhusu ushindani wa silaha mpya.

Mkataba huo unaohusu zana za nyuklia za masafa ya kati (INF) ulisainiwa na rais wa Marekani Ronald Reagan na kiongozi wa iliyokuwa Sovieti, Mikhail Gorbachev mwaka 1987.

Mkataba huyo ulipiga marufuku makombora ya masafa ya kati ya kilomita 500-5,500.

Hata hivyo mapema mwaka huu Marekani na Nato ziliishutumu Urusi kwa kukiuka makubaliano hayo kwa kufyatua aina mpya ya kombora, jambo ambalo Urusi inalikana.

Marekani imesema ina ushahidi kuwa Urusi imetuma kombora aina ya 9M729 linalofahamika kwa Nato kama SSC-8.

Tuhuma hizo ziliwasilishwa kwa washirika wa Nato wa Marekani ambao wote waliunga mkono madai ya Marekani.

Makombora mapya ya 9M729 ya Urusi yanaitia tumbo joto Marekani na washirika wake.

Rais wa Marekani, Donald Trump mwezi Februari alitangaza kuwa Marekani itajitoa kutoka mkataba huo iwapo Urusi haitotii, na kuweka tarehe ya mwisho kuwa Agosti 2.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin naye amesitisha majukumu ya taifa lake katika mkataba huo muda mfupi baadaye.

“Breki ya thamani katika vita vya nyuklia inaeleka kupotea,” ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, (UN) Antonio Guterres.

“Huenda hili likaongeza na sio kupunguza tishio la makombora,” aliongeza, na kuomba pande zote kutafuta “makubaliano mapya ya mtazamao wa pamoja ya udhibiti wa silaha kimataifa”.

Wachambuzi wanahofia kwamba kutibuka kwa makubaliano hayo ya kihistoria huenda kukachangia ushindani mpya wa silaha kati ya Marekani, Urusi na China.

“Kutokana na kuvunjika kwa mkataba huo sasa, tutashuhudia utengenezaji na utumiaji wa silaha mpya,” Pavel Felgenhauer, mchambuzi wa zana za Urusi ameliambia shirika la habari la AFP  na kuongeza kuwa  

“Urusi tayari ipo tayari.”

Mwezi uliopita, Katibu mkuu wa Nato, Jens Stoltenberg aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kuwa makombora ya Urusi – ambayo alisema kuwa ni “ukiukaji wa wazi wa mkataba huo” – yana uwezo kama yale ya nyuklia, ambayo ni magumu kuyadhibiti na yanaweza kufika katika miji ya Ulaya katika muda wa dakika.

“Hili ni jambo zito, mkataba wa INF umekuwa jiwe la msingi katika udhibiti wa silaha kwa miongo kadhaa, na sasa tunashuhudia kuvunjika kwa mkataba huo .” alisema na kuongeza;

“hakujakuwepo  na ishara zozote kuwa Urusi itatii na makubaliano hayo ni lazima tujitayarishe kwa ulimwengu usiokuwa na mkataba wa INF na ulio na makombora zaidi ya Urusi,”.

Stoltenberg pia alisema kuwa uamuzi wowote wa Nato kuhusu namna gani ya kujibu utatolewa baada ya kupita muda huo wa mwisho uliotolewa.

Nato haina mpango wa kutuma makombora yake ya ardhini Ulaya lakini makombora ya angani na ya ulinzi, ya mazoezi na utayari wa vikosi vyake na mipango mipya ya udhibiti wa silaha huenda yakawa ni sehemu ya jibu lake.

Mkataba wa INF

Kiongozi wa iliyokuwa Sovieti Mikhail Gorbachev na rais wa Marekani Ronald Reagan walisaini mkataba wa INF mnamo mwaka 1987.

Mkataba huo ulipiga marufuku silaha zote za nyuklia na makombora yasio ya nyuklia ya masafa marefu na ya wastani isipokuwa ya baharini.

Marekani ilikuwa na wasiwasi kuhusu kutumwa kwa kombora la SS-20 la Sovieti mwaka 1979 na ilijibu kwa kuweka makombora ya masafa mafupi ya ardhini Ulaya – hatua iliyozusha maandamano makubwa.

Kufikia mwaka 1991, takriban makombora 2,700 yaliharibiwa.

Mataifa hayo mawili yaliruhusiwa kukagua hifadhi za taifa mwenza.

Hata hivyo mambo yalianza kuharibika mwaka 2007, baada ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin kutangaza kuwa mkataba huo haushughulikii maslahi ya Urusi.

Hilo lilifanyika baada ya rais wa Marekani George W Bush, mwaka  2002, kuitoa Marekani katika mkataba wa kupinga makombora ya masafa ya juu, uliopiga marufuku silaha zilizoundwa kuzuia makombora ya aina hiyo.

Mwaka 2014, rais wa wakati huo Marekani Barack Obama aliishtumu Urusi kwa kukiuka mkataba huo wa INF baada ya kutuhumiwa kufanya majaribio ya kombora la ardhini.

Inaarifiwa aliamua kutojitoa katika mkataba huo chini ya shinikizo la viongozi wa mataifa ya Ulaya, waliosema hatua kama hiyo huenda ikachangia ushindani wa umiliki wa silaha.

Mwaka jana, Nato ikaunga mkono tuhuma za Marekani na kuishutumu rasmi Urusi kwa kukiuka mkataba huo.

“Washirika wamehitimisha kuwa Urusi imeunda na kutumia kombora 9M729, hatua inayokiuka mkataba wa INF na kuzusha hatari kwa usalama kati ya Ulaya na Atlatiki,” taarifa kutoka mawaziri wa mambo ya nje wa Nato ilieleza.

Taarifa hiyo ilisema mataifa wanachama “yanaunga mkono” tuhuma za Marekani kuwa Urusi inakiuka mkataba huo, na kutoa wito kwa Urusi kurudi na kutii mkataba huo.

Hata hivyo Urusi ilikana tuhuma hizo ikisema ni kisingizio kwa Marekani kujito akatika mkataba huo.

Wakati nchi hizo mbili zikiwa na sintohamu hiyo mwezi uliopita Uturuki mwezi ilipokea sehemu ya kwanza ya mfumo wa kombora la ulinzi S-400 kutoka Urusi hatua ambayo ilipata upinzaji mkali kutoka Marekani.

Marekani iliionya Uturuki  ikisema haiwezi kumiliki kwa pamoja mfumo huo wa S-400 na ndege za kivita za Marekani aina ya F-35.

Uturuki na Marekani sio washirika wa Nato lakini Uturuki imekuwa na ushirikiano wa karibu na Urusi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles