32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani kuondoka Syria kutasababisha damu kumwagika upya

RAIS Donald Trump wa Marekani ameamua kuyaondoa majeshi ya nchi yake kutoka Syria. Uamuzi huo unaweza ukaiingiza Mashariki ya Kati yote katika machafuko. Unaweza ukasababisha kuwapo pengo ambalo kwamba mataifa tafauti yatataka kulijaza.

Serikali ya Syria, Wakurdi, Urusi, Iran, Israel na Uturuki wote wana maslahi yao katika Syria. Pale wanajeshi wote karibu 2000 wa Marekani watakapoondoka kutoka eneo hilo yawezekana mivutano mipya ikazuka na ile iliyoko sasa ikaongezeka. Kuna hatari ya kutokea machafuko, ghasia na damu kumwagika.

Ili kuwatuliza washirika wa Marekani, mshauri wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo, John Bolton, ameahidi kwamba wanajeshi hao wataondoka Syria pale wanamgambo wa kigaidi wa Dola ya Kiislamu (ISIL) watakaposhindwa kabisa na pale Uturuki nayo itatoa dhamana juu ya usalama wa wanamgambo wa Wakurdi wa Chama cha YPG ambao ni washirika wa Marekani katika vita vyake dhidi ya ISIL.

Tamko hilo la Bolton lilipingwa na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki ambaye aliahidiwa na Rais Trump kwamba kuondoshwa majeshi ya Marekani kutoka Syria ni jambo ambalo yeye Trump ameshaliamua bila pingamizi yoyote.

Tangazo la Trump liliwashangaza watu wengi duniani, seuze tena washauri wake katika Wizara za Ulinzi na Mambo ya Kigeni na pia kuufanya mji mkuu wa Washington uingie katika hamkani. Hasa kwa kwa vile tangazo hilo lilitolewa muda mfupi sana baada ya rais huyo kutangaza kwamba majeshi ya nchi yake yamewashinda kabisa wapiganaji wa ISIL.

Lilikuwa ni tangazo lililokwenda kinyume na siasa yake mwenyewe kuelekea Mashariki ya Kati yaani kuizingira Iran na kuzivunja tamaa za nchi hiyo za kupanua ushawishi wake katika eneo hilo kwa vile inaweza ikaacha pengo kwa Iran na nchi nyingine kulijaza.

Trump alisema wavulana wetu, wasichana wetu, watu wetu sasa wanarejea nyumbani. Tumeshinda. Na hivyo ndivyo tunavyotaka. Na hivyo ndivyo walivyotaka.

Uamuzi wa Trump wa kuachana na Syria unatimiza malengo ya Rais Vladimir Putin wa Urusi na unazusha tetesi mpya juu ya madhumuni ya Trump katika uhusiano wake na Urusi, jambo ambalo linazidi kuchunguzwa.

Siku chache kabla, utawala wa Trump uliliambia Bunge huko Washington kwamba unaondoa vikwazo kwa kampuni mbili za Urusi. Trump analaumiwa ndani na nje ya Marekani kwamba hana msimamo unaotambulika.

Na uamuzi huu wa kuondoka Syria unafungua njia ya yeye kulaumiwa waziwazi kwamba ni ndumilakuwili, kwa vile ni yeye Trump aliyemlaumu mtangulizi wake, Barack Obama, kwamba ni  mwanzishaji wa ISIL, baada ya kikundi hicho cha kigaidi kufaidika na kuondoka majeshi ya Marekani kutoka Iraq mwaka 2011.

Si siri kwamba Trump anaamini kwamba majeshi ya Marekani yasipigane katika vita anavyoviona kuwa ni vita vya watu wengine na anauona ushirika wake na mataifa mengine ni tu nafasi kwa washirika hao wa jadi wa Marekani kuzidi kuichuna kifedha Marekani.

Je, Marekani inataka kuwa polisi wa Mashariki ya Kati, huku haipati chochote, lakini tu kutumia mapesa, matrilioni ya dola na roho za vijana wake? Tena washirika hao hawathamini nini sisi tunfanya? Je, tunataka sisi tubakie Mashariki ya Kati maisha? Aliuliza Trump katika mtandao wake wa Twitter.

Lakini bado kuna watu wengine wanaouona uamuzi wake huo kuwa ni makosa makubwa katika  siasa ya kigeni ya Marekani.

Eneo lililoko Kaskazini Mashariki ya Syria ni muhimu katika mikakati ya kivita. Kwa Rais Bashaar al-Assad wa Syria eneo hilo si tu muhimu katika kurejesha mamlaka yake katika nchi nzima. Eneo hilo hapo kabla lilikuwa lenye kutoa chakula kingi (ngano) kwa nchi hiyo. Pia kutoka eneo hilo Bwawa la Mto Euphrates linatoa umeme na kunapatikana visima vikubwa kadhaa vya mafuta. Bila ya kulidhibiti eneo hilo itakuwa wazi ni taabu zaidi kwa Assad kuijenga upya nchi yake baada ya vita.

Lakini, pia wanamgambo wa Kikurdi wanagharamia harakati zao kutokana na mapato wanayoyachuma kutoka eneo hilo. Wakurdi kulidhibiti eneo hilo ni hatua ya kuelekea ile ndoto yao ya muda mrefu ya kuwa na serikali yao ya mambo ya ndani katika Kaskazini ya Syria. Uturuki inaziona juhudi za Wakurdi kutaka kuwa na utawala wao wa mambo ya ndani katika upande wa Syria kuwa ni kitisho kwake na imetangaza waziwazi na tena mara kadhaa kwamba italizuia jambo hilo kufa na kupona.

Kuondoka majeshi ya Marekani kutoka Syria kunafungua mlango wazi kwa Rais al-Assad na Warusi wanaomuunga mkono. Kizingiti pekee ambacho kilimzuia Assad kuidhibiti tena sehemu ya Mashariki ya nchi ni kuwapo wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo ambao pia walimaanisha kuwa ni himaya kwa wanamgambo wa Kikurdi. Bila ya msaada wa Marekani, wapiganaji wa Kikurdi watalazimika wasikilizane na Urusi pamoja na utawala wa Assad ili wapate uhakika wa ulinzi dhidi ya adui wao mkubwa Uturuki.

Haitarajiwi kwamba Dola ya Kiislamu (ISIL) itatoweka kabisa. Badala yake wapiganaji wake wataendelea kuendesha harakati zao katika eneo hilo hata kama litashikiliwa na wanajeshi wa Assad.

Wanajeshi wa Kituruki pamoja na waasi 15000 wa Syria tayari wameanzisha hujuma huko Mashariki ya Syria ili kuwaondoa wanamgambo wa Kikurdi katika mpaka wa Syria na Uturuki. Hali hii si tu itasababisha kuwapo mvutano na Marekani, lakini pia na Urusi.

Zaidi ya hayo ni kwamba hali hii inaweza kufanya usifanye kazi ule mkataba wa kusitisha mapigano katika Mkoa wa Idlib ulioko Kaskazini Mashariki. Mkataba huo ulifikiwa baina ya majeshi ya Assad na waasi kwa upatanishi wa pamoja baina ya Uturuki na Urusi.

Pindi Serikali ya Syria itayapanua mamlaka yake kamili katika eneo la Mashariki ya nchi, basi Iran nayo itataka pia ifaidike na matunda ya ushindi wa vita alioupata Assad. Iran ilimsaidia sana Assad kwa hali na mali katika Vita vya Syria.

Iran, bila shaka, itataka ule upenu wa njia unaowezesha kutuma silaha na bidhaa kwa Chama cha Hizbullah cha Lebanon unaopitia Syria upanuliwe zaidi. Israel hivi sasa inastushwa na hali ya mambo inavyoendelea huko Syria na huenda ikazidisha mashambulizi yake ya angani dhidi ya vituo vya kijeshi vinavyoshukiwa ni vya Iran nchini Syria.

Rais Trump anahisi kazi ya jeshi la nchi yake katika Syria kupigana dhidi ya ISIL imemalizika. Kwa hivyo, hakuna sababu tena kwa Marekani kubakia na kujiingiza katika mizozo ya Syria.

Lakini wachunguzi wa mambo miongoni mwa Muungano wa Kijeshi unaoongozwa na Marekani huko Syria wanaonya kwamba baada ya kuondoka wanajeshi wa Marekani huenda wapiganaji wa ISIL wakachipuka upya. Pia wasiwasi unaozidi miongoni mwa makabila ya Kiarabu katika Mashariki ya Syria kutokana na ubabe uliooneshwa na Wakurdi hivi karibuni, unaweza ukawa chemchemi ya mivutano upya.

Kweli, maafa ya vita vya Syria bila shaka yamechangiwa sana na kujiingiza mataifa kadhaa ya nje katika mambo ya ndani ya nchi hiyo. Lakini kiroja cha mambo ni kwamba hata sasa kuondoka moja ya mataifa hayo ya nje tena taifa lenyewe ni kubwa na lenye nguvu, yaani Marekani kunaleta hali ya wasiwasi. Vipi kuuvunja mduara huo si jambo rahisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles