24.6 C
Dar es Salaam
Thursday, December 2, 2021

Waziri Hasunga: Maeneo yanayohitaji kurekebishwa, kufanyiwa kazi ni mengi

MWANDISHI WETU

SERIKALI ina mpango kabambe wa kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa lengo la kupata chakula cha kutosha, kuongeza tija katika uzalishaji na thamani ya mazao.

Tangu alipoteuliwa mwishoni mwa mwaka jana, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, amekuwa akizunguka katika mikoa mbalimbali nchini kuzungumza na wakulima, watendaji katika wakala na taasisi zilizo chini ya wizara yake na kuweka mipango ya kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo.

Hasunga alisema wameweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika utendaji pamoja na kujitathmini kabla ya kufikia nusu mwaka ya utekelezaji wa bajeti ya wizara ya mwaka 2018/2019 ili kujipanga kwa mwaka ujao wa 2019/2020.

“Maeneo yanayohitaji kufanyiwa kazi ni mengi na tunashirikiana vizuri na manaibu mawaziri wangu na watendaji wengine wa wizara kuhakikisha tunayapatia ufumbuzi yote,” anasema Hasunga.

Korosho

Hasunga alisema uamuzi uliochukuliwa na Serikali katika zao la korosho unalenga kuongeza kipato kwa mkulima, kutoa ajira mpya kwa kuzibangua korosho ndani ya nchi na kuliongezea thamani zao hilo kwa kulifungasha kabla ya kusafirisha nje ya nchi na kuongeza pato la taifa.

 “Wananchi wote waliouza korosho nawahakikishia kwamba Serikali inazo fedha za kutosha na tutawalipa wote na zoezi la uhakiki tunaliharakisha ili watu wote walipwe haraka.

“Tutahakikisha kufikia Januari 31, mwaka huu zoezi la uhakiki liwe limekamilika kwa asilimia 100 ili angalau asilimia 80 tuwe tumewalipa ili Februari mwanzoni tuwe tumemaliza wote.

 “Tukishauza korosho tutarudi tuone vyama vya msingi, vyama vikuu vya ushirika vinatakiwa vipate kiasi gani, wasafirishaji, wenye magunia na wengine wote watakuja kupata fedha zao baada ya mauzo,” anasema Hasunga.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mojawapo ya mikakati ambayo wameweka kuhakikisha uzalishaji unaendelea ni kukiimarisha Kituo cha Utafiti cha Naliendele ambacho hadi sasa kimeshasambaza miche ya korosho 37,816.

“Lakini tumewawekea mkakati wa kuzalisha mbegu za kutosha na hadi sasa wanazo tani za mbegu 40.1 zenye uwezo wa kutoa miche milioni 5.6.

“Nawaomba wananchi wawasiliane na vituo vyetu ambavyo viko saba nchi nzima wanunue kiwango cha mbegu wanachohitaji na bei si kubwa, kilo moja ni Sh 5,000 tu,” anasema.

Alisema kama mbegu hizo zitatoa miche milioni 5.6 wana uwezo wa kuongeza ekari 330,491 na baada ya miaka mitatu watafika mbali.

“Wananchi waendelee kuongeza tija kwenye uzalishaji wa korosho na kama Serikali tumejiwekea lengo, tunataka mwakani tufikie uzalishaji wa tani 350,000. Lengo tunataka ifikapo mwaka 2023 tuwe tumefikia tani 600,000,” anasema.

Hasunga alisema Serikali inatarajia kuanza kuwasajili wakulima wote ili waweze kutambua idadi yao na uwezo wao wa kuzalisha.

Alisema usajili huo utafanywa na wizara kwa kushirikiana na bodi za mazao na ifikapo Juni wakulima wote watakuwa wamesajiliwa na kupatiwa vitambulisho.

“Tunataka wakulima wasajiliwe tuwajue, anaitwa nani, analima wapi, shamba lina ukubwa gani, ana miche mingapi na ana uwezo wa kuzalisha kiasi gani na je, alichouza kinalingana na alichozalisha shambani.

“Lengo hatutaki tuwe na wafanyabiashara katikati ambao wanawanyonya wakulima, hawana leseni, hawalipi kodi lakini wanapata mapato makubwa sana,” anasema Hasunga.

Alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha inakuwa na mipango sahihi ya kuwaendeleza wakulima kuanzia kwenye kilimo chenyewe hadi kufikia hatua ya kuvuna, kuhifadhi na kulifikia soko.

“Usajili wa wakulima utarahisisha kuweza kufikiwa kirahisi na wataalam na kuongezewa weledi na ujuzi na kushughulikia mahitaji yao kisasa na kwa haraka zaidi kwani wengi wamekuwa wakilima bila kufuata taratibu za kilimo,” anasema.

Pia anasema watasimamia kwa weledi uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora na kwa wingi ili wakulima waweze kunufaika katika uzalishaji wenye tija kwa kilimo cha kibiashara.

Ununuzi wa mazao

Hasunga alisema wanaimarisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na kuanzia mwakani itafanya kazi ya kununua mahindi na mazao mengine.

“Tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha tunaongeza uzalishaji, lakini pia tuongeze tija, badala ya kuzalisha mahindi magunia 10 kwa ekari yafike 25 tukitumia kilimo cha kisasa,” anasema Hasunga.

Alisema wanajitahidi kuhakikisha pembejeo zinafika kwa wakati na kwa bei nzuri ili wakulima wazalishe zaidi, kipatikane chakula cha kutosha na mazao ya biashara.

Hasunga anasema wataendelea kutafuta masoko zaidi na kwamba wataanza kununua tena mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na zaidi ya tani 13,000 zitanunuliwa kutoka mkoani Ruvuma.

“Tulikuwa hatujaweka mkazo sana kwenye utafutaji wa masoko na tunakusudia kuwa na kitengo maalumu kitakachoshughulikia masoko ya ndani na nje na kitashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kila uzalishaji utakaofanywa masoko yawe yameshabainishwa… ‘Market intelligence’ itasaidia kukiweka kilimo chetu katika hali nzuri,” anasema.

Alisema NFRA lazima wanunue nafaka ya kutosha kwa niaba ya Serikali huku wakiwasaidia wananchi katika suala zima la masoko na bei.

Hasunga alisema pia ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa (Silos) katika maeneo nane ya kanda saba za wakala huo utaongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Mradi huo wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi umeanza kutekelezwa katika Manispaa ya Songea (Ruvuma), Dodoma, Mpanda (Katavi), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga Mjini (Shinyanga) na Babati (Manyara).

Alisema katika kutekeleza mradi huo, Serikali ya Tanzania na Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola za Marekani milioni 55 sawa na Sh bilioni 124.

Hasunga alisema mradi huo utasaidia kuongeza uwezo wa hifadhi ya chakula, kupunguza gharama za uendeshaji badala ya kutumia magunia, vibarua na gharama nyingine.

“Ni imani yetu kwamba mradi huu na mingine saba inayoendelea katika maeneo tofauti itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa NFRA na kufanya mahindi yote yatakayonunuliwa na kuhifadhiwa kuwa na bei nzuri,” anasema.

Alisema mikakati mingine ni kuongeza tija na matumizi ya mbolea katika maeneo mbalimbali kwa sababu katika maeneo mengi wakulima hawazingatii tija.

“Kama kwenye mahindi mkulima akilima kitaalamu anaweza kupata kati ya magunia 25 hadi 40 kwa ekari.

“Ukienda kwenye zao kama la pamba sasa hivi uzalishaji katika ekari moja ni takriban kilo 300 wakati kama wangeongeza tija kwa kutumia utaalamu wa kisasa, wakapanda kwa hatua zinazostahili, wana uwezo wa kuzalisha hadi kilo 2,000.

“Tunaweka mkazo zaidi katika kuongeza tija, matumizi bora ya mbegu, mbolea na kutumia utaalamu,” anasema.

Ushirika

Hasunga alisema pamoja na mambo mengine, mipango ya Serikali ni kupitia upya sheria ya uanzishwaji wa vyama vya ushirika ili kuondoa changamoto za kiuendeshaji zilizopo sasa.

“Tunataka kupitia upya sheria ya uanzishwaji wa vyama vya ushirika ili kuoanisha sifa zinazotajwa na hali halisi iliyopo ili wananchi wanapochagua viongozi wazingatie sifa tajwa.

“Kwenye zao la korosho ushirika upo vizuri, lakini kuna changamoto nyingi za kiuendeshaji, zinatokana na uwezo wa viongozi wengi wanaoendesha na kusimamia vile vyama vya ushirika, namna ya kuweka kumbukumbu za wanachama na kumbukumbu za kilo na mauzo.

“Kuna ujanja ujanja mwingi unatumika na ndiyo tatizo ambalo tumeliona ni kubwa, hasa katika zoezi hili la uhakiki linaloendelea (akimaanisha kwenye korosho),” anasema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,646FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles