Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Ikulu Dar es Salaam jana.
Mkapa na Rais Magufuli walikutana ikiwa siku chache baada ya kiongozi huyo wa nchi alipokutana na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Kikwete ambaye bado ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa na mazungumzo na Rais Magufuli, Ikulu Dar es Saalam.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugeniz ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa Rais Magufuli pia alipokea ujumbe wa Rais wa Guinea Bissau, Jose’ Mario Vaz.
Kiongozi huyo wa Guinea Bissau alimhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali, hususan katika uchumi kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Rais Jose’ Mario Vaz aliyasema hayo katika ujumbe wa barua uliwasilishwa kwa Rais Magufuli na Mjumbe maalum wa Rais huyo, Jenerali Omar Embalo, Ikulu Dar es Salaam jana
“Napenda kusisitiza kuwa nchi zetu ni marafiki wa muda mrefu, naomba urafiki na uhusiano huu mzuri uendelee na ninakuhakikishia kuwa nchi yangu itaendelea kuuenzi ushirikiano huu,” ilieleza sehemu ya ujumbe huo.
Rais Vaz alimpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuiongoza Tanzania na amemualika kuitembelea Guinea Bissau ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Naye Rais Magufuli alimshukuru Rais Jose Mario Vaz kwa kumtuma mjumbe maalum kwa ajili ya kumletea ujumbe wa pongezi, na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Guinea Bissau.
“Nakushukuru sana Jenerali Umaro Sissoco Embalo kwa kuniletea ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau na nakuomba umwambie namshukuru kwa pongezi, mimi na serikali yangu tupo tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano,” alisema Rais Magufuli.