- Uzalishaji umeongezeka kutoka tani 43,625 hadi 68,147
MWANDISHI WETU-SONGWE
SERIKALI imepanga kubadilisha kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kwa kuzingatia mazao ya kipaumbele.
Miongoni mwa mazao hayo ya kipaumbele ni kahawa ambapo katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Kahawa imepanga kuongeza uzalishaji kutoka tani 65,000 hadi tani 80,000. Aidha bodi imepanga kuzalisha na kusambaza miche milioni 10 ya kahawa katika wilaya 42.
Zao hilo lina mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa na kwa maendeleo ya jamii lakini katika miaka ya karibuni lilionekana kuzorota kutokana na kuwapo kwa changamoto mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo Serikali imeendelea kubuni mikakati mipya ya taratibu za usimamizi wa sekta hiyo ili kuleta ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.
Mojawapo ya mikakati hiyo ni kuanzishwa kwa minada ya kanda ya kahawa ambayo itakuwa ikiendeshwa katika kanda nne zinazohusika na uzalishaji wa kahawa.
Kanda hizo ambazo minada itafanyika ni Kanda ya Mbeya/Songwe ambapo mnada unafanyika Mbozi, Kanda ya Ruvuma/Njombe (Mbinga – Ruvuma), Kanda ya Ziwa (Bukoba – Kagera) na Kanda ya Kaskazini (Moshi – Kilimanjaro).
Kabla ya uamuzi huo kampuni za watu binafsi zilikuwa zikinunua kahawa kwa wakulima na kusababisha baadhi ya wakulima kuuza kahawa ikiwa mbichi kwa lengo la kupata fedha za haraka.
Kwa utaratibu wa sasa vyama vya msingi vy ushirika ndivyo vyenye jukumu la kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima na kuipeleka kwenye viwanda kwa ajili ya kuikoboa na baadaye kuipeleka mnadani.
Wiki iliyopita Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alizindua minada ya Kahawa Kanda ya Mbeya – Songwe na kusema kuwa kuanza kwa minada ya kanda ya kahawa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuwa kuanzia msimu wa kahawa 2019/2020 Bodi ya Kahawa ianze kuendesha minada ya kahawa katika kanda nne za uzalishaji wa kahawa.
Anasema tija katika uzalishaji wa kahawa kwa wakulima wadogo wa kahawa ni ndogo ukilinganisha na wakulima wa mashamba makubwa na wakulima wa kahawa wa nchi nyingine.
Kwa mujibu wa Hasunga, wastani wa tija kwa mti mmoja wa kahawa ya Arabika ni gramu 350 ikilinganishwa na kilo moja (gramu 1,000) kwa nchi za Brazil na Vietnam.
Anazitaja sababu kubwa zinazosabisha tija ndogo kwenye kahawa kuwa ni pamoja na matumizi madogo ya mbolea na virutubisho kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji na wakulima kutozingatia kanuni za kilimo bora cha kahawa ambapo wengine wamekuwa hawatunzi kabisa miti na huvuna tu kile kitakachopatikana.
“Sababu nyingine ni uwepo wa magonjwa na wadudu waharibifu wa kahawa, miti iliyozeeka na kupoteza uwezo wa kuzaa vizuri badala ya kutumia miti iliyoboreshwa yenye uwezo mkubwa wa kuvumilia magonjwa na kuzaa sana. Nimeambiwa mti wa mmoja ulioboreshwa unao uwezo wa kuzalisha wastani wa kilo tatu hadi tano za kahawa kavu,” anasema Hasunga.
Hata hivyo anasema ili kuhakikisha sekta hiyo inaondokana na changamoto ya tija ndogo na uzalishaji, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kuongeza kasi ya upatikanaji wa miche bora ya kahawa kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI).
Anasema kumekuwa na ruzuku ya miche inayotolewa na Bodi ya Kahawa na kuanzisha utaratibu wa upatikanaji wa mikopo ya mbolea kwa wakati kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na sekta binafsi.
Waziri huyo anasema hatua hizo zimewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa kutoka tani 43,625 za kahawa safi msimu wa mwaka 2017/2018 mpaka kufikia tani 68,147 msimu wa 2018/2019.
“Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kahawa na kuhakikisha inaendelea kutoa mchango mkubwa katika kupunguza umaskini, kuongeza pato la taifa na kuongeza ajira kupitia viwanda mbalimbali vya kahawa.
“Ili kufikia lengo la kuwa na Tanzania ya Viwanda, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuhamasisha matumizi ya miche bora ya kahawa kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima, kuimarisha mazingira ya biashara na kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya kahawa ili kuiwezesha kutoa mchango unaohitajika katika kujenga Tanzania ya viwanda,” anasema.
Waziri huyo anawataka wakulima wote nchini kupitia vyama vya ushirika kuweka mkakati wa kununua na kutumia mitambo ya kuchakata kahawa ili kuongeza ubora wa kahawa inayozalishwa na kupata bei nzuri mnadani au kwenye soko la moja kwa moja.
Anazitaka halmashauri kupitia vyanzo vyake vya mapato kuendelea kuwekeza katika uendelezaji wa zao la kahawa ikiwemo uzalishaji wa miche, ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kuchakata kahawa na kuwawezesha wakulima na maofisa ugani kupata mafunzo ya kilimo bora cha kahawa ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi.
Hasunga anasema ili kulinda ubora wa kahawa, matumizi ya mitambo ya kisasa ya kuchakata kahawa hayaepukiki na kwamba nchini kuna takribani mitambo 481 ambayo bado haitoshelezi ukilinganisha na kiasi cha kahawa kinachozalishwa.
“Nawasihi wadau wote waone umuhimu wa kuwa na mitambo hii kwa sababu ili upate kahawa nyingi zenye sifa za ubora unaofanana ni lazima kuwepo na matumizi makubwa ya mitambo tena kwa kuzingatia hatua zote za uchakataji wa kahawa,” anasema Hasunga.
Waziri huyo anasema lengo la Serikali ni kuona kahawa zote zinaandaliwa katika mitambo ya kisasa ili zipate bei nzuri katika masoko kwa lengo la kuimarisha tija katika uzalishaji na kutafuta masoko ya mazao nje na ndani ya nchi.