24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mapinduzi ya elimu

Pg 1Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

SERIKALI imetangaza kuwa itaanza kutoa elimu ya sekondari bure kuanzia Januari 2016, ili kila Mtanzania awe na elimu ya kidato cha nne katika miaka ijayo.
Imesema sambamba na kutoa elimu ya sekondari bure, sera mpya ya elimu na mafunzo inaelekeza utaratibu wa kupanga ada kwa shule binafsi ili kupunguza malalamiko ya wazazi ya kulipa fedha nyingi kwa elimu za awali.
Uamuzi huo wa serikali ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete, wakati akizinduzi Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ambayo ni matokeo ya kuhuishwa na hatimaye kufutwa kwa Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1996, Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999 na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Elimu ya Msingi ya Mwaka 2007.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika katika Shule ya Msingi Majani ya Chai iliyopo Kipawa, Rais Kikwete alisema sera hiyo ni mwanzo wa nguvu mpya ya kuendeleza elimu kitaifa na kimataifa, hivyo lazima iwe kielelezo cha utashi wa kupanga mikakati ya kuinua elimu nchini.
Alisema ukombozi wa elimu ni nyenzo ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kati, hivyo ni jambo la lazima kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya kidato cha nne.
“Baada ya uzinduzi huu, kuanzia mwaka ujao tunataka kuondoa ada za shule za sekondari ili mtoto anayeanza asilipe Sh 10,000 wala Sh 20,000, ili miaka saba ijayo tuhakikishe kila mtu ana uwezo wa kufika form four (kidato cha nne), lengo tufike mahali elimu ya msingi iishie kidato cha nne,” alisema Rais Kikwete.

Alisema ili kukamilisha mpango huo, shule za msingi nchini zinapaswa kujiandaa kujenga shule za sekondari na wenye dhamana ya utekelezaji wa kazi hiyo wahakikishe kila mtoto anapata elimu ya awali kabla ya kujiunga na shule ya msingi.
“Lengo ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe nchi ya kipato cha kati, pato la wastani liwe dola 3,000, kwa sasa tupo katika dola 977, naamini miaka kumi ijayo tutafikia hapo kwa sababu ya mabadiliko na zana ambazo zitahitajika katika elimu, hakuna maendeleo bila elimu,” alisema Rais Kikwete.
Ada shule za binafsi na mitaala
Akizungumzia ada zinazotozwa na shule binafsi, Rais Kikwete alisema sera mpya ya Elimu na Mafunzo inasisitiza elimu ni huduma, hivyo utaratibu wa kupanga ada kwa shule binafsi ni lazima uzingatiwe ili kupunguza malalamiko ya wazazi kulipa fedha nyingi kwa watoto wa elimu za awali.
“Zipo kindergarten (shule za awali) zinatoza ada kubwa kushinda chuo kikuu, mtu mtoto anakwenda kuchezacheza tu analipa milioni mbili, wakati chuo kikuu unalipa Sh mil 1.5. Sijadharau shule zao, lakini tuangalie na kiwango cha elimu kinachotolewa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema shule binafsi zinazotaka kutoza ada kubwa zinapaswa zithibitishe kiwango cha ubora wa elimu wanayotoa na wamiliki wa shule wanapaswa wakumbuke kuwa elimu ni haki ya mtoto, hivyo wanapaswa kujiepusha kutoza ada kubwa na ubaguzi wa elimu na huduma za elimu.
Aidha, Rais Kikwete alisema kupishana kwa mitaala ya kufundishia kunaelezwa katika sera kuhitaji mwongozo katika kila somo na kutumika kitabu kimoja cha kufundishia kwa shule zote ili kuondoa tofauti za utoaji wa elimu.
“Hatuwezi kuruhusu utaratibu wa kutumika kwa mitaala ya nchi nyingine, huwezi kuwa Tanzania halafu ukatumia mtaala wa Cambridge, wakati huo ni mfumo wa nchi nyingine.
“Hatuwezi kuwa na shule ambayo ina kitabu chake wanakuja wanafanya mtihani au wakiteuliwa kutunga mitihani wanafunzi wote wanafeli tunaanza kulaumu,” alisema Rais Kikwete.
Alisema mwongozo huo hautakataza matumizi ya vitabu vingine vya kujifunzia, isipokuwa kitabu kitachochaguliwa ndicho kitachotumika kutungia mitihani.
Alisema sera pia inatoa mwongozo wa kusimamia ubora wa elimu, kwakuwa hakuna nchi isiyokuwa na changamoto katika masuala hayo.
Matumizi ya kompyuta
Kuhusu matumizi ya kompyuta, Rais Kikwete alisema Serikali imeanza kufikiria kugawa kompyuta mpakato kwa kila mwanafunzi anayesoma elimu ya sekondari ili kukidhi mabadiliko ya sera ya elimu.
Alisema kompyuta hizo sasa zimeanza kutumiwa na walimu ili waweze kuwa na utaalamu wa kutosha katika ufundishaji.
“Mheshimiwa Kawambwa, naomba tufanye hili kabla sijaondoka, tuhakikishe wanafunzi wanatumia kompyuta shuleni,” alisema Rais Kikwete.
Ujenzi wa madarasa na maabara
Akizungumzia ujenzi wa madarasa na maabara, Rais Kikwete alisema serikali ilianza kujenga shule za kata kabla ya kuajiri walimu wa kutosha, lengo likiwa kuhakikisha yanakuwepo mazingira mazuri ya kusomea.
“Tulipoanza kujenga shule za kata watu waliziita yebo yebo, wakawa wanatucheka, lakini nikasema acha tuanze hata tukiwa hakuna walimu basi kufuli ziwepo.
“Nasema kama kuna mahali watoto wanasomea chini ya mti au kwenye mbavu za mbwa basi kuna matatizo ya kiuongozi.
“Nimegundua ukiwatisha watu mambo yanaenda, mara ya mwisho nilisema ujenzi wa maabara mwisho mwezi Juni, ukifikia muda huo kama kuna shule itakuwa haina maabara wahusika wanapaswa kuwajibika,” alisema Rais Kikwete.
Tatizo la walimu na changamoto za utoaji elimu
Rais Kikwete alisema hakuna nchi ambayo haina changamoto katika suala la elimu, isipokuwa changamoto hizo zinatofautiana.
“Asilimia 20 ya Bajeti ya Serikali ni elimu na mikopo imeongezeka vya kutosha, shule za msingi, sekondari na vyuo vimeongezeka ukilinganisha na awali, hivyo ni dhahiri kuwa tunapiga hatua pamoja na changamoto zilizopo,” alisema Rais Kikwete.
Alisema tatizo la walimu wa sanaa limemalizika na kwa sasa serikali ina mkakati wa kuondoa uhaba wa walimu wa sayansi katika shule za sekondari.
“Tumefikia hapo kwa jitihada hizi tunazoendelea kuzionyesha, watu wasione vyaelea, vimeundwa, sera tatu za elimu ya msingi, sekondari na ufundi ndizo zimetufikisha hapa, hakuna nchi ambayo imemaliza changamoto za elimu, nchi zote zina mijadala ya kuendeleza elimu,” alisema Rais Kikwete.
Uzinduzi wa sera hiyo ulienda sambamba na uzinduzi wa maabara tatu zilizopo katika Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai.
Kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Awali akimkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema sera hiyo italeta mabadiliko ya kiuchumi na kutatua changamoto za elimu kikanda, ambazo zitaongeza fursa ya rasilimali watu.
“Ili tufikie malengo kwa mwaka 2025, ni wakati muafaka baada ya sekta ya elimu kufuatilia utaratibu mpya ili kuleta mazingira mazuri kufikia malengo ya Matokea Makubwa Sasa (BRN),” alisema Dk. Kawambwa.
Kauli ya Rais wa CWT
Naye Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema sera ni matamko ambayo hutolewa, lakini yanakuwa na changamoto za kuyafanyia kazi.
“Bado sijaisoma lakini kwa uzoefu wangu, sera huwa ni matamko, yanaweza yakatekelezwa au yakaachwa, sera yoyote itatekelezwa kama vigezo vyote vimezingatiwa katika elimu, hivyo lazima kuwa na walimu bora, zana za kufundishia pamoja na malipo mazuri ya walimu. Kama hayo yatatokea basi itatekelezeka,” alisema Mukoba.
Sera hiyo imezinduliwa huku kukiwa na malalamiko mbalimbali ya udhaifu katika Sekta ya Elimu, ikiwa ni pamoja na hoja iliyowahi kutolewa bungeni na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, aliyedai kuwa Tanzania haina mitaala ya elimu na kwamba nchi haijawahi kuwa na mitaala ya elimu tangu ipate uhuru mwaka 1961.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles