26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mapigano ya wakulima, wafugaji yaua mtu mmoja, ng’ombe 71 Morogoro

FB_IMG_1450111743756NA RAMADHAN LIBENANGA, MOROGORO

MTU mmoja amefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa, akiwamo askari polisi mmoja baada ya kutokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Dihinda, Kata ya Kanga, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Dihinda, Hariri Kilama, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 11, saa 11 jioni.

Kwa mujibu wa Kilama, tukio hilo lilisababishwa na mfugaji mmoja aliyejulikana kwa jina la Shaban Ramadhan, kuingiza ng’ombe wake katika shamba la mkulima aliyetambuliwa kwa jina la Bakari Mlunguza ambao waliharibu mazao.

“Baada ya uharibifu wa mazao hayo, uongozi wa kijiji ulimwita Bwana Shamba wa Kijiji, Mathew Limbanywa, kwa ajili ya kufanya tathimini ya  mazao yaliyoharibiwa na mifugo hiyo.

“Baada ya tathmini hiyo, ilibainika, kuwa uharibifu uliofanyika ulikuwa mdogo na bwana shamba huyo aliomba suluhu ifanyike ili kutatua mgogoro huo.

“Pande hizo zilipokaa pamoja, mkulima aliomba alipwe fidia ya shilingi laki tatu, lakini mfugaji alikataa na kusema yupo tayari kulipa shilingi laki mbili.

“Makubaliano hayo yalipofanyika saa nane katika ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Wiliam Masanyika, mfugaji aliondoka na saa 11 jioni alirudi na kundi la wenzake na kuanza kupiga miruzi ya kuita ng’ombe wake waliokuwa chini ya ulinzi ofisini hapo.

“Wakulima walipoona kuna dalili za mapigano, nao walijibu mapigo, ambapo wafugaji walimpiga mkulima mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Mohamed ambaye alifariki dunia wakati akipelekwa katika Hospitali ya Mission ya Bwagala wilayani humo.

“Pamoja na mauaji hayo, ng’ombe 71 nao waliuawa na wengine 120 walijeruhiwa vibaya na wakulima hao,” alisema Kilama.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, Mwigulu Nchemba, aliliagiza Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kuimarisha ulinzi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuwakamata waliohusika katika vurugu hizo.

Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema polisi mkoani hapa wanawashikilia watu 19 wakiwamo watatu wanaodaiwa kuwaua ng’ombe hao kwa kuwakatakata kwa mapanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles