24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Mpinzani wa Lema atoa visingizio lukuki

dscf0844ELIYA MBONEA NA ABRAHAMU GWANDU, ARUSHA

ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philemon Mollel ‘Monaban’, ameibuka na madai mazito kwa Jeshi la Polisi kuwa walichangia kushindwa kwake na Godbless Lema wa Chadema.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jijini hapa juzi, wapigakura 105,800 walijitokeza kati ya 317,814  waliojiandikisha ambapo kura halali zilikuwa 104,353 huku 1,447 zikiharibika.

Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Iddi, alimtangaza Lema kuwa mshindi wa kiti cha ubunge kwa kupata kura 68,848 sawa na asilimia 65.9 akifuatiwa na Mollel 35,607 sawa na asilimia 34, Navoi Mollel (ACT-Wazalendo) 342, Zuberi Hamisi (CUF) 96 na Makame Jaria (NRA) 41.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kuahirishwa awali kutokana na kifo cha aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo, Estomih Mallah aliyefariki kabla ya Oktoba 25, mwaka huu.

Akizungumzia matokeo hayo, Mollel alisema hakuridhishwa na namna ulivyoendeshwa na kusimamiwa na vyombo vinavyohusika.

Mollel ambaye pia ni Kamanda wa Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha, alidai kuwapo kwa kasoro nyingi wakati wa kampeni na upigaji kura.

“Kulikuwa na gari Noah ya diwani wa Chadema ilipita baadhi ya vituo vya kupigia kura na kudai inawapelekea chakula mawakala. Lakini gari hiyo tumeambiwa ilikuwa na kura bandia zilizofanikiwa kuingizwa kwenye masanduku,” alisema Mollel.

Pia alilitupia lawama Jeshi la Polisi mkoani hapa, kwamba walizunguka na magari yenye maji ya kuwasha, huku mengine yakiwa na polisi mitaani jambo ambalo lilichangia wapigakura kujitokeza wachache, hususan wanawake na wazee.

“Wazee na akina mama waliogopa kwenda kupiga kura kutokana na magari ya polisi na askari wengi walioonekana mitaani. Hapakuwa na vurugu zozote, kwanini kuwatisha wananchi kwa silaha na vifaa vingine vya kivita?” alihoji Mollel.

 

MBOWE ANENA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye alikuwa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Njiro jijini wakati matakeo hayo yakitangazwa, alisema wakazi wa Arusha wameweza kuzungumza na kupaza sauti zao kupitia sanduku la kura.

“Ushindi wa Lema na kutangazwa kuwa mbunge mteule, umeonyesha kwa mara nyingine umuhimu wa kuheshimu sanduku la kura kama msingi wa amani na utulivu katika Jiji la Arusha,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Lema aliwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kupiga kura bila ubaguzi wa kabila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles