CHRISTINA GAULUHANGA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ilala imewakamata maofisa wawili wa Wizara ya Kilimo kwa tuhuma za Kuzuia mizigo inayoingia nchini kutolewa bandarini ili kushinikiza kujipatia fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 9, Kamanda wa Takukuru wilaya ya Ilala, Christopher Myava amesema, watuhumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo kwa muda mrefu jambo ambalo limekuwa ni kero.
Amewataja watuhumiwa hao ni Prisca Joseph na Flora Kuhabwa ambao ni wakaguzi wa mimea katika Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani katika Mahakama ya Ilala na kesi yao namba CC 607/2019 mbele ya Hakimu Flora Mujaya.
Myava amesema watuhumiwa wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma chini ya kifungu Cha 15 (1) Cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007.