Bunge la Watoto latoa neno kwa walipa kodi

0
545

Elisante John – Singida

BUNGE la watoto la wanafunzi wa shule za msingi 20 wa Wilaya ya Singida, limewataka Watanzania kuacha tabia ya kulalamikia kwa kuda kwamba kodi ni mzigo, badala yake waongeze kasi ya kulipa tozo hilo, ili waweze kupata uhalali wa kuhoji miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.

Hali ya jamii kushindwa kulipa kodi, imeelezwa na Bunge hilo kuwa inachangia kudhoofisha mipango mingi ya Serikali na kurudisha nyuma kasi ya kuwaletea wananchi maendeleo yaliyokusudiwa na viongozi wao.

Baadhi ya wanafunzi, Nasra Alli Shule ya Msingi Kinyeto na Editer Mtinda wa Shule ya Mtinko, walisema kodi ni tozo ya lazima ambalo kampuni, taasisi na raia yeyote ambaye ni mkazi na asiyekuwa mkazi, hulazimika kulipa kwa mujibu wa sheria, kutokana na nchi kutegemea kwa ajili ya mapato, ili kutekeleza majukumu yake.

Mratibu wa Shirika la Maendeleo na Elimu Mtinko (MEDO), Hassan Rasuli alisema jana pamoja na mambo mengine, bunge hilo limedhamiria kushirikiana na serikali ya wilaya katika kuboresha elimu, wilayani humo.

Alisema jamii inapaswa kupokea kwa dhati sera ya Serikali ya elimu bure kwa kudumisha ushirikiano na wadau wengine wa maendeleo, ili sekta hiyo iweze kuimarika, kutokana na mchango wa wananchi katika kulipa Kodi.

“Utafiti tuliofanya katika shule 20 za mradi huo zilizopo kwenye halmashauri ya wilaya ya Singida, zikiwemo shule za msingi na sekondari, tumebaini jamii bado ina mchango mkubwa katika kulipa kodi, kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya elimu,”alisema.

Mafunzo  ya siku tatu, yalishirikisha Wanafunzi wa shule za msingi wa halmashauri ya Wilaya ya Singida, yakiwa na lengo la kuwapatia elimu ya kodi, ili waweze kuwa raia wema siku za baadaye, katika kulipa kodi.

Asasi ya MEDO, chini ya shirika la Actionaid, imesimamia Bunge hilo  kwa ufadhili wa Shirika la Ushirikiano na Maendeleo la nchini Norway (NORAD), huku lengo likiwa ni kuwapa elimu ya Kodi wanafunzi na jamii kwa ujumla, ili siku za usoni wawe raia wema wa kulipa kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here