30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maofisa watatu wa Serikali kortini tuhuma za rushwa

Mutta Robert -Geita

TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Mkoa wa Geita, imewapandisha kizimbani aliyekuwa mratibu wa uchaguzi Mkoa wa Geita, Sania Mwangakala, Ofisa Ardhi Mteule, Vedastus Sulusi na Ofisa Ardhi Msaidizi, Revocatus Mafumbila wa Halmashauri ya mji wa Geita kwa tuhuma za  rushwa.

Sania pia ni Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Geita katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita na alikuwa mratibu wa mkoa huo wakati wa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Obadia Bwegoge katika shtaka namba 55 la mwaka 2020, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Kelvin Mrusuri akisaidiana na Augustino Mtaki alidai kati ya Oktoba 22, 2015 na Novemba 11, 2015, mtuhumiwa Sania alitenda makosa sita ya kughushi saini za watumishi mbalimbali wa umma na kufanikiwa kujipatia Sh milioni 11 kinyume na kifungu cha 333, 335 na 337 vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ya mwaka 2002.

Mrusuri alisema anashtakiwa kwa kutenda  makosa matano ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Mtuhumiwa wa pili, Sulusi ambaye ni Ofisa Ardhi Mteule Halmashauri ya Mji wa Geita,  akisomewa mashtaka yake na Mrusuri mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, alidai mtuhumiwa kati ya mwaka 2017 na 2018, alijipatia manufaa binafsi zaidi ya Sh milioni 10 malipo ya kiwanja kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 23.

Mshtakiwa wa tatu, Mafumbila ambaye ni Ofisa Ardhi Msaidizi Halmashauri ya Mji wa Geita katika shtaka namba 56 la mwaka 2020, anatuhumiwa kusaidia kosa kutendeka kinyume na kifungu cha 30 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Washtakiwa wote wako nje kwa dhamana, baada ya kukidhi vigezo na shauri hilo litatajwa tena Machi 3, mwaka huu.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Leonidas  Felix aliwaomba wananchi wa mkoa huo kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa miradi ya maendeleo vinavyofanyika maeneo na idara mbalimbali za Serikali, Serikali za mitaa na halmashauri ili watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles