25.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 20, 2024

Contact us: [email protected]

Maofisa wa Serikali wachomwa moto

moto-dodoma-1*Ni baada ya mchungaji wa kanisa kuita wananchi

 Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

WAKAZI wa Kijiji cha Iringa Mvumi katika  Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wamewaua watu watatu waliokuwa kwenye gari la Kituo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo cha Selian, Arusha.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi jioni  kijijini hapo, baada ya wananchi kuchoma moto gari hiyo ya Toyota Hilux   namba   STJ 9570, lililokuwa likitumiwa na maofisa hao kwa   shuguli za utafiti wa udongo.

Habari zinasema,  watu hao walikatwakatwa mapanga kabla ya kuuawa na kuchomwa moto wakazi wa kijiji hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, aliwaambia waandishi wa habari jana  kuwa waliouawa ni watafiti wawili na dereva wao na   waliuawa baada ya kuhisiwa kuwa ni wanyonya damu.

Alisema tukio hilo  lilitokea juzi  saa 12 jioni katika Kijiji cha Iringa Mvumi, Kata ya Iringa Mvumi, Tarafa ya Makang’wa wilayani Chamwino.

“Watu watatu  walikutwa wamefariki dunia huku miili yao ikiwa imeungua vibaya baada ya kukatwakatwa na mapanga na  kuchomwa moto na wakazi wa kijiji hicho.

“Waliouawa walikuwa kwenye gari   namba   STJ 9570   ya Toyota Hilux, mali ya Kituo cha Utafiti cha Udongo na Maendeleo cha Selian mkoani  Arusha.

“Katika gari hili  walikuwamo watafiti wawili na dereva wao na mmoja kati yao alikuwa ni mwanamke.

“Kwa bahati mbaya majina yao hatujayafahamu kwa kuwa waliungua vibaya,” alisema Kamanda Mambosasa.

Alisema chanzo cha mauaji hayo  ni mwanamke mmoja aliyepiga yowe kuwaita wananchi wenzake akiwaeleza jinsi alivyoona wanyonya damu.

“Chanzo cha tukio hili ni mwanamke mmoja aitwaye Cecilia Chimanga (34) aliyepiga yowe kijijini hapo kueleza ameona watu ambao anawahisi ni wanyonya damu.

“Taarifa hizi zilipofika kijijini, Mchungaji wa Dhehebu la Christian Family, Patrick Mgonela (46) ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, alitangaza kupitia kipaza sauti cha kanisa kuwa wamevamiwa na wanyonya damu.

“Kutokana na tangazo hili, wanakijiji walijitokeza kwa wingi na kuvamia gari hilo wakawaua waliokuwamo na kuwachoma moto pamoja na gari lao.

“Kwa sasa miili ya marehemu imehifadhiwa katika  Hospitali ya Mvumi Mission wilayani Chamwino.  Msako unaendelea kuwatafuta waliohusika na tukio hili,” alisema Kamanda Mambosasa.

Kamanda   alisema hadi kufikia jana jioni walikuwa wametiwa  mbaroni watu 30,   kati yao 21 ni wanaume na tisa  ni wanawake.

Alisema watu hao  wanasaidikiwa kuhusika na mauaji hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Jordan Rugimbana alitembelea eneo la tukio kujua undani wa tukio hilo.

Hadi tunakwenda mitamboni, Rugimbana na baadhi ya maofisa wa ulinzi na usalama wa mkoa huo, walikuwa eneo la tukio wakizungumza na wananchi.

Habari nyingine zilisema kutokana na hali hiyo, Rugimbana   alitangaza kuwasimamisha kazi  liyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Godfrey Manyale  ambaye pia ni ofisa kilimo wa wilaya kwa kudaiwa kukalia barua ya kuwatambulisha watafiti hao.

Alisema Mnyamale alipelekewa barua   kuhusu kazi ya watafiti hao lakini alikaa nayo ofisini bila kuishusha ngazi ya chini kwa hatua zaidi.

“Polisi wamekamata watu 30, msako mkali unaendelea maeneo yote,tunataka kuona watu waliohusika wanatiwa mbaroni ili wafikishwe mbele ya sheria…hakuna mtu aliyepewa mamlaka ya kukatisha uhai wa wenzake.

“Taifa limepoteza wataalamu ambao walikwenda Chamwino kufanya kazi ya utafiti wa udongo wakiwa na vibali vyote vinavyotakiwa.

“Hadi wanauawa walikuwa wamezunguka vijiji tisa baada ya kumaliza kazi kama hiyo katika Wilaya ya Mpwapwa kwa ajili ya kuchukua sampo za udongo,”alisema Rugimbana.

Alisema marehemu wote walikuwa na barua halali kutoka kwenye mamlaka zao kwenda vijiji husika hivyo inashangaza kuona wanavamiwa na wananchi na  kuuawa.

“Hawa maofisa wote walikuwa na barua zinazowaruhusu kufanya kazi ya utafiti, lakini walizungukwa na wananchi na kabla ya kuwaua waliwakatakata mapanga sehemu mbalimbali za miili yao.

“Tumeunda kamati ndogo ambayo inahusisha maofisa wetu wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kuchunguza ukweli wa tukio hili.

“Kama ikibainika mamlaka husika hazikufuata taratibu za kuwaruhusu hawa maofisa kwenda huko, tutajua namna ya kushughulika nao na kama kulikuwa na upungufu wa mawasiliano tutajua tu,”alisema Rugimbana.

Alisema tume hiyo  itafanya kazi kwa siku chache kabla ya  kukabidhi ripoti yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles