24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Manufaa ya Diaspora si ya kupuuziwa

Rais Dk. John Magufuli akizungumza na waandishi wa habari
Rais Dk. John Magufuli akizungumza na waandishi wa habari

NA TENGO KILUMANGA,

Nimeamka kwa kishindo, kichwa kinanigonga kama ngoma za Mzee Mwinamila, ila tu ngoma zake zilikuwa nzuri sana. Sijui ngoma zake bado zipo kwenye taarifa za habari. Kisa cha mie kichwa kunigonga ni kwamba usku mzima sie Diaspora (Wanaughaibuni) tunajadili maswali ambayo yaliulizwa kwenye mkutano wa Rais John Pombe Magufuli na wanahabari wa Tanzania.

Swali kubwa ambalo lilitugusa sana ni lile lililoulizwa na Sarah Mossi Shamte Mhariri wa gazeti la Mtanzania jarida la siasa. “Kwamba Serikali ina mtazamo na mipango gani na Watanzania waishio nje ya nchi hususani katika masuala ya uwekezaji nchini, umiliki wa ardhi na mali zingine zisizohamishika? Ni swali ambalo ni la msingi sana na ambalo Diaspora wengi walisikiliza kwa makini sana dunia nzima. Kwa bahti mbaya Swali halikujibiwa kikamilifu na ni swali ambalo linahitaji uchambuzi mrefu na linaingiliana na katiba ya nchi.

Sisi tunashukuru sana mwaka huu mmoja wa Rais umekwenda sana ingawa bado kuna changamoto nyingi ambazo bado zipo katika jamii. Na hii Rais alikiri kwa moyo mweupe. Changamoto zipo na zinafanyiwa kazi.

Hata hivyo swali aliloulizwa na Mhariri Sarah Mossi lilileta mwangaza na kutuonyesha kwamba safari yetu bado ni mbali na mvutano bado upo.

Changamoto ni nyingi Tanzania wakati tunaelekea kwenye kujenga nchi kuwa ya viwanda na ninaamini tutafanikiwa kama Tanzania itaamka na kuona manufaa ya Wanadiaspora. Katika kujenga uwezo wetu kama nchi na kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi ya kushiriki katika kubadilisha Tanzania kuwa ya viwanda basi kwa maoni yangu ni muhimu pia kuwashirikisha Watanzania ambao wanaishi nje waweze kurudi na kusaidia.

Urasimu upungue, mikakati na miundombinu ya kurahisisha Wanadiaspora kuweza kuwekeza kama Mtanzania yeyote iwepo na utaratibu wa kuhakikisha kwamba hata watoto wetu wanakuwa katika hiyo mikakati. Watoto na vizazi ambavyo vimezaliwa nje ya Tanzania na Watanzania wanoishi nje visisahaulike katika utaratibu huo, kwani wengi wamesoma sana na wamekalia na ujuzi mwingi wa kuweza kuchangia katika maendeleo ya kutuwezesha kuwa Tanzania ya viwanda na kuwa nchi yenye kipato cha kati kufikia mwaka 2025.

Changamoto hazipo ndani ya nchi tu, katika mahitaji makubwa wakati tunajenga Tanzania ya viwanda isisahulike mipaka yetu na kuboresha usalama na hasa usalama baharini na maji ambayo yanapakana na Tanzania.

Mamlaka ya bahari ni moja ya nguzo kubwa ambayo uboreshaji wake utaweza kusaidia kulinda maliasili ya Watanzania baharini na kuangalia au kuzuia uharibifu kwenye bahari kuu ambayo inapakana na maji ya Tanzania.

Mchango wa Wanadiaspora na vizazi vyao vitaweza kuleta tija kubwa katika sehemu nyingi kwenye shughuli za maendeleo Tanzania. Ni kukubali kwamba wengi wao baada ya miaka mingi nje ni watu ambao wanaajirika na ujuzi wao utakuwa na ”umwagikaji wa ujuzi” kwa wengi na kuelimisha Watanzania katika maadili ya kazi na nidhamu. Fikra na mtazamo wa Watanzania wengi utabadilika.

Nina imani kilio cha Diaspora kinasikika kwa wananchi na kada za wabunge, hawa ndio wataamua kunyolewa kwa chupa au wembe. Naamini pia wanaelewa umuhimu wa kuweka mazingira mazuri kwa kusaidia kurahisisha Watanzania wanaoishi nje kuchangia katika maendeleo ya nchi.

Sina budi kusema, kama unataka kujua rangi nyeusi ni rangi gani basi ni sharti ufahamu rangi nyeupe ni rangi gani. Hautaweza kuieleza rangi nyeusi kama hufahamu rangi nyeupe.

Wanadiaspora wanafahamu tofauti ya rangi hizo na wanafahamu tofauti ya mzingira waliyotoka, waliokwenda na watakayorudia. Kufahamu hizo tofauti ni kuweza kutafuta mbinu za kubadilisha na kuboresha mazingira yetu na kuweza kuchangia katika kubadilisha maisha ya Watanzania.

Tunafahamu sana mahitaji ya wengi ambayo yanatugusa wote na mwito kwa Mheshimiwa Rais kwamba hii ni Tanzania ya wote na ni sisi Watanzania tutaijenga nchi yetu ulinigusa kama ulivyowagusa Diaspora.

Kitu ambacho mie kinanisikitisha sana ni kwamba ile kazi wanayofanya Diaspora mara nyingi inapita bila ya kutambulika au watu kufahamu imepita mikononi mwetu na kama watu wanaiona basi ni wachache sana.

Diaspora hawaji wenyewe tu, sisi tumeweza kuwashawishi hata wenyeji wawekeze Tanzania. Mie nina watu kadhaa ninaowafahamu ambao wamefanya hivyo na sasa wanafanya vizuri sana. Kila moja wetu Ughaibuni ni balozi waTanzania, kila tunayekutana naye ambae si Mtanzania tunatumia nafasi hii kuwaunganisha na Tanzania. Huwezi kuacha kwa sababu ni nchi ambayo imetulea na kutupa uzima.

Mfano mzuri ni kwa jinsi tunavyojipanga duniani na kuonyesha umoja. Kama tungekuwa ni watu  wasioipenda Tanzania na ndugu zetu kwanini tuhangaike na kugombania tupate nafasi ya kuchangia na kurahisishiwa urasimu ambao unatupotezea muda na gharama kubwa?

Jamia ya Diaspra wa Tanzania duniani ni rasilimali kubwa sana. Kuipoteza au kutokuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kusaidia na kuchangia kwenye mapato ya Taifa ni kutokufahamu umuhimu wao. Kama ni chombo ambacho kitatumika kutafuta ushauri au taaluma tofauti katika masuala na matakwa mbali mbali kwa ajili ya nchi.

Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga.. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles