MAREGESI PAUL Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
HALMASHAURI Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imemrudisha tena Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula, kuwania nafasi hiyo.
NEC pia imewateua na kuwapitisha wagombea wawili wa kugombea nafasi za juu katika chama hicho.
Mangula aliteuliwa Novemba 2012, kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa.
Kurudishwa kwa jina la Mangula, kunaondoa minong’ono ya mwanasiasa huyo kupumzika siasa baada ya kuitumikia CCM katika nafasi mbalimbali, ikiwamo ya Katibu Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema katika kikao kilichofanyika jana, NEC iliwateua Rais Dk. John Magufuli kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohammed Shein, kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Mangula, kutetea nafasi yake hiyo.
“Majina yaliyopitishwa ni ya Dk. John Magufuli kugombea nafasi ya Mwenyekiti, Dk. Ally Mohamed Shein, kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) na Philip Mangula, kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti CCM kwa upande wa Tanzania Bara.
“NEC imefanya uteuzi wa kuwapitisha wana CCM hao ambao wataomba ridhaa ya Mkutano Mkuu wa Taifa utakaofanyika kuanzia kesho (leo) na keshokutwa (kesho),” alisema Polepole.
Kwa upande wa nafasi za wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Polepole alisema waliochukua fomu ni wanachama 51 kwa upande wa Tanzania Bara.
“Hapa tuna nafasi 30 ambapo kwa Tanzania Bara, wanatakiwa wawe 15 na Zanzibar wanatakiwa wawe 15 ingawa hadi sasa tumepata majina 51 ya wagombea kwa upande wa Tanzania Bara,” alisema.
Kuhusu Mkutano Mkuu huo, Polepole alisema NEC pamoja na mambo mengine, imepitisha ajenda ili uweze kufanyika kwa mafanikio.
KUPANDA, KUSHUKA KWA MANGULA
Mangula aliondoka katika uongozi mwaka 2006, baada ya kuchaguliwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, kuwa mwenyekiti wa chama hicho akipokea kijiti kutoka kwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Baada ya kuchaguliwa Kikwete, alipanga upya safu ya viongozi ndani ya chama hicho huku Mangula akiachwa nje na kugeukia kilimo cha viazi nyumbani kwake wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.
Mangula, ambaye alishika nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM kwa kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, hadi anateuliwa tena kushika nafasi ya umakamu mwenyekiti mwaka 2012, alikuwa mshauri wa mambo ya siasa wa chama tawala cha Afrika ya Kusini – ANC.
Nafasi hiyo alianza kuitumikia tangu mwaka 2008 na amekuwa akisifika kuwa ni mtu mwenye mbinu nyingi za kisiasa, hasa kwenye masuala ya uchaguzi na mikakati ya kueneza siasa.
Hata hivyo katika uchaguzi wa ndani ya CCM alitupa kete yake kuwania uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa kabla ya kugawanywa na kuwa mikoa miwili ya Iringa na Njombe mwaka 2012, lakini alijikuta akishindwa kufua dafu dhidi ya Deo Sanga.
- SALIM ATOA NENO
Katika hatua nyingine, Polepole alisema awali katika kikao cha Kamati Kuu kilichokaa jana, Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, alitoa neno la shukrani kwa utumishi wake wa miaka mitano kuanzia mwaka 2012 hadi 2017.
Pamoja na hayo, Dk. Salim alionyesha kuridhishwa na uongozi wa Rais Magufuli kutokana na jinsi anavyotanguliza masilahi ya Watanzania, hasa wanyonge.
“Rais Magufuli amekuwa kielelezo tosha na kwa vitendo anaishi maisha yanayomuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere.
“Nitazidi kuhakikisha CCM inaimarika kwa manufaa ya amani na umoja wetu ndani ya chama chetu na taifa letu la Tanzania,” alisema Dk. Salim…….
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya MTANZANIA