LONDON, ENGLAND
LIGI Kuu nchini England iliendelea jana kwenye viwanja mbalimbali, huku mchezo ambao ulipigwa mapema ukiwa kati ya Middlesbrough, ambayo ilikubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Manchester United.
Mchezo huo, ambao ulipigwa Uwanja wa Riverside, wenyeji walijikuta wakiwa katika wakati mgumu wa kuzuia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wapinzani wao.
Manchester United waliutawala mchezo katika dakika 45 za kipindi cha kwanza na waliweza kupata bao katika dakika ya 30, lililowekwa wavuni na Marouane Fellaini, baada ya krosi safi iliyopigwa na Ashley Young.
Wenyeji waliingia uwanjani wakitumia mfumo wa 4-3-3, wakati huo wapinzani wao, Manchester United wakitumia 3-4-3 ambapo walionekana kujaza viungo.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika United walikuwa wanaongoza bao moja, baada ya kipindi cha pili kuanza bado United walionekana kuutawala mchezo na kutafuta bao la pili.
Bao la pili lilipatikana dakika ya 62, ambalo liliwekwa wavuni na kiungo wao, Jesse Lingard, baada ya kupewa pasi ya mwisho kutoka kwa Juan Mata.
Baada ya Mata kutoa pasi ya mwisho katika bao la pili, kocha wa klabu hiyo, Jose Mourinho, alifanya mabadiliko ambapo alimtoa kiungo huyo na kumpa nafasi Marcos Rojo amalizie dakika 20, lakini kutoka kwake kulionekana kupunguza kasi ya Manchester United na kuwapa nafasi wapinzani wao kucheza eneo la katikati.
Zikiwa zimebakia dakika 13, Middlesbrough walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililowekwa wavuni na nyota wao, Rudy Gestede.
Mourinho aliendelea kufanya mabadiliko ambapo mfungaji wa bao la pili ambaye anacheza nafasi ya kiungo, Lingard alipumzishwa na nafasi yake ikachukuliwa na Anthony Martial kwa ajili ya kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji, mchezaji huyo aliingia katika dakika ya 80.
Zikiwa zimebakia sekunde chache mchezo huo kumalizika, United waliongeza bao la tatu ambalo lilifungwa na Antonio Valencia na mara baada ya mchezo huo kuanza, hatimaye mwamuzi Jonathan Moss alimaliza mchezo.