32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAMILIONI YA WATU HATARINI KUFA NJAA

Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN), Stephen O’Brien

NEW YORK, MAREKANI

UKAME, uhaba wa chakula na mvua za kutosha vimesababisha idadi kubwa ya watu kuwa katika hatari ya kufa kwa njaa iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa.

Nchi mbalimbali zimekumbana na sintofahamu na kuwa moja ya janga kubwa linaloikabili dunia kwa sasa kuliko kipindi chochote cha miaka ya nyuma.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN), Stephen O’Brien, anayehusika na misaada ya kibinadamu, amesema ulimwengu unakabiliwa na tatizo kubwa zaidi la kibinadamu tangu Umoja wa Mataifa kuundwa mwaka 1945 ikiwa ni miaka 72 iliyopita.

Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, O'Brien amesema bila ya juhudi za pamoja na uratibu wa Jumuiya ya Kimataifa kushughulikia baa la njaa, watu watakufa na wengine wengi watataabika kutokana na magonjwa.

Umoja wa Mataifa unatoa wito wa kutolewa kwa michango ya fedha ili kuwepo kwa misaada ya dharura kuwasaidia raia wa Yemen, Sudan Kusini, Somalia na Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na pia kuwepo njia salama kufikisha misaada katika maeneo ya mizozo ili kuepusha janga.

O'Brien amesema zinahitajika dola bilioni 4.4 ifikapo Julai mwaka huu na kuongeza bila ya ufadhili huo, watoto watadumaa kutokana na utapiamlo hivyo hawataweza kwenda shuleni, kutakuwa na athari katika maendeleo ya kiuchumi na riziki, matumaini na vizazi vijavyo vitapotea.

Umoja wa mataifa na mashirika ya chakula yanaeleza baa la njaa kuwa pale asilimia 30 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanapokabiliwa na utapiamlo mbaya na idadi ya watoto wanaokufa ikiwa wawili au zaidi kati ya watu 10,000 kwa siku.

Nchini Yemen ambako kuna mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu, theluthi mbili ya idadi ya Wayemen milioni 18.8 wanahitaji misaada na zaidi ya watu milioni saba wakikumbwa na njaa na hawajui pale mlo mwingine utakapotoka.

Idadi hiyo ni milioni tatu zaidi ya waathiriwa walioripotiwa mwezi Januari. Taifa hilo masikini zaidi la Kiarabu linakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambako watu 48,000 wameyatoroka mapigano katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Kwa mwaka huu, Umoja wa Mataifa unahitaji dola bilioni 2.1 kuwasaidia Wayemen milioni 12 kwa kuwapa misaada ya dharura. Ni asilimia 6 tu ya idadi hiyo ambayo mpaka sasa imepokea misaada.

Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres, anatarajiwa kufanya mkutano wa wafadhili kwa ajili ya Yemen ifikapo Aprili 25, mwaka huu mjini Geneva nchini Uswisi.

Guterres pia aliizuru Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani linalokumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mitatu iliyopita ambako pia kuna janga kubwa la njaa. Zaidi ya watu milioni 7.4 nchini humo wanahitaji misaada.

Zaidi ya watoto milioni moja wanakadiriwa kukumbwa na utapia mlo mkubwa wakiwemo watoto 270,000 ambao wako katika hatari ya kufa njaa iwapo misaada haitawafikia kwa wakati.

Wakati huo huo mlipuko wa kipindupindu katika maeneo kadhaa nchini humo yanaifanya hali kuwa mbaya zaidi. Mlipuko huo ulianza mwezi Juni mwaka jana na umesambaa hivi sasa katika maeneo mengi.

Somalia nako zaidi ya nusu ya idadi ya raia milioni 6.2 wanahitaji misaada ya kibinadamu wakiwemo watu milionii 2.9 ambao wanakumbwa na baa la njaa na hivyo wanahitaji misaada ya haraka ili kuyaokoa maisha yao.

Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, uasi wa miaka saba wa kundi la waasi la Boko Haram umesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na kupelekea wengine milioni 2.6 kuhama makazi yao.

Umoja wa Mataifa unasema utapiamlo ni mbaya sana katika eneo hilo kiasi cha kwamba watu wazima wamedhoofika sana na kushindwa kutembea na baadhi ya jamii zimepoteza watoto wao wote.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada ya kibinadamu, ameonya pia watu milioni 2.7 nchini Kenya ambako kuna ukame mbaya hawana chakula cha kutosha na huenda idadi hiyo ikaongezeka hadi watu milioni 4 ifikapo mwezi ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles