Na PATRICIA KIMELEMETA – bagamoyo
MAMIA ya wananchi wa Kijiji cha Kerege, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, wamejitokeza kupata tiba za magonjwa mbalimbali katika kambi maalumu iliyoendeshwa na zaidi ya madaktari 30 na madaktari wanafunzi 60.
Baadhi ya matibabu waliyotibiwa katika kambi hiyo ni magonjwa ya meno, macho, malaria, kisukari, ngozi na magonjwa mengine.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa matibabu hayo, Mtaalamu wa Madawa na Tiba, Dk. Sajjad Fezal, alisema kambi hiyo imeshirikisha madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mwananyamala, Mnazi Mmoja, Sanitas na wanafunzi kutoka Hospitali ya Dk. Kairuki.
“Katika kambi hiyo, zaidi ya wanaume saba waliopimwa wameonekana wana maambukizi katika kibofu cha mkojo na tumewaandikia rufaa ya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa uchunguzi zaidi ili waweze kuangaliwa kama wana matatizo ya tezi dume au la.
“Lengo la kupiga kambi katika eneo hilo ni kutoa huduma za matibabu bure kwa wananchi wa kijiji hiki pamoja na vijiji jirani, jambo ambalo limesaidia kujitokeza kwa wagonjwa zaidi ya 1,500, ” alisema Dk. Sajjad.
Alisema idadi kubwa ya wananchi ambao wanaona wana matatizo makubwa, yakiwamo kisukari na tezi dume, wanashindwa kwenda hospitali kwa sababu ya ukosefu wa fedha.
“Hivyo basi kambi kama hizi zinawasaidia wananchi hao kupata vipimo bure na kujua afya zao, pamoja na mambo mengine, mkakati wetu ni kuhakikisha tunazunguka nchi nzima kupiga kambi ya matibabu jambo ambalo linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Klabu ya Rotary Oysterbay, Alfred Woiso, alisema kambi hiyo ni ya siku moja ambayo imeandaliwa na wadau mbalimbali wakiwamo Benki ya DTB.
Alisema lengo ni kushirikiana na Serikali ili kutoa huduma za matibabu kwa wananchi wa kipato cha chini.