27.7 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mambosasa: Suala la Mo mikononi mwa DCI

ANDREW MSECHU – DAR ES SALAAM

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa,  amesema hana jambo la kuzungumza kuhusu kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’ kwasababu tayari alishakamilisha jukumu lake na kulikabidhi kwa viongozi wa juu wa jeshi hilo. 

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mambosasa alisema kwa sasa wanaojua kinachoendelea ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kwani ndiye mwenye jadala hilo na ndiye anatakiwa kutoa uamuzi kutokana na taarifa za uchunguzi zilizowasilishwa kwake kutoka ofisi ya upelelezi Kanda Maalumu ambayo iko chini yake.

“Kuhusu maelekezo ya Rais aliyoyatoa jana (juzi) Ikulu kuhusu kutekwa kwa Mo, maadamu aliyatoa mbele ya Mkuu wetu wa Jeshi la Polisi (IGP Simmon Sirro) na DCI (Robert Boaz) ambao walikuwepo, jalada hilo lilishafika kwao huko ndiko wanakojua kinachoendelea. 

“Mimi jukumu langu lilishakwisha kwa hiyo ni suala la maamuzi ya juu kuhusu hatua zilizofikiwa kwenye jalada hilo.

“Kwangu mimi kwa sasa ndicho ninachoweza kuzungumza, zaidi ya hapo mtafute Msemaji wa Jeshi la Polisi anaweza kukusaidia zaidi kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo, kwa hatua ambayo limeshafikia kwa sasa. Mimi ninaendelea na majukumu yangu mengine,” alisema Kamanda Mambosasa.

Alipoulizwa, Msemaji wa Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ahmed Msangi,  alisema kwa taarifa aliyo nayo ni kwamba jalada hilo limeshafika kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), ambaye ndiye anayetakiwa kuandaa mashtaka.

“Jalada hilo la uchunguzi lilishapelekwa kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, (DPP) ambaye ofisi yake ndiyo inayoandaa mashtaka yote na kuyapeleka mahakamani,” alisema.

Alipoulizwa kuwa jalada hilo lilifika lini kwa DPP, alisema hana taarifa rasmi lakini lilifika muda kidogo.

Kauli ya Rais 

Juzi baada ya Rais Magufuli, kuwaapisha Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na makamishna wapya wa Jeshi la Polisi, alisema tukio la kutekwa kwa Mo limeacha maswali mengi.

“Watanzania si wajinga wanafahamu na wanajua ku– analyze mambo, alipotekwa Mohammed tulipata story nyingi lakini lilipokuja kumalizika lile suala limeacha maswali mengi zaidi.

“Aliyetekwa alikutwa Gymkhana, alikwendaje pale, lakini bunduki ziliachwa pale, wakajaribu kuchoma gari…lakini baadaye tunamwona aliyetekwa anakunywa chai na Mambosasa maelezo hayapo.

“Lakini baada ya siku chache tunaelezwa nyumba alikokuwa ametekwa na aliyebeba watekaji huyu hapa lakini baadaye kimya mpaka leo na miezi imepita. 

“Tukio hili limeacha maswali mengi bila majibu, nikajiuliza labda ndiyo mambo ya kisasa kama lilivyo jina la Kamanda Mambosasa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Watanzania wanataka kuona hatua zinachukuliwa lakini dosari ndogondogo zinalichafua Jeshi la Polisi.

“Watanzania wanataka kuona angalau huyo mmiliki wa nyumba akajibu, haya hata kama Watanzania wakinyamaza lakini mioyo yao haitakaa kimya. 

“Walitegemea huyo aliyeonyesha nyumba alimokuwa akiishi anapelekwa mahakamani kesho lakini hakuna, mkilianzisha suala lazima limalizike,” alisema.

Alisema makamishna wapya na makamanda wengine wa Jeshi la Polisi lazima wajenge taswira nzuri ya jeshi hilo na akataka wachache wanaolichafua washughulikiwe.

“Usiogope IGP kubadili kamishna au kupunguza nyota zao wala usisite, ambao wanashindwa ku – perform wasiwe kila siku wanapelekwa makao makuu, waende wakawe chini ya ma – RPC wengine,” alisema.

Mo alivyotekwa

Mo alitekwa Oktoba 11, mwaka jana saa 11:00 alfajiri akiwa Hoteli ya Collesum iliyopo Barabara ya Haile Selassie, Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi ya viungo. Mfanyabiashara huyo alipatikana Oktoba 20 mwaka jana eneo la Gymkhana, katikati ya jiji.

Kulingana na taarifa za awali zilizotolewa na polisi, watekaji hawakuwa Watanzania, wawili kati yao walikuwa wanongea Kingereza chenye lafudhi sawia na za nchi za Kusini mwa Afrika na mmoja alikuwa akiongea Kiswahili kibovu.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Naibu wake, Hamad Masauni, kwa nyakati tofauti walikaririwa wakisema vyombo vya ndani vya ulinzi vina uwezo wa kutosha kufanya uchunguzi wa tukio hilo. 

Jumla ya watu 26 walikamatwa kutokana na tukio hilo na baadaye 19 waliachiwa kwa dhamana.

Baada ya kukaa kimya kwa siku nne, familia ya Mo ilijitokeza na kutangaza kuwa watatoa zawadi ya Sh bilioni moja kwa yeyote atakayewapatia taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa Mo.

Mo anakisiwa kuwa na utajiri wa Dola 1.5 bilioni kwa mujibu wa jarida la masuala ya fedha la Forbes na kumfanya kuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki na bilionea mwenye umri mdogo zaidi Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles