NORA DAMIAN -DODOMA
TUMETEKELEZA kwa Kishindo Tunasonga Mbele kwa Pamoja, ndiyo kaulimbiu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.
Chama hicho tayari kimezindua kampeni zake na kuanza kuinadi Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 kikiomba ridhaa ya Watanzania ili kiweze kuwaongoza tena katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Wagombea wa chama hicho wakiongozwa na mgombea urais, Dk. John Magufuli wanaendelea kuinadi ilani hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchi ili wananchi wapate fursa ya kujua yale ambayo CCM imepanga kuyatekeleza katika miaka mitano ijayo sambamba na yale yaliyotekelezwa kwa kipindi cha 2015 – 2020.
Katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, chama hicho kimeainisha vipaumbele sita vitakavyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Makala haya yanaangazia vipaumbele hivyo na mambo muhimu yatakayozingatiwa katika kuvitekeleza.
VIPAUMBELE
Vipaumbele vitakavyotekelezwa katika miaka mitano ijayo ni pamoja na kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa, kukuza uchumi wa kisasa, fungamishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.
Vipaumbele vingine ni kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi, kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini.
Vingine ni kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi na kutengeneza ajira milioni 8.
“Tutaimarisha jitihada za kukuza uchumi kwa kuboresha sera za uchumi na sera za fedha na kupunguza viwango vya riba, tutahakikisha uchumi unakua kwa wastani wa asilimia nane kwa mwaka,” anasema Dk. Magufuli.
KILIMO, UVUVI, UFUGAJI
Dk. Magufuli anasema eneo la umwagiliaji litaongezwa kutoka hekta 511,383 hadi kufikia milioni 1.2 sambamba na kuimarisha huduma za ugani na vyama vya ushirika.
Anasema pia maeneo ya ufugaji yataongezwa kutoka hekta milioni 2.7 hadi kufikia hekta milioni 6 na kwamba wataongeza vituo vya kuzalisha mbegu bora ili kuwa na tija ya mifugo nchini.
Kwa upande wa uvuvi anasema itajengwa bandari ya uvuvi katika ukanda wa Pwani, kuongeza uzalishaji wa vifaranga na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki.
“Kwenye madini tutaimarisha udhibiti na usimamizi wa uchimbaji madini ili uweze kunufaisha taifa, tutawezesha wachimbaji wadogo wafanye shughuli zao kwa tija. Tutaimarisha masoko kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji madini,” anasema Dk. Magufuli.
UTALII, SANAA, MICHEZO
Anasema mapato yatokanayo ya utalii yataongezeka kutoka Dola bilioni 2.6 hadi Dola bilioni 6 huku idadi ya watalii ikitarajiwa kuongezeka na kufikia milioni 5.
Dk. Magufuli ameahidi kujenga uwanja mkubwa katika Jiji la Dodoma ili kuwawezesha wananchi wote kushuhudia matukio yatakayokuwa yakifanyika badala ya wengine kukaa na kuangalia kwenye luninga.
“Sekta hii inakua kwa kasi na imeajiri vijana wengi, tutaimarisha usimamizi wa hati miliki ili wasanii wanufaike na kazi zao. Sekta ya sanaa na michezo tutaibeba kwa nguvu kubwa zaidi,” anasema Dk. Magufuli.
USAFIRI, MAWASILIANO
Anasema watanunua meli ya kubeba mizigo katika Bahari ya Hindi, kujenga meli tatu na kununua meli ya kubeba mabehewa ya treni.
Katika usafiri wa anga anasema wanatarajia kununua ndege mpya tano na kati ya hizo mbili zitakuwa za masafa marefu, mbili za masafa ya kati na moja ya mizigo.
Pia anasema wataimarisha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kiwe na uwezo wa kutoa wataalam mbalimbali wa anga.
Katika sekta ya mawasiliano anasema wataongeza matumizi ya intaneti kutoka asilimia 43 hadi kufikia asilimia 80.
Kwa upande wa barabara mipango ki kuendelea kuunganisha barabara katika mikoa ambayo bado haijaunganishwa ikiwemo ujenzi wa kilomita 359 kutoka Mpanda – Tabora.
Barabara nyingine ni ile ya Manyoni – Tabora – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi na ile ya Lupilo – Malinyi – Kilosa pamoja na madaraja makubwa 7 yakiwemo ya Busisi na Salenda.
AFYA, MAJI
Dk. Magufuli anasema watumishi mbalimbali wa kada ya afya wataongezwa kufikia 25,000 pamoja na kukamilisha ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na rufaa.
Katika sekta ya maji, Dk. Magufuli anasema watahakikisha asilimia 90 ya Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.
“Ninajua wako baadhi ya watu wanaweza wasiamini kwamba tunaweza kuyatekeleza, naomba Watanzania watuamini uwezo wa kuyatekeleza tunao kama ambavyo tumeweza kuyatekeleza yale mengine kwa kipindi cha miaka mitano.
“Uchaguzi huu utaamua ama tuendelee na mageuzi tuliyoyaanzisha ama tusiendelee nayo, uchaguzi huu utaamua tupate viongozi watakaokuwa nasi wakati wa shida ama watatukimbia…uamuzi ni wenu.
“Tunajua tumejenga msingi mkubwa, tumeanzisha miradi mingi sina uhakika kama mkichagua zaidi ya CCM kuna watakaokuja kuiendeleza, tuangalie mahali tulipotoka, tulipo na tunapoelekea.
“Nawaomba sana kura zenu mkipigie Chama Cha Mapinduzi ili haya niliyoyaeleza tuweze kuyatekeleza kwa kasi,” anasema Dk. Magufuli.
AJIRA MILIONI NANE
Mambo yatakayozingatiwa katika
kutekeleza kipaumbele hicho ni kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inaajiri vijana wengi zaidi wa Kitanzania.
Aidha kuchochea ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi pamoja na utalii.
Mambo mengine yatakayozingatiwa ni kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali ikiwemo kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na asasi za utoaji mikopo yenye riba na masharti nafuu.
Pia kuwahamasisha na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika utamaduni, michezo na sanaa kwa ajili ya afya bora na burudani na kuongeza fursa za ajira na kipato.
Mikakati mingine ni kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini ili shughuli za uchumi na biashara ziongezeke na kuzalisha ajira.
Kuhamasisha na kusimamia halmashauri zote nchini kuendelea kutenga, kurasimisha na kupima na kuweka miundombinu kwenye maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujishughulisha na uzalishaji mali na biashara.
Aidha utawekwa mkakati wa makusudi wa kuwawezesha vijana wabunifu na makundi mbalimbali ya vijana na wanawake kuanzisha shughuli za uzalishaji mali na ujasiriamali ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine.
Pia kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kati ili kuhakikisha vijana wanaohitimu wanapata maarifa na ujuzi wa kazi utakaowawezesha kujiajiri na kuajirika.
Hatua nyingine ni kuimarisha mifumo na kuongeza kasi ya kurasimisha ujuzi ili nguvu kazi ya taifa itumike ipasavyo katika soko la ajira la ndani na nje.
Pia kuimarisha mifumo ya taarifa za soko la ajira na mitaji ili kuwezesha vijana kutumia fursa hizo, kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi mbalimbali za kazi kwa nguvu kazi ya taifa katika sekta za kipaumbele.
Mkakati mwingine ni kuwawezesha vijana wanaohitimu elimu ya juu na vyuo vya ufundi kuunda makampuni kwa lengo la kuwapatia mitaji na nyenzo kupitia taasisi za fedha na mifuko mingine ya uwezeshaji.
YALIYOTEKELEZWA 2015-2020
Dk. Magufuli anasema mwaka 2015 Watanzania walitaka kuona mabadiliko ya kero mbalimbali yanashughulikiwa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kukata kiu hiyo.
Anasema wamejitahidi kuimarisha nidhamu katika utumishi wa umma, kupambana na rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za umma.
“Mwaka 2015 Watanzania walitaka kuona mabadiliko, wakienda ofisi za umma wanahudumiwa vizuri, huduma za jamii, elimu, afya, umeme, maji, umeme zinaboreshwa.
“Mabadiliko ya kuona kero zao mbalimbali zinashughulikiwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kukata kiu hiyo ya kuleta mabadiliko nchini.
“Tumefanya yaliyo mazuri kwa wananchi wetu ndiyo maana tunaomba tena miaka mitano tuendelee kufanya mazuri… tupeni tena miaka mitano tukafanye makubwa zaidi,” anasema Dk. Magufuli.
Anasema mashauri ya rushwa 2,256 yamefunguliwa na kwamba Serikali imeshinda 1,013 kati ya 1,929 yaliyoamriwa.
Anasema pia kutokana na kutungwa kwa sheria ya kulinda rasilimali za taifa mwaka jana sekta ya madini iliongoza kwa kukua kwa asilimia 17.7 huku mapato yakiongezeka kutoka Sh bilioni 168 (2014/15) na kufikia Sh bilioni 528 (2019/20).
Anayataja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa kodi kutoka Sh bilioni 850 hadi kufikia Sh trilioni 1.5.
Dk. Magufuli anasema uchumi umeendelea kukua kutoka asilimia 6.9 hadi 7 huku Pato Ghafi la Taifa likiongezeka kutoka Sh trilioni 94.349 (2015) hadi kufikia Sh trilioni 139.9 (2019).
“Kutoka kundi la nchi maskini na kuingia kundi la uchumi wa kati huu ni ushahidi tosha kuwa tunastahili kupewa miaka mingine mitano, tupeni tuendelee kuongoza,” anasema Dk. Magufuli.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli mafanikio mengine ni kupungua kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 6.1 hadi asilimia 4.1 huku fedha za kununua bidhaa na huduma kwa miezi sita zikiongezeka kutoka Dola bilioni 4.4 hadi Dola bilioni 5.168.
Anasema pia thamani ya biashara ya nje imeongezeka kutoka Sh trilioni 14.5 hadi Sh trilioni 16.6 wakati viwanda vimeongezeka kutoka 52,633 hadi 61,110.
Mafanikio mengine ni kuzalishwa ajira zaidi ya milioni 6 na kufanikiwa kupunguza umaskini wa kipato kwa asilimia 26.4.
Aidha watumishi 306, 917 wamepandishwa vyeo na kwamba Serikali ilifanikiwa kupunguza madeni ya Sh bilioni 472.6 yakiwemo ya mishahara Sh bilioni 14.5 na yasiyo ya mishahara Sh bilioni 358.1.
SEKTA YA ELIMU
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imetumia Sh trilioni 1.9 kutoa elimu bila malipo huku mikopo ya elimu ya juu ikiongezeka kutoka Sh bilioni 348.7 (2014/15) hadi kufikia Sh bilioni 450 (2020/21).
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli uandikishaji darasa la kwanza umeongezeka kutoka wanafunzi milioni 1 hadi milioni 1.6, wanafunzi msingi wakiongezeka kutoka milioni 10.2 hadi milioni 12.6 na wale wa kidato cha kwanza hadi cha nne wakiongezeka kutoka milioni 1.6 hadi milioni 2.1.
Anasema pia shule mpya za msingi zimejengwa 905, za sekondari 73, mabweni 253, maabara 227 pamoja na ununuzi wa madawati zaidi ya milioni 8.
“Mafanikio haya yote yasije yakavurugwa, tupeni tena miaka mitano tukayaendeleze,” anasema Dk. Magufuli.
AFYA, MAJI, UMEME
Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya ni pamoja na kupungua kwa vifo vya watoto wachanga kutoka 25 hadi 7 kwa kila vizazi hai 1,000 na kupungua kwa rufaa za nje.
Mengine ni kujengwa kwa zahanati mpya 1,198, vituo 487, hospitali za wilaya 99, hospitali za mikoa 10, hospitali za rufaa katika kanda 3, kuajiri watumishi wa afya 14,479, kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 31 hadi kufikia Sh bilioni 270, magari ya kubebea wagonjwa 117 na kuimarisha matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo, figo, ubongo na kansa.
Aidha miradi ya maji 1,423 imekamilishwa na mingine inaendelea kutekelezwa sehemu mbalimbali nchini ikiwemo ya kupeleka maji katika miji 28 inayotekelezwa kwa Sh trilioni 1.2.
Gharama za kuunganisha umeme zimepungua kutoka Sh 177,000 hadi Sh 27,000 hatua iliyowezesha kusambaza umeme katika vijiji 9,570 kutoka vijiji 2,218.
Aidha mradi wa Kinyerezi 11 unatarajiwa kuzalisha megawati 240 huku ule wa Kinyerezi 1 ukitarajiwa kuongeza megawati 325 kutoka 190 za sasa.
USAFIRI
Dk. Magufuli anasema wamejenga kilomita 3,500 za lami na kwamba kilomita 2,200 zinaendelea kujengwa sambamba na madaraja 13.
“Kazi zote hizi tulizomaliza na zingine zinazoendelea zimetufanya tuje tuwaombe kura ili tusije tukamuachia mtu mwingine ambaye hajui hata kutafuta nondo,” anasema Dk. Magufuli.
Kwa upande wa reli alisema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaendelea vizuri na kwamba Jumatatu wiki hii walitangaza zabuni ya ujenzi wa Mwanza – Isaka.
Akizungumzia usafiri wa majini anasema wameboresha bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa kupanua bandari zake sambamba na kukarabati na kujenga meli 5.
“Nina uhakika baada ya kazi kubwa hii tuliyoifanya kwa miaka mitano tutaanza kufaidi mavuno ya meli tulizozijenga, barabara, reli, ukarabati na ujenzi wa viwanja tunavyovijenga na ndege tunazonunua,” anasema Dk. Magufuli.
MGOMBEA MWENZA
Mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, anasema miaka mitano iliyopita wameweza kutekeleza kwa kishindo yale waliyoahidi na kwamba kishindo hicho kitaendelea kwa miaka mingine mitano.
“Tumeweza kufanya kwa kiwango cha kutosha, tumeweza kutekeleza kwa kishindo kwa maana hiyo kishindo hiki lazima kiendelee.
“Yote ambayo hatukuyamaliza tutakwenda kuyatekeleza na tuelewe kwamba tukisema tunatekeleza.
“Kampeni tuzifanye kwa amani na utulivu, kwa heshima na kuomba kura kwa wananchi,” anasema Samia.
DK. MWINYI
Mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, anasema atafanya kazi ya kuendeleza pale alipoishia Dk. Ali Mohamed Shein kwa kasi zaidi.
“Kazi yetu mwaka huu itakuwa nyepesi kwa sababu pande zote mbili za Muungano ilani ya CCM imetekelezwa vizuri sana, inatupa kila sababu katika uchaguzi huu wagombea wa CCM wote kupita kwa kishindo na hilo hatuna shaka nalo.
“Lazima sote kwa umoja wetu tuhakikishe kwamba siku ya uchaguzi tunajitokeza kwa wingi kupiga kura na bila shaka tutashinda kwa kishindo,” anasema Dk. Mwinyi.
DENI LA KURA
Baadhi ya wagombea wa chama hicho katika majimbo mbalimbali wanamhakikishia Dk. Magufuli kuwa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya wana deni kubwa la kumpa kura.
Mgombea ubunge Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, anasema maamuzi ya kuhamishia Serikali Dodoma yamebadili maisha ya jiji hilo na uchumi umezidi kukua.
“Tulizoea hoteli kujaa wakati wa mkutano mkuu wa CCM na vikao vya Bunge, leo zinajaa wakati wote.
“Mwaka huu kura zinamwagika tutahakikisha unapata nyingi, ndugu zangu wa Dodoma aliyofanya Magufuli kama ninyi hamtasema mawe yataongea,” anasema Mavunde.
Kwa upande wake Japhet Hasunga (Vwawa), anasema watapambana usiku na mchana kuhakikisha mambo yaliyofanywa na Dk. Magufuli yanaendelea kwa miaka mitano mingine.
“Tutachapa kazi usiku na mchana kuhakikisha Watanzania wanamuelewa na Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kubaki madarakani.
“Tutainadi Ilani yetu ambayo ina mambo mengi makubwa na muhimu hasa ya sekta ya kilimo na nyingine, ni imani yangu CCM kitashinda kwa kishindo na kuendelea kuongoza dola,” anasema Hasunga.
Naye Dk. Ashatu Kijaji (Kondoa), anamshukuru Dk. Magufuli kwa ujenzi wa vituo vitano vya afya ambavyo pia vinatoa huduma ya upasuaji kwa wajawazito na kumhakikishia kuwa watampa kura zote.
Mgombea Viti Maalumu Dodoma, Fatma Tawfiq anasema; “Kura za wanawake na wakwe zetu wote utazipata kwa sababu mambo mengi sana umetufanyia, tutaongea na waume zetu, watoto wetu na ndugu zetu.