27.5 C
Dar es Salaam
Friday, July 1, 2022

Wagombea 1,000 waliokatwa Chadema wakusanyika Dodoma

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA

ZAIDI ya wagombea ubunge na udiwani 1,000 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wapo jijini hapa wakisubiria hatma yao kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutokana na kukata rufaa mara baada ya majina yao kukatwa katika nafasi walizogombea.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, alisema Dar es Salaam jana kuwa wamepokea rufaa 557 kwenye ubunge na udiwani na zilianza kufanyiwa kazi jana katika maeneo yote nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wagombea hao jana, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Susan Kiwanga ambaye aligombea Jimbo la Mlimba, alisema wanashangaa NEC kukaa kimya wakati wamepeleka rufaa zao.

“Mimi nimesimama kwa niaba ya wanawake, wanawake wengi tuliingia katika uchaguzi ili tuwawakilishe wanawake wenzetu, lakini imekuwa kinyume.

“Huu ni moto wanautengeneza, katika majimbo yetu sisi tupo tayari kwa lolote, sipo tayari kuomba haki, nipo tayari kuipigania, sisi msitujaribu, hatupo tayari kujaribiwa.

“Niwaambie Tume hali ya kule majimboni ni tete sana ni muhimu majibu yakatoka. Mimi nashangaa hawa wakurugenzi mpaka leo wanahesabika ni wasimamizi wa uchaguzi, wanatakiwa waondolewe, wanaenda kuhatarisha amani, haki itadaiwa mpaka siku ya mwisho,” alisema Kiwanga.

 Naye, aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, alisema yeye hajakatwa, lakini yupo Dodoma kuhakikisha waliokatwa hatma yao inajulikana kutoka NEC.

“Hatuifundishi tume kufanya kazi, lakini sisi ni wadau wa uchaguzi, tunayo haki ya kutoa mawazo yetu kwa sababu wao hawakuwepo kwenye majimbo huku chini, sisi kama ni dhuluma gani ilifanyika kwa wagombea wote zaidi ya 1,000 wapo Dodoma wakifuatilia.

“Baada ya kuishiwa pumzi tupo hapa tunaitaka tume ieleze majibu ya rufaa zetu, lakini tunaitaka tume ituambie tunashangazwa na maelezo kwamba majimbo 18 wamepita bila kupingwa, hii maana yake ni nini kwa sababu majimbo haya ni kati ya 57 ambayo rufaa zipo kwao.

“Kulikuwa kuna wagombea wa vyama kadhaa sio Chadema tu, kulikuwa kuna wagombea wa CUF na vyama vingine, tunashangaa kuona majimbo wamepita bila kupingwa.

“Mimi sijaenguliwa, lakini nipo hapa kwa sababu wameengua madiwani 16 kati ya 36 hii maana yake wanataka kuleta ujanja ujanja tunasema hiki kitu hakikubaliki, wagombea wetu wamekatwa kihuni.

“Kuna sehemu ya kujaza chama cha mtu, ambaye amemalizia Demokrasia na Maendeleo ameenguliwa na aliyeandika kifupi Chadema amekatwa, huu ni uhuni mkubwa,” alisema Sugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,419FollowersFollow
544,000SubscribersSubscribe

Latest Articles