Na JOSEPH LINO
KUFANIKIWA kuhitimu elimu ya juu ni jambo la heri, ambalo kila mtu mpenda maendeleo hutamani kulifikia. Safari ya kuhitimu chuo kikuu ni ndefu, ina changamoto za hapa na pale na imejaa kumbukumbu za maisha.
Ukiwauliza wasomi wengi waliopitia maisha ya chuo, watakwambia mambo mengi ambayo waliyafanya na sasa wanayajutia. Kama ingetokea wakapata fursa ya kurudi tena chuoni, basi wangejitahidi kuyarekebisha na kufanya kwa ufanisi wa hali ya juu tofauti na awali.
Wahitimu wengi wanapokuwa chuoni mara nyingi husahau masomo na kufanya mambo yasiyofaa ambayo kwa namna moja au nyingine huwafanya wajutie kupoteza muda wao.
Jambo muhimu kwa sasa ambalo wahitimu wanapaswa kulifanya ni kuwashauri wanafunzi waliowaacha chuoni au wale wanaotarajia kujiunga na vyuo kujali zaidi masomo na kwamba mambo mengine yatafuata baadaye.
Haya ni baadhi ya mambo mbayo wahitimu wengi hujutia baada ya kumaliza elimu ya juu.
Kuchagua taaluma mbaya
Wanafunzi waliohitimu huishia kufanya kazi ambazo hawakuzitarajia au si taaluma waliyosomea.
Mara nyingi huwa hawaridhishwi na kitendo cha kufanya kazi wasiyoisomea, hii inawafanya wajutie au kufikiria kwamba hawakufanya chaguo sahihi wakati wa kuomba kujiunga na vyuo.
Changamoto za ajira kwa wahitimu hutokana na kukosekana kwa fursa za ajira, hali ambayo huwafanya vijana wengi kufanya kazi hata zile wasizozipenda.
Wasomi siku hizi wanashauri wanafunzi kufanya utafiti wa kina kabla ya kuchagua taaluma ya kusomea, wakijiridhisha ndipo wafanye uamuzi.
Hata hivyo, kuchagua taaluma kulingana na upatikanaji wa ajira ni jambo baya kwa sababu mhusika unakwenda kufanya jambo ambalo hujalipenda ila kutokana na uhaba wa ajira wa kile unachokipenda inakulazimu kubadili fani ili usihangaike kutafuta kazi pindi watakapohitimu.
Njia mojawapo ya kuwa na furaha ni pale mhitimu anapofanikiwa kupata ajira inayohusiana na mahitaji ya taaluma yake.
Uhusiano
Wanafunzi wengi wanapokuwa vyuoni hujikita katika masuala ya kimapenzi, ambayo kwa namna moja ama nyingine huishia njiani – si ya kudumu. Baada ya kuachana hujikuta wakijuta kwa sababu wakati mwingine huwaharibia malengo yao ya baadaye.
Kwa wale ambao hawakuwa katika uhusiano wa kimapenzi hujutia kukosa fursa hiyo ambayo huenda ingewafanya wapate wenza wa maisha, jambo ambalo wakati mwingine huwa ni la kubahatisha.
Mambo haya yote hutokea kwa sababu ya uhuru wanaokuwa nao wanavyuo, wengi hufanya mambo ambayo pengine wakiwa majumbani kwao hawawezi kuyafanya.
Kutosoma kwa bidii
Kwa mujibu wa wanasaikolojia, jutio kubwa kwa vijana wengi ni kuhusu suala la elimu, wanaamini kuwa kama wangejikita kwenye masomo ipasavyo maisha yao yasingekuwa kama yalivyo sasa.
Huamini kuwa elimu humfanya mtu haeshimike, kujengewa nidhamu ya kutosha katika familia, uhusiano, kipato na afya.
Wahitimu wengi hujihisi kuwa wanakosa vitu vingi ambavyo kama wangesoma kwa bidii leo hii yasingewasumbua. Wengi wao hujutia uzembe wa kutosoma kwa bidii na kupoteza muda katika starehe.
Kukosa mtandao wa marafiki
Wengi wao wanajutia kushindwa kutengeneza mtandao wa marafiki wa kudumu. Hii ni kwa sababu mtandao wa marafiki ni kitu muhimu pindi unapokuwa chuoni na baada ya kuhitimu masomo. Wakati mwingine marafiki husaidia hasa katika kipindi cha kutafuta ajira uraiani.
Mikopo ya chuo
Benki ya Citizens ya nchini Marekani ilifanya utafiti kwa wanafunzi wa zamani wa chuo na kubaini kuwa asilimia 77 ya wahitimu wanajutia kwa kushindwa kutumia vizuri mikopo wanayoipata wakiwa chuoni. Jambo hili huwasababishia msongo wa mawazo na hofu pindi wanapomaliza na hivyo kuwafanya watafute ajira kwa haraka zaidi ili kurejesha fedha hizo ambazo kwa namna moja au nyingine hazikuwasaidia sana kwa kuwa walijikita zaidi katika starehe.