30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOMLEA KIJANA CHIPUKIZI

Na CHRISTIAN BWAYA


KIJANA chipukizi ni mtu aliye katikati ya utoto na utu uzima. Huyu ni kijana ambaye bado tunasita kumwita mtoto kwa sababu anaonekana kukomaa zaidi ya watoto wengine lakini pia hatumuweki katika kundi la watu wazima kwa sababu kuna mambo bado hayajamfisha huko.

Tunazungumzia mtu aliye kati ya umri wa miaka 12 hadi 19.  Katika umri huu, kijana huyu hukutana na mabadiliko makubwa ya kimwili yanayochochea mabadiliko katika maeneo mengine ya maisha yake kama vile ufahamu, hisia na uhusiano wake na watu wengine.

Kwa kawaida, mabadiliko haya huanza na ongezeko kubwa la homoni za kijinsia zinazofanya kazi  ya kutengeneza tabia za kiume au za kike. Tabia hizi za kijinsia si tukio linalokuja kirahisi. Ikiwa hataandaliwa vyema, kijana huyu hujikuta hana la kufanya zaidi ya kushangazwa na mabadiliko ya kasi anayomfanya ajiulize maswali yasiyo na majibu ya moja kwa moja.

 

Nimekuwa tofauti?

Mabadiliko ya kimwili humfanya kijana aanze kuamini kuna kitu kinamtofautisha na wadogo zake, labda, sauti yake imeanza kukwaruza, uso wake unaota chunusi, kifua chake kinaanza kutanuka na kidevu chake kinaanza kuota ndevu.

Kwa msichana, hali kadhalika, naye anaanza kuona tofauti yake na watoto wa kike. Umbo lake linabadilika, ngozi yake inaanza kuwa nyororo sambamba na kuota chunusi na kuanza kuoa kwa maziwa kifuani mwake. Hali zote hizi kwa pamoja zinaweza kumfanya akakosa amani hasa kama anazungukwa na wenzake ambao bado hawajaanza kuona mabadiliko hayo.

Mzazi ana wajibu wa kukaa na mtoto mapema mara anapoona dalili hizi. Mazungumzo ya kirafiki yanayolenga kumwandaa kijana chipukizi na mabadiliko hayo makubwa ni jambo la msingi hasa kwa sababu yanaambatana na tamaa ya kuwa na marafiki wajinsia nyingine. Mzazi anapomsaidia kijana chipukizi kuelewa kinachoendelea mwilini mwake na namna ya kukabiliana vyema na mabadiliko hayo, anamsaidia kuwa kijana shujaa baadae.

Kinyume chake, yaani usiri na hofu ya kuzungumza mambo haya inaweza kusababisha matatizo makubwa hasa kwa sababu kijana huyu chipukizi anajiuliza swali lifuatalo,

 

Mimi ni nani?

Swali hili linatokana na kujifananisha na watu wazima wanaomzunguka. Tayari anaanza kujiona na yeye ni mtu mzima kwa sababu anaona sifa ambazo alizoea kuziona kwa watu wazima wanaomzunguka.

 

“Mimi ni nani?” ni swali linalolenga kujipambanua na watu wengine wanaomzunguka. Anatamani si tu kujua anafananaje na watu wazima waliomzunguka, bali kuelewa anatofautianaje na watu wazima aliozoea kuwaiga.

 

Shauku ya kuwa tofauti ni kubwa kuliko kufanana na anaowafahamu. Kijana huyu anaanza kujitafiti kujua namna gani mitazamo yake inaweza kumpambanua na mzazi wake; namna gani anaweza kufikiri tofauti na mzazi wake; na kwa kiwango gani ameanza kuwa mtu mzima.

 

Kwa vijana wengi chipukizi, maswali haya hawayaulizi hadharani. Wanajiuliza kimya kimya. Maswali haya yasipojibiwa, na ikiwa watahisi hawapewi hadhi ya utu uzima wanayoitaka, huanza kujenga namna fulani ya uasi dhidi ya mamlaka ya wazazi. Huanza kutafuta watu wengine wanaoamini watawafanya wajisikie nao ni watu wazima.

 

Mzazi ana wajibu wa kuhakikisha kijana huyu chipukizi anajisikia mtu mzima anayestahili staha. Ingawa hata mtoto hutarajia kuheshimiwa, kijana chipukizi hutafsiri staha kama kusikilizwa kwa mawazo yake na kupewa kiasi fulani cha uhuru walionao watu wazima wengine.

 

ITAENDELEA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles