26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo muhimu ya kuzingatiwa

 MWANDISHI WETU– DAR/DODOMA

HATIMAYE wanafunzi wa vyuo vikuu na kidato cha sita kukaa siku 74 nyumbani, ikiwa ni hatua ya kujikinga na ugonjwa wa corona, leo wanaanza rasmi masomo yao, huku masharti ya kujikinga yakizingatiwa.

Itakumbukwa Machi 17, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kufungwa kwa shule, vyuo, kusitisha warsha mbalimbali pamoja na michezo, ikiwa ni siku chache baada ya ugonjwa huo kuthibitishwa kuingia nchini.

Wakuu wa vyuo mbalimbali waliliambia gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, kuwa maandalizi yamekamilika

UDOM

Akizungumza na MTANZANIA jana, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma,(UDOM), Profesa Faustine Bee alisema maandalizi yote yamekamilika.

Profesa Bee alisema anauhakika wanafunzi wote watamaliza vizuri masomo yao na chuo kimefanya maandalizi ya kutosha, ikiwemo kujikinga na ugonjwa wa corona.

Aliwataka wanafunzi kuzingatia uvaaji wa barakoa wanapokuwa maeneo ya chuo.

Alisema wanafunzi ambao wanatashindwa kujisajili, wanatakiwa kuendelea na masomo huku taratibu za kujisajili zikiendelea mara baada ya kutoka katika vipindi.

“Watakaoshindwa wataendelea na shughuli za usajili wakati masomo yakiendelea na ninauhakika wenzetu benki za biashara, watatusaidia katika mchakato huu vijana wajitahidi hasa yale yanayowahu ikiwemo kujaza fomu.

“Chuo Kikuu cha Dodoma kimepokea pia maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya ya namna ya kujikinga na ugonjwa huu,maelekezo haya yametolewa kwa nchi nzima, katika maagizo hayo ni pamoja na kuzingatia usafi,katika maeneo yetu yote tutakuwa na maji tiririka, pamoja na sabuni, la pili ni kuvaa barakoa.

“Nitumie fursa hii kuwaomba vijana wetu wawe na barakoa zinazokubalika, zinazoweza kuwakinga, na pale maji yanapokuwa hayapatikani, wawe na vitakasa mkono. Tunaamini hakuna mwanafunzi au mtumishi atakaeugua,” alisema Profesa Bee.

Gazeti hili, limeshuhudia mamia ya wanafunzi mwishoni mwa wiki stendi ya mabasi ya Nzuguni kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa wakiingia na kutoka, ikiwa ishara wanafunzi wengi wameishawasili kwa ajili ya kuanza masomo leo.

Katika eneo la Chuo cha Biashara (CBE) Makole ambako ndiko abiria wa kutoka mikoani huwa wanashukia, kulikuwa na watu wengi huku wengi wakiwa na mabegi.

Mkoa wa Dodoma kuna vyuo vya Elimu ya Biashara (CBE) ST John,Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo) Chuo cha Mipango,Chuo cha Ualimu Capital na Udom

UDSM

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye alisema maandalizi yote yamekamilika, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kuanza kusoma kwa makundi ili kuepukana na ugonjwa wa corona

“Tumejipanga vizuri tangu tulipopewa maelekezo na wizara, tangu Mei 27, wanafunzi wengi wamefika kukamilisha taratibu za kujisajili.

“Wapo wale wanaonufaika na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, wanaendelea na taratibu za kuhakikisha wanakamilisha masomo, tunapenda kuna kila mwanafunzi anarudi na kuendelea na masomo yake kama kawaida,”alisema.

Kuhusu walimu, alisema wapo ambao walikuwa likizo, tayari wameitwa wote kurudi kazini ili kuhakikisha wanafunzi wanafidia masomo yao baada ya kuyakosa.

“Kuna walimu walikuwa likizo, tumewaita warudi ili kuanza kesho (leo), tunngependa kuona masuala yetu ya taaluma yanaendelea kama kawaida,”alisema.

Alisema kutokana na mabadiliko hayo, sasa watafundisha wiki 12 badala ya 13 katika viwango na ubora ule ule ambao umekuwa ukitolewa miaka yote.

“Tutafundisha wanafunzi wetu wiki 12 badala ya 13 ili kuhakikisha zile mada ambazo wanapaswa kuzisoma wanazisoma kwa wakati, walimu wako tayari,”alisema.

Kuhusu ugonjwa wa corona, Profesa Anangisye alisema wamejiandaa vizuri na kuwataka wanafunzi kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa.

“Tumejipanda vizuri kukabiliana na ugonjwa huu, tumeweka sehemu za kunawia mikono, tumetengeneza barakoa za kisasa mno ambazo moja inauzwa shilingi 2,500.

“Hapa chuoni asilimia 90 watu wote ni watu wazima, hatuna mtu ambaye yuko chini ya miaka 18, sasa kila mmoja anatambua umuhimu wa kuvaa barokoa, kunawa mikono na mambo mengi…ni mategemeo yetu watazingatia,”alisema.

Taarifa zaidi zinasema, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha jana alitembelea UDSM kwa ajili ya kukagua maandalizo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alipiga marufuku kwa vyuo na shule kutoza ada mara mbili kwa wale ambao walikuwa wamemaliza karo ya muhula.

Pamoja na hali hiyo waziri huyo amepiga marufuku michango yote isiyo kwenye utaratibu ikiwa ni pamoja na kuagiza wanafunzi waende na malimao na tangawizi akisema corona isitumike kama fursa ya kujipatia fedha.

Mei 21, Rais Dk. John Magufuli, alitangaza kufungua vyuo vyote nchini na kidato cha sita Juni mosi, mwaka huu ikiwa ni baada ya kupungua kwa maambukizi ya corona.

Itakumbukwa Machi 17, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kufungwa kwa shule, vyuo, kusitisha warsha mbalimbali pamoja na michezo ikiwa ni siku chache baada ya corona kuthibishwa kuwa imeingia nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Profesa Ndalichako, alitaka watu aache kutumia corona kama kitega uchumi na kuonya wale ambao wanaanza kuagiza wanafunzi kutoa michango ya ziada.

“Watu wanaanza kuagiza hela za ziada, za kazi gani? wanafunzi walikuwa wameshalipa ada kabla ya kufunga shule, walienda nyumbani kwasababu kulikuwa kuna changamoto ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (homa kali ya pamafu).

“Sasa baada ya kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali hali ya maambukizi imepungua, Serikali imeona kwamba inaweza ikafungua shule na taasisi (wanafunzi) wanakwenda kuendelea pale walipoachia kwa fedha zao zilezile walizolipa, hakuna malipo ya ziada.

“Kwa hiyo nitumie nafasi hii kukemea shule ambazo zinataka kutumia corona kama kitega uchumi, hapa hakuna kitega uchumi. Kama taifa tumeunga pamoja, tumeweka na maombi Mungu wetu ametusikia sasa tusianze kuumizana kwasababu ambazo hazina msingi wowote.

“Wizara itafuatilia shule ambazo zinataka kutumia corona kama kitega uchumi, kuweka michango ambayo haina uhalali wowote, wizara itachukua hatua ikiwamo hata kuzifutia shule usajili kwasababu tumekuwa tunawaambia kila mara watu wanaoendesha shule wanatoa mafunzo kwa Watanzania, wasiwe na ile roho ya kukomoana.

“Sasa imekuja changamoto ya corona watu wanaona ni fursa, hili jambo halikubaliki, naomba niwasisitize wale wanafunzi ambao walikuwa hawajakamilisha ada zao hao ndiyo wafanye malipo ili kuziwezesha shule kufanya kazi yao vizuri.

“Kwa hiyo hapa kuna pande mbili, wale ambao walikuwa hawajakamilisha malipo ya ada wakamilishe ili shule ziweze kufanya kazi yao vizuri, lakini wale ambao walikwisha kamilisha na walifunga kwa sababu kulikuwa na tatizo, warejee shuleni kuendelea na masomo kama vile ambavyo waliachia bila kuwa na michango ama ada za ziada,” alisema Prof. Ndalichako.

MWONGOZO

Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ilitoa mwongozo ambao unalenga kuweka mazingira wezeshi ya kudhibiti maambukizi ya corona katika taasisi za elimu.

Mwongozo huo, umezingatia maeneo makuu manne ambayo ni maandalizi ya mazingira ya taasisi ya elimu kabla ya shule kufunguliwa, uchunguzi wa afya, usafiri wa kwenda na kurudi na mazingira ya kujifunza.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema wamezingatia utoaji wa elimu ya corona shuleni, vyuoni, ikiwemo dalili na hatua za kuchukua ili kujikinga.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais Tamisemi na wizara zote zinazosimami vyuo na taasisi elimu wanatakiwa kuhakikisha uwepo salama ya shule, vyuo na taasisi kabla ya wanafunzi kurejea ili kudhibiti maambukizu ya Covid-19.

“Moja ya maandalizi ni kutakasa mazingira yote ya shule, chuo au taasisi kwa kuzinagatia miongozo ya utakasaji iliyotolewa na Wizara ikihusisha taasisi ambazo zilitumika kutunza washukiwa au wagonjwa wa corona.

“Kuhakikisha kuwepo kwa vifaa vya kunawa mikono yenye maji tiririka na sabuni katika kila eneo la shule au vyuo,uongozi wa shule uhakikishe kuwa unavitakasa mikono yenye ubora unaotakiwa kwa wanafunzi na wanavyuo,” alisema Waziri Ummy.

Kutokana na hali hiyo aliutaka uongozi wa shule na vyuo kuhamasisha wanafunzi, waalimu na wafanyakazi kuvaa barakoa za vitambaa huku wazazi wakichukua jukumu la kuwanunulia watoto barakoa hizo.

“Shule, vyuo na taasisi vyenye vituo vya kutolea huduma za afya watumishi wapewe elimu ya kuwahudumia wanafunzi, waalimu na wafanyakazi watakaoshukiwa kuwa na Covid-19 ikiwemo kuwapa msaada wa kisaikolojia na kuondoa unyanyapaa.

“Shule za bweni zihakikishe kuwepo kwa nafasi kati ya kitanda kimoja na kingine na kudhibiti uchangiaji wa vifaa,uongozi uhakikishe utaratibu mzuri wa upatikaji wa barako na unapaswa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kuhifadhi taka zinazotokana na barakoa,” alieleza .

Alisema wanafunzi wanaohisiwa kuwa na dalili za Covid-19 wafanyiwe vipimo kabla ya kurudi shule au vyuoni huku watakaobanika kuwa na maambukizi wabaki nyumbani hadi afya zao zitakapo imarika.

“Kwa wanafunzi watakaobainika kuwa na dalili wakiwa shuleni uongozi wa shule, chuo utoe taarifa kituo cha afya kilicho karibu,” alisema

Katika mwongozo huo, Waziri Ummy, aliwataka wamilikiwa wa magari za shule kuweka vitakasa mikono na kuhakikisha wanafunzi wamevaa barakoa za vitambaa na kutumia vitakasa mikono kabla ya kupanda gari.

Waziri Ummy pia aliwataka wataalamu wa afya wa mikoa na halmashauri kushurikiana na uongozi wa shule au chuo kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya barakoa, hatua za unawaji mikono na utumiaji sahihi wa vitakasa mikono.

“Uongozi wa shule unapaswa kuhimiza kanuni za usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara katika kila eneo muhimu aidha vitakasa mikono zinaweza kutumika kama mbadala.

 “Uongozi wa shule au vyuo uhakikishe kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu, kuzingatia matumizi ya Tehama wakati wa kufundisha ili kupunguza uwezekano wa maambukizi,”alisema Ummy .

Aliwataka wataalamu wa afya wa halmashauri zote nchini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara shuleni, vyuoni na katika taasisi za elimu ili kuhakikisha tahadhari zote zinazingatiwa.

Alishauri kuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wanafunzi na waalimu wenye magonjwa ya moyo, selimundu na magonjwa ya mfumo wa hewa kama pumu kutokuvaa barakoa.

“Kwa shule na vyuo vyenye wanafunzi wenye mahitaji maalum, waalimu wanapaswa kuvaa barakoa maalum zitakazoruhusu mwanafunzi mwenye matatizo ya usikivu kuwasiliana na mwalimu,” alibainisha.

Alisema mwongozo huo utakuwa ukiboreshwa mara kwa mara ili kukidhi nahitaji ya wakati husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles