28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo 30 yaliyomwingiza Trump Ikulu

Donald Trump
Donald Trump

NEW YORK, MAREKANI

DONALD Trump, kada wa chama cha Republican, ameshinda mbio za urais wa Marekani dhidi ya Hillary Clinton. Je, wajua ni mambo gani yalimpatia ushindi mwanasiasa huyo mtata, imani na sera zake kwa wapigakura? Haya ni mambo 30 yaliyompatia ushindi huo.

1. Kuwahusisha Wamarekani wenye asili ya Kiarabu na mashambulizi ya ugaidi

Mara kadhaa Trump amerudia kuwasema watu wenye asili ya Kiarabu kuhusika na shambulizi la kigaidi la Septemba 11, 2001, katika majengo ya kituo cha Kimataifa cha Biashara (World Trade Center), ambalo lilikatisha uhai wa watu 3,000 nchini humo.

Akizungumza na wananchi katika Jimbo la New Jersey, Trump alisema ndege mbili zilizogonga majengo pacha ya WTC (World Trade Center) ziliendeshwa na Waislamu wanaoishi nchini humo. Rais huyo mteule alirudia maneno hayo kwa msisitizo mkubwa.

 1. Misikiti yote inatakiwa kupelelezwa

Trump anaamini Waislamu wanatakiwa kuchunguzwa kisheria kwa madai wanafadhili vikundi vinavyojihusisha na ugaidi. Anasema inatakiwa kuwapo takwimu mpya juu ya shughuli zote za raia wa Kiislamu wa nchi hiyo, na kwamba hajali kama kutakuwa na ulazima wa kutegwa kamera misikitini ili waangaliwe mienendo yao kwa kuwa inaonekana ni majengo ya kisiasa, si ya imani (ibada).

 1. Kuwadhalilisha wanawake kwa mwonekano

Kulingana na video ya mwaka 2005 alipokuwa akihojiwa na Billy Bush, inaonyesha Trump akitoa matamshi ya kejeli na dhihaka, pamoja na kutaja tuhuma mbalimbali za kuwadhalilisha wanawake kijinsia. Katika video hiyo, Trump anaonekana kusema katika moja ya mikutano yake kuna mwanamke hakuwa na mvuto wala kustahili kuwapo kwenye mkutano wake.

Mwanamke mmoja ambaye amewahi kushiriki mashindano ya urembo alimtuhumu Trump kwa madai ya jina baya la ‘kahaba wa jamii’. Ilishangaza kumwona mtu maarufu aliyeshiriki vipindi vya runinga akiwahukumu wanawake kwa mwonekano wao pekee.

 1. Wanawake wenye zaidi ya miaka 35 wamechoka

Kwa mujibu wa ‘audio’ iliyotolewa na kituo maarufu cha runinga cha CNN, imemkariri Trump akisema wanawake wenye umri wa miaka 35 wamechoka na hawana mvuto tena. Trump alisema hayo wakati akizungumzia mvuto wa binti yake, Ivanka pamoja na tabia yake (Trump) ya kujihusisha kimapenzi na wanawake wenye umri wa miaka 30, kwamba ndio umri bora zaidi. Lakini alisema wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 wamechoka, na ndiyo muda wa kuachana nao.

 1. Marekani inatakiwa kufanya doria baharini

Trump alipendekeza matumizi ya mbinu kali za kupambana na kuwahoji magaidi wa ISIS. Trump aliamini mbinu ya kuwateka nyara inayotumiwa na jeshi pamoja na kuwalisha sumu au kuwachinja ili kuwatokomeza.

 1. 6. Kuwatwanga mabomu ISIS

Trump anaamini kuwa njia pekee ya kuwatokomeza ISIS ni kuwapiga kwa mabomu. Anasema hakukuwa na mgombea mwingine mwenye uwezo wa kuchukua uamuzi mzito kama huo zaidi yake. Na kwamba atawadhoofisha magaidi wa ISIS kwa kulipua vyanzo vyao vya mafuta.

 1. Dunia ingekuwa bora kama Saddam Hussein na Mummar Gaddafi wangekuwa madarakani

Trump anaamini kuwa ili kutatua matatizo yanayoikabili dunia ilikuwa jambo bora zaidi kama Saddam Hussein na Muammar Gaddafi wangelikuwepo madarakani. Aliiambia CNN kwamba, anaamini hali iliyopo Libya na Irak ni mbaya kuliko wakati wa utawala wa viongozi hao.

Pia anaamini kuwa Saddam alikuwa kiongozi ambaye alifanya mambo mazuri nchini mwake. “Saddam alikuwa kiongozi mbaya sana, mbaya mno. Lakini unajua nini? Alifanya kazi vizuri sana. Aliwaua magaidi. Hiyo ilikuwa kazi nzuri sana. Viongozi wetu hawakumwelewa vizuri Saddam. Magaidi hawakuongea na Saddam. Ni kipigo tu.”

 1. Kujenga ukuta wa kutenganisha Mexico na Marekani

Trump anataka kujenga ukuta mkubwa ambao utazitenganisha Marekani na Mexico. Mwanzoni mwa kampeni zake, Trump alisema raia wengi wa Mexico wanaoingia Marekani ni wahalifu.

“Wanakuja hapa na dawa za kulevya, na kutenda uhalifu, pamoja na ubakaji”. Trump anaamini kuwa ukuta huo hautawafukuza wahamiaji kutoka Mexico pekee, bali hata wale wanaotokea Syria hawataruhusiwa kuingia Marekani. Katika ujenzi wa ukuta huo anaamini Serikali ya Mexico inatakiwa kutoa gharama zote. Kwa mujibu wa BBC, gharama hizo ni kati ya dola bilioni 2.2 hadi 13.

 1. Kuwafukuza wahamiaji wote Marekani

Kwa mujibu wa takwimu halisi, inakadiriwa wahamiaji milioni 11 wanaishi nchini Marekani. Trump anataka wahamiaji wote hao wafukuzwe nchini Marekani haraka iwezekanavyo.

Licha ya kukosolewa juu ya mpango huo kwa kuwa unachochea ubaguzi, hata hivyo, taarifa ya BBC inasema Marekani inalazimika kutumia kiasi cha dola bilioni 114 kwa ajili ya kuhudumia wahamiaji.

Aidha, Trump anaamini masuala ya uhamiaji yanatishia uraia wa wananchi waliozaliwa Marekani, hivyo ataanzisha upya sera ya ‘Haki ya uraia” kwa watoto waliozaliwa na wazazi wahamiaji haramu bila kujali kama wamezaliwa nchini humo. Haungi mkono mkakati mpya wa kutoa uraia kwa wageni wenye kuingia kwa kigezo cha kufanya kazi.

 1. Waislamu hawatakiwi kuishi Marekani

Kwa mujibu wa taarifa aliyotoa kwa vyombo vya habari mara baada ya shambulizi la kigaidi lililofanyika San Bernardino, California, Trump alisema, “Inahitaji mkakati wa jumla na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia Marekani, kwa kuwa ni mawakala wa magaidi.”

Taarifa hiyo ilizua taharuki na matamshi makali kwa madai ilichochea ubaguzi mkongwe. Kufuatia tamko hilo, Bunge la Uingereza lilipitisha azimio la kumpiga marufuku kuingia nchini mwao. Hata hivyo, Trump alikoleza matamshi yake kwa kudai angefanya uchunguzi maalumu kwa wahamiaji wote walioomba kuingia nchini Marekani.

 1. Kuwafukuza wakimbizi wa kisiasa wa Syria

Trump anaamini kuna ulazima wa kuwafukuza wakimbizi wa kisiasa wa Syria wanaoomba kuingia Marekani. Anasema shambulizi la Paris, nchini Ufaransa limethibitisha kuwa na mkono wa magaidi ambao waliingia nchini humo kwa kigezo cha wakimbizi na kusababisha uharibifu mkubwa, hivyo angepinga kuivuruga Syria.

 1. Kuwekeza katika matibabu ya akili

Ili kupambana na matatizo ya mauaji yanayotokea nchini humo, Trump anaamini njia pekee ni kuongeza uwekezaji katika matibabu ya akili kwa watu mbalimbali wenye uhitaji. Hata hivyo, Trump haamini katika sera ya kuweka masharti magumu ya kudhibiti silaha.

“Serikali haina ulazima wa kuweka masharti magumu ya kumiliki silaha, wapo watu wazuri wanaruhusiwa kumiliki”. Trump anapinga mpango wa kubinya umiliki wa silaha.

 1. Vladimir Putin ni jembe

Trump anamsifu Rais wa Russia, Vladimir Putin kuwa ni jembe katika uongozi. Pia alikosoa uhusiano mbaya uliopo kati ya nchi yake na Russia. Katika mahojiano yake na CNN, Trump alisema: “Bila shaka kabisa natamani kufanya kazi nzuri na Putin. Sidhani kama Marekani itakuwa na aina ya matatizo kama yaliyopo sasa.

14. Kupunguza kodi kwa watu wa kipato cha chini

Trump anaamini ni muhimu kuanzisha utaratibu maalamu wa kodi, ambapo wenye vipato duni kuanzia Dola 25,000 hawatakiwi kulipa kodi. Anasema watu wa aina hiyo hawana cha kulipa. Pia atapunguza kodi ya VAT kwa asilimia 15 na kuziruhusu kampuni kuhifadhi fedha zao nje ya nchi kwa gharama ya kodi asilimia 10 tu.

 1. Kupunguza kodi kwa mameneja na tabaka la kati

Trump anaungana na kada wa Democrat, Elizabeth Warren, ambao wanaamini ni muhimu kupunguza kiwango cha kodi kwa mameneja kulingana na sheria za sasa. Awali walisema mameneja hao hawalipi kodi ipasavyo, lakini baadaye Trump alitangaza kuwapunguzia kodi sambamba na tabaka la kipato cha kati.

 1. China ni mdau wa biashara yenye maslahi

Trump anasema kulingana na masuala yaliyopo, kuna umuhimu wa kuangalia mambo nyeti katika biashara baina yao na Marekani, ili kulinda thamani ya fedha ya dola. Anasema atahakikisha anaizuia China kushusha thamani ya fedha yao (Yen) bila kujali mazingira na viwango vya kazi. Pia kuikataza kuongeza kodi kwa bidhaa za Marekani na kudukua mawasiliano.

 1. Takwimu za ukosefu wa ajira ni za uongo

Trump alisema takwimu rasmi zilizotolewa na Serikali ni kuwa uhaba wa ajira umefikia asilimia 20, wakati hali halisi inaonyesha kuwa ni asilimia 42. Trump aliiponda mamlaka ya takwimu nchini humo kwa madai iliwadanganya wananchi juu ya tatizo la ajira.

 1. Harakati za watu weusi zina matatizo

Katika hali isiyotarajiwa, Trump alibainisha kuwa mmoja wa watia nia ya urais wa Democrat, Martin O’Malley, anatakiwa kuomba radhi kutokana na vitendo vya kundi la Black Lives Matter ambalo limekuwa likipambana na vitendo viovu vya Polisi. Trump anaamini kuwa kundi hilo ni janga kwa taifa. “Nafikiri wanatafuta matatizo tu, hawana kitu kingine,” aliwahi kuandika Trump kwenye mtandao wa Twitter.

 1. Anamiliki utajiri wa dola bilioni 10

Kulingana na taarifa binafsi za kifedha, Trump anamiliki utajiri wa dola bilioni 10, ambapo Bloomberg walitathmini kuwa ni dola bilioni 2, wakati Forbes walisema dola bilioni 4. Hata hivyo, Trump alipinga taarifa zote hizo na kudai anamiliki utajiri wenye thamani ya dola bilioni 10.

 1. Sheria za afya za wazee zifanyiwe mabadiliko

Trump anataka mamlaka ya afya za wazee ifanyiwe mabadiliko makubwa, hususan utaratibu wa kuwasubiri madaktari ambao  umeongeza matatizo kwao, huku sheria ikiweka vikwazo vya kuingilia suala hilo. Anasema maelfu ya wazee waliofariki dunia wanakabiliwa na matatizo ya akili, na misongo ya mawazo. Anasema njia nyingine ni kuhakikisha idadi ya madaktari inaongezwa.

 1. Obamacare ni janga

Trump kama walivyo wanasiasa wengine kutoka chama cha Republican wanaamini mpango wa afya ulioletwa na Obama, Obamacare umesababisha janga nchini humo. Anaamini sheria iliyounda Obamacare, yaani Affordable Care Act, inatakiwa kufanyiwa mabadiliko makubwa kwa masilahi ya wananchi wa Marekani.

 1. Mabadiliko ya Tabia Nchi si janga, ni hali ya hewa tu

Wakati dunia inaaminishwa kuwa mabadiliko ya tabia nchi ni janga linaloiandama, Trump anasema hayo ni mabadiliko ya kawaida ya hali ya hewa. Anaamini dhana ya kulinda anga na maji safi na salama, kama mambo muhimu kwa binadamu. Anapinga mabadiliko ya tabia nchi kuwa janga kwa kuwa mazingira hayazuii kufanya biashara na kuleta ushindani katika soko.

 1. Udalali udhibitiwe

Trump anasema kutakuwa na mpango wa miaka mitano wa kuwazuia maofisa kuacha kazi na kufanya udalali. Anasema lazima iwepo sheria ya kuwapiga marufuku maofisa wote wa serikali kufanya uwakala wa serikali za kigeni, na analiomba Bunge la Congress libadilishe sheria za fedha ambapo za sasa zinavutia maofisa kufanya udalali.

 1. Trump ni mtanashati

Anaamini kuwa yeye ni miongoni mwa watanashati duniani. Kulingana na kitabu chake cha Crippled America, anasema: “Mimi ni mwanamume safi sana. Najiamini na najisifu kwa hilo. Ni mwanamume mtanashati sana”.

 1. Tokyo na Seoul wajenge mitambo ya nyukilia

Trump anaamini kuwa Serikali za Tokyo (Japan) na Seoul (Korea Kusini) zinatakiwa kujenga mitambo ya nyukilia. Lakini alionya isikaribie mafanikio ya Marekani. Anasema mitambo hiyo itasaidia Japan kupambana na Korea Kaskazini ambayo ni taifa korofi.

 1. NATO imejaa makupe

Trump anaamini kuwa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi hauna mpango wowote, kwa sababu Marekani imekuwa ikilipa fedha nyingi kuliko wanachama wengine. Anaamini NATO ni umoja uliojaa makupe.

 1. Madaktari waadhibiwe kwa kutoa mimba

Trump amekuwa akipinga sera za utoaji mimba. Alipozungumza kwenye mahojiano na MSNBC, alisema ni lazima madaktari wote waadhibiwe kwa kosa la kuwatoa watu mimba, hasa kama watafariki dunia.

 1. Kamati Kuu ilipanga kumpinga

Trump aliituhumu Kamati Kuu ya chama cha Republican kuwa ilikuwa na mikakati ya kumzuia asigombeaa urais. Aliita kamati hiyo ya kijinga na kwamba haikutenda haki wakati wote wa kuwania kiti hicho. Alisema kanuni ziliandaliwa ili kumchagua Ted Cruz awe mgombea wa Republican.

 1. Mishahara iongezwe

Trump anaamini ni jambo jema kuongeza mishahara ya kufanya kazi kutoka Dola 7.25 kwa saa inayolipwa sasa.

 

 1. Hillary Clinton alitoa rushwa kwa mwanasheria mkuu

Trump anaamini kuwa Hillary alitoa hongo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Loretta Lynch, kwa ahadi ya kupatiwa nafasi ya kazi endapo angeshinda kiti cha urais, ikiwa ni njia ya kuepuka kitanzi. Anaamini kuwa Hillary pia aliwaangusha wanawake kwa kumtuhumu mumewe kutembea nje ya ndoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles